Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maaskofu wastaafu waingilia kati sakata la KKKT

Masskofupic Data Maaskofu wastaafu waingilia kati sakata la KKKT

Mon, 4 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) likitoa tamko la kufafanua mgogoro wa Dayosisi ya Konde mkoani Mbeya, baadhi ya maaskofu wastaafu wametoa waraka wa kupinga hatua zilizochukuliwa na uongozi wa kanisa hilo kwa mgogoro huo.

Mgogoro wa Dayosisi ya Konde umekwenda mbali na kufikia hatua ya Mkutano Mkuu Maalumu ulioitishwa na mkuu wa Kanisa, kumuondoa madarakani Askofu wa Dayosisi hiyo, Edward Mwaikali, uamuzi ambao unapingwa na baadhi ya maaskofu.

Maaskofu hao pia wameshangazwa na hatua ya Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kumuondolea hadhi ya uaskofu, Askofu wa zamani, Dk Stephen Munga, wakisema hatua hiyo ni kichekesho.

Waraka wa maaskofu wastaafu

Katika andiko lao hilo, maaskofu hao (majina tunayo) wamezungumzia mgogoro wa Dayosisi ya Konde wakidai kuwa walijaribu kupaza sauti zao kwa namna tofauti kuhusu namna shauri la mgogoro wa Dayosisi ya Konde linavyoendeshwa.

“Tunajua tumezungumziwa mahali fulani katika baadhi ya vikao vyenu, msimamo wetu ukaongelewa kwa lugha na staili ya aina yake. Kama vile Maaskofu wastaafu tuliokosa kazi. Kama ni hivyo, sawa lakini hiyo lugha haitukatishi tamaa,” wameandika.

Advertisement Walisema licha ya kustaafu kazi, bado wana uzoefu mkubwa na wanajua namna bora ya kushughulikia migogoro.

“Kwa hiyo, kama tukijaribu kutoa ushauri wetu kuhusiana na migogoro, kama huu uliojitokeza katika Dayosisi ya Konde na namna ya kuitatua, hatufanyi hivyo kama watu wasiojua au kuelewa lolote kuhusiana na masuala kama haya.”

Katika waraka wao, Maaskofu hao wastaafu wa KKKT wamesema upinzani dhidi ya hatua ya kuhamisha makao makuu ya Dayosisi kutoka Tukuyu kwenda Jijini Mbeya kiuhalisia hautokani na ukiukwaji wa Katiba ya KKKT au Dayosisi ya Konde.

“Hiyo inatumiwa kama kisingizio cha kuendeleza na kuukuza mgogoro ili wahusika wapate au wabaki na wanachokitaka. Kulikuwa na namna bora zaidi ya kushughulikia tatizo hilo, katika roho ya amani na maelewano,” walisema.

Wamesema kuwa wanashangazwa na Mkuu wa KKKT na Kamati iliyoundwa kuchunguza mgogoro huo kukwepa kuzungumzia kiini chake.

Maaskofu hao wamesema kwa kufumbia macho kiini cha sababu za msingi za kuhamishia Jijini Mbeya makao makuu ya Dayosisi ya Konde, iko katika hatari kubwa ya mpasuko wa muda mrefu na kuliathiri kanisa.

Kwa mujibu wa maaskofu hao, itakuwa ni kujidanganya kutumia Serikali kama njia ya mkato kutatua tatizo hilo.

Wametaja sababu mojawapo kubwa ya kuamua kuhamishia makao makuu Mbeya ni kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa wana Dayosisi ya Konde na kwamba siku zijazo kuna haja ya kubadili jina la Dayosisi ili kuleta umoja.

“Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu, lakini halali, kwamba wakati Mbeya ni katikati kwa wana-Konde wote, Tukuyu ni pembezoni mno na mji mdogo tu, nafasi finyu ya eneo la makao makuu.

“Tukuyu ni kwa kabila moja tu hata kama asilimia ndogo sana wanaweza kuwa wanatoka nje ya Wilaya za Rungwe na Kyela, wakati Mbeya ni makao ya watu kutoka makabila mbalimbali ndani na nje ya Nyanda za juu Kusini.

“Inabidi kujiuliza tena na tena, kwa nini katika upinzani unaoendelea sasa dhidi ya kuhamishia makao makuu Mbeya mjini hawamo watu wa makabila mengine yanayounda Dayosisi ya Konde?” wamehoji maaskofu hao.

Wamemtaka Mkuu wa Kanisa la KKKT kuangalia na kujihoji kama alichukua msimamo sahihi katika kushughulikia mgogoro wa dayosisi hiyo.

Wadai katiba Konde imekanyagwa

Maaskofu hao katika waraka huo wamedai waliojitwisha jukumu la kutatua mgogoro huo wanakwepa kufanyika kwa usuluhishi wa dhati kati ya pande mbili zinazotofautiana na badala yake wanachukua njia za mkato kumaliza tatizo hilo.

“Wanatumia njia ya mkato kuitisha Mkutano Mkuu Maalumu usiokuwa na tija, tena wenye kukiuka Katiba ya KKKT-Dayosisi ya Konde Toleo la 2006 na kuikanyaga Katiba ya KKKT kwa makusudi.

“Hata kama makao makuu yangerudishwa Tukuyu sasa, uzito wa mgogoro uliopo sasa utaongezeka mara mbili au zaidi kwa sababu walio wengi karibu robo tatu wanaounga mkono hatua ya kuhamia Mbeya hawatakubali kurudi Tukuyu.

Wapinga Mwaikali kuondolewa

Wastaafu hao wamekosoa Mkutano mkuu ulioitishwa kwa madai kuwa haukufuata utaratibu kumvua uaskofu Dk Edward Mwaikali.

“Hii imemshangaza kila mtu, mtu ambaye alifuata mfumo wa Kanisa na vikao vya maamuzi vya Kanisa anaondolewa kwenye uongozi, badala yake aliyekwenda kinyume na Mungu anapewa nafasi ya uongozi.

“Kumbukeni uchungaji hautolewi na maaskofu, bali unatolewa na Mungu kupitia ninyi maaskofu. Sasa barua ya Mkuu wa KKKT juu ya Askofu Mwaikali inajichanganya sana.

“Maana Mkutano Mkuu bila kupokea tuhuma zake kutoka kwa Halmashauri ya KKKT Dayosisi ya Konde na yeye akapata nafasi ya kujitetea, hauna mamlaka ya kumwondoa kuwa Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Konde hata kama ungependa kufanya hivyo kwa namna yoyote ile.”

Kuhusu Askofu Munga

Maaskofu hao katika waraka wao wamezungumzia pia hatua ya Halmashauri Kuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kumuondoa katika uchungaji askofu wa zamani wa Dayosisi hiyo, Dk Stephen Munga ili kupoteza sifa ya kuwa Askofu.

“Tumesikia pia kwamba Dayosisi mojawapo ya KKKT huko Kaskazini Mashariki imemwondelea hadhi ya Uaskofu Baba Askofu Mstaafu Dk Stephen Munga. Tena kwa kuitumia Halmashauri Kuu. Hicho ni kichekesho mno!” wamesema.

Novemba 2 mwaka jana, Dayosisi hiyo iliwaandikia barua wachungaji, mashemasi na Wakristo wote wa Dayosisi ikiwaeleza maamuzi ya kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya KKKT kilichokaa Oktoba 29, 2021 huko Utondolo, Lushoto.

Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Kaimu Katibu mkuu wa Dayosisi hiyo, Mchungaji Godfrey Walalaze, ilisema kikao hicho kilipitia kwa kina taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Dayosisi kipindi cha 2019 na 2020 na kumvua uchungaji Dk Munga.

Kutokana na hatua hiyo ya kuvuliwa uchungaji ambayo inakwenda kugusa nafasi ya Askofu mstaafu, Dk Munga aliwaandikia barua maaskofu wa KKKT ,kuwa hawezi kutii agizo dhalimu linalojenga juu ya mambo ya uongo, hila na chuki.

Mwananchi lilimuuliza Dk Mungu juu ya waraka huo ambapo alisema anafahamu ungetoka wakati wowote ingawa hakwenda Dodoma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live