Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Mafyatu wa yesu’ wanavyoliwa

60954 YESU+PIC

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Namshukuru Mungu. Kweli namshukuru Mungu kwa mema yote anayonitendea. Baada ya kufunga kwa lazima kutokana na ugonjwa wa UMIMFU (Uhaba wa Michuzi Mfukoni) na kusali sana huku nikiangalia kasarafu kalikobaki humu ndani kwa muda wa masaa matatu, nilishtuka nimeanguka chini.

Wengine mnaweza kusema kwamba ilikuwa sababu ya njaa lakini najua nilipigwa chini na fimbo ya Mungu, maana ghafla niliona mwanga mkali huko malaika akishuka na kusimama mbele yangu.

Kwa kweli nilitetemeka kwa hofu lakini malaika akasema kwa sauti ya upole.

‘Wewe Makengeza, Mungu amekuona. Ameona jinsi unavyohangaika na ameamua kukuletea mema wewe kama mtumishi wake. Amesema hivi. Amka ufungue kipakatalishi chako (nilishangaa malaika anajua Kiswahili vizuri hivyo). Ingia kwenye mitandao na kuwatangazia watu kwamba wewe ni mteule wa Mungu. Umeletwa duniani ili kuwafariji mafukara na kuwatajirisha wenye mitobo mfukoni. Umeletwa duniani kunyoosha njia za watu waweze kupata mema katika maisha yao. Wakikutunuku wewe, na wao watatunukiwa. Wakikuzawadia wewe, na wao watazawadiwa mara dufu.’

Niliinama kama ishara ya utii ingawa moyo ulijaa wasiwasi pia.

‘Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema yake yote. Lakini mheshimiwa malaika, watanitunuku vipi?’

Pia Soma

Ghafla nyumba ilitetemeka nikagundua kwamba malaika yule amepiga mguu chini kwa ghadhabu.

‘Labda wewe hustahili huruma ya Mungu. Anakuonesha njia, anakunyooshea njia, kisha ni juu yako kufuata ile njia itakayokufikisha kwenye neema. Kuna kalamu takatifu, kitambulisho kitakatifu, leso takatifu … tumia akili yako uliyopewa na Mwenyezi Mungu.’

‘Lakini serikali …’

‘Wewe hujui neema za Mungu wewe. Hukumbuki serikali ilipotangaza kwamba mpango fulani wa wachungaji ulikuwa ni utapeli, watu wakazidi kumiminika kujiunga? Mungu anawapenda wajasiri wa utukufu si wenye udhaifu wa moyo. Uamuzi ni wako.’

Mara PAAP, malaika akatoweka nikabaki kuangalia sarafu yangu iliyobaki. Harakaharaka nikamkimbilia mke wangu na kumhadithia yaliyotokea na kumwomba anigawie pesa zake za mkopo wa Vicova. Mke akashtuka. Kwanza akanishika paji la uso.

‘Unaumwa mume wangu?’

‘Wewe utamwambiaje mteule wa Mungu anaumwa? Nipe hizo pesa haraka tupate baraka ya haraka kabisa.’

‘Lakini … wenzangu wa Vicoba …’

‘Lakini ya nini? Huwezi kushindana na Mwenyezi Mungu. Shetani mwenyewe alishindwa sembuse yeye. Ukitoa sasa, utarudishiwa mara lukuki.’

Mke wangu akatoa shingo upande lakini sikujali. Ni kama nilikuwa nabebwa na nguvu ya Mungu. Nikakimbia kununua leso, na kalamu na kutengeneza vitambulisho harakaharaka.

Baada ya kuwa tayari niliongea na jirani yangu ambaye mtoto wake alipata divisheni 1 katika mitihani na kukubaliana naye kwamba tutagawana neema ya Mungu watu watakaponunua kalamu zangu za baraka. Nikampigia picha huyu kijana akishika kalamu moja.

Baada ya maandalizi haya, nikakimbilia kipakatalishi changu na kufungua akaunti za @Mafyatu wa Yesu katika kila mtandao. Nikachukua picha ya yule kijana na kuiweka chini ya kichwa:

MAFYATU WA YESU

Chini ya picha niliweka maneno:

‘Asante Bwana Mungu. Asante Nabii Makengeza. Bila wewe nisingepata Divisheni 1. Kalamu ya neema hii.’

Nikaongeza na post nyingine.

‘Msikose neema. Kadiri utakavyomtunuku Mungu, na wewe utatunukiwa.

Shilingi elfu kumi: Divisheni 3

Shilingi elfu thelathini: Divisheni 2

Shilingi laki moja: Divisheni 1.

Msikose nafasi hii ya kuonesha upendo wako kwa Mungu, ili akuoneshe upendo wake pia.

Baada ya hapo nilitangaza huduma ya kupata magari pia. Kila mtu anatakiwa kununua kitambulisho chake cha Kanisa la Mafyatu wa Yesu (MY). Kadiri atakavyotoa pesa kununua vitambulisho atapata gari kubwa zaidi.

Kisha nilitangaza biashara ya leso.

Nunueni leso ili uweze kufuta jasho la wanaoteseka na mambo ya dunia. Leso yako ni leseni ya kufanikiwa sana katika biashara.

Baada ya hapo, nilimaliza kusema.

Njooni kwangu ninyi nyote mnaolemewa na mawazo ya kutajirika ndani ya ufukara, njooni nyote ambao mnapenda kupata utajiri bila jasho, ndiyo ufyatu wenyewe. Njooni mjiunge na Mafyatu wa Yesu mkapate tulizo. Msikose fursa hii.

Baada ya kutuma matangazo hayo, nikatulia na kusubiri. Yaani baada ya muda mfupi majibu yakaanza kumiminika kwa mwendo kasi wa ajabu, kila mmoja akitaka kujua atapataje neema hizo. Ikabidi nitengeneze tangazo lingine.

MAFYATU WA YESU

Mungu anawapenda. Mungu anajua mafyatu ni watu wa kisasa. Hakuna haja kujisumbua kuja kanisani kila wakati. Mimi nabii wake nitawafuata hapo mlipo, tukusanyike, niwaombee kisha nitunukiwe ili Mungu awatunuku.

Kisha nikatoa ratiba kila siku nitakuwa wapi saa za jioni ili niweze kuwawezesha waumini mafyatu. Weeee! Watu walivyokusanyika ikabidi kuongea na polisi na kuwaambia kwamba wao nao watapata neema ya Mungu. Niliwapatia kalamu na leso kwa bei nafuu ili waruhusu mikusanyiko.

Mwezi mmoja, nilikuwa nimeshabadilisha maisha yangu. Tukaongea na waifu na kukubali inabidi kuanzisha sasa Supermarket ya Mafyatu wa Yesu (MY) ambapo watu wataweza kuja kununua vitu vyote ambavyo vitawawezesha kupata neema katika maisha yao. Itaitwa MY Supermarket.

Mungu yu mwema. Karibuni tufyatue kwa ufyatu pamoja.

Chanzo: mwananchi.co.tz