Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli, Lowassa washiriki kumuaga Mercy Anna Mengi

Sat, 10 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Rais John Magufuli ni miongoni mwa waombolezaji wanaoshiriki ibaada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa mwasisi wa Kampuni za IPP, Mercy Anna Mengi katika Kanisa la Azania Front, jijini Dar es salaam.

Pia, Waziri Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa naye alikuwapo katika shughuli hiyo.

Mercy, alifariki dunia Oktoba 31, 2018 katika Hospitali ya Mediclinic Morningside iliyopo Johannesburg nchini Afrika Kusini, alikopelekwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Jumatano ya Oktoba 17, 2018 Mercy alikwenda Johannesburg katika hospitali hiyo na kulazwa ikiwa ni maandalizi ya kufanyiwa upasuaji.

Alifanyiwa upasuaji Oktoba 17 na kwa bahati mbaya kazi ya upasuaji haikwenda kama ilivyotarajiwa na Mercy hakurudia hali yake ya kawaida hata baada ya kuendelea na matibabu.

Taarifa ya familia iliyosambazwa kwa waombolezaji kanisani hapo imeeleza kuwa ilipofika Oktoba 31, 2018, Mercy alionekana dhaifu kupita kiasi kabla kufikwa na mauti jioni.

Akizungumza kanisani hapo leo, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa amewataka kutumia dakika zilizobakia hapa duniani kuishi katika mapenzi ya Mungu.

"Wapo watu wanaishi kwa heshima kanisani lakini katika jamii hakuna, inabidi kuonyesha maisha ya utakatifu wakati wote, jambo la msingi ni kuongeza uhusiano wetu na Mungu," amesema Dk Malasusa.

Dk Malasusa amesema binadamu wanatumia muda mwingi kutafuta ulinzi wa kiafya kwa njia ya kufanya mazoezi na chakula kizuri lakini si kitu mbele ya kifo.

Mercy alizaliwa Aprili 13, 1948 kijijini Wari, Machame mkoani Kilimanjaro.

Chanzo: mwananchi.co.tz