Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maaskofu zaidi ya 8 wamzika Mkapa

Cb7979d84b6f77695d46c487af7192ef Maaskofu zaidi ya 8 wamzika Mkapa

Thu, 30 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAASKOFU zaidi ya wanane wengi wao kutoka majimbo ya mikoa ya Kusini, jana walishiriki ibada takatifu ya misa ya mazishi la Rais m staafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa. Katika misa hiyo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu alitaka msiba huo uwe sababu ya kuongeza umoja wa kitaifa, umoja wa familia, mshikamano na utayari wa kuwatendea wengine mema.

Askofu Mkuu Dallu alisema hayo wakati wa mahubiri ya misa hiyo kwenye uwanja wa makazi ya Mzee Mkapa katika Kijiji Cha Lupaso, Masasi mkoani Mtwara.

Alisema kuwa Mkapa alikuwa mcha Mungu hivyo ili kumuenzi taifa linapaswa kuwa na mshikamano zaidi na pia muungano wa Tanganyika na Zanzibar uimarishwe zaidi na Watanzania wapeane faraja zaidi, badala ya machungu hasa kupitia mitandao ya kijamii.

“Naomba kila mmoja amuone mwenzake amefanya vizuri zaidi kuliko yeye, tukifanya hivyo hatutagombana. Hiyo ndio ilikuwa sera ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kifo cha Mkapa kituunganishe familia kwani Mkapa sasa hivi ana nguvu zaidi ya kuwaombea,” alisema Askofu Dallu.

Askofu Mkuu Dallu alisema ibada hiyo ni zawadi kwa Benjamin Mkapa na ni tafakari juu ya uzima na maana ya maisha aliyopewa mwanadamu, kama zawadi inayohitaji atende mema ili Mungu wakati wa hukumu asiwabague kama mbuzi, bali awaite kama kondoo na kupata taji la uzima wa milele.

Aliwakumbusha waombolezaji kuwa wanadamu ni wasafiri, hivyo waishi na kutenda kwa busara, wasilemazwe na wanayokutana nayo na watumie vizuri muda kwa kuwa na huruma, ukarimu, wema, upole na usafi.

Alitoa mfano wa Mkapa kuwa wakati wa uhai wake, popote alipojiunga na elimu ya juu alikuwa muumini safi wa imani yake.

Askofu Dallu alitoa mfano kuwa katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, Mkapa alijiunga na Chama cha Wanafunzi Wakatoliki chuoni kilichoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema Mkapa kutokana na misingi mizuri ya kiimani aliyokuwa nayo, alifanya toba hadharani kupitia kitabu chake cha My Life, My Purpose na kwamba ni mtu aliyejifunza msamaha na kujikatalia.

Askofu Mkuu Dallu alisema imekuwa jambo jema kwa siku ya jana ya maziko ya Mkapa, kwani katika kalenda ya Kanisa ni siku ya Mtakatifu Matha, ambaye alihangaika sana na kifo cha kaka yake Lazaro na kisha alikutana na Yesu njiani na kuamini kuwa ujio huo utamletea faraja.

Alisema kuwa katika msiba huo wa taifa, kila mtu amuone mwenzake amefanya vizuri zaidi kuliko yeye ikiwa ni hatua ya kumuenzi Mkapa, kwani alipowapa watu kazi aliamini watafanya vizuri zaidi kuliko yeye.

Aliishukuru na kuipongeza serikali kwa kuandaa vizuri tukio hilo na kupeleka maziko katika uongozi wa kikanisa wa Kusini, na nyumbani kwa marehemu kijijini Lupaso.

Ibada hiyo ya Misa ilihudhuriwa na mapadri, watawa wa kike na wa kiume, waumini kutoka maeneo ya mikoa ya Kusini, na iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Kwa upande wa serikali, viongozi mbalimbali walihudhuria wakiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, Naibu Spika Dk Tulia Ackson, wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, mawaziri, naibu mawaziri, viongozi wa kijamii, machifu na waombolezaji.

Chanzo: habarileo.co.tz