Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maaskofu wasisitiza amani, usawa utoaji haki

33315 Pic+maaskofu Maaskofu

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya maaskofu wa makanisa mbalimbali nchini wamewataka Watanzania kudumisha amani wakati wa msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya huku wakiitaka Serikali kusimamia utoaji wa haki kwa watu wote.

Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, aliwataka viongozi wa Serikali kuwaunganisha wananchi bila kujali tofauti za kidini, kisiasa, kiuchumi na kikabila.

“Bwana Yesu alipozaliwa ujumbe wake mkuu ulikuwa ni upendo na amani. Tukishakuwa na amani ndiyo inatupeleka kwenye upendo nayo inatupeleka kwenye mshikamano,” alisema Askofu Kilaini.

“Viongozi wa Serikali wadumishe umoja, sote tuwe kitu kimoja bila kujali imani zetu licha ya itikadi na misimamo yetu. Tushikamane pamoja ili tusukume gurudumu la maendeleo mbele.”

Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo alisisitiza amani na upendo kwa Watanzania akisema ndiyo lengo la kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

“Niwaombe watu wote tusherehekee kwa furaha na amani na kuonyeshana upendo. Yesu alipokuja duniani akazaliwa kwa upendo, hivyo ndivyo tuwatendee wanadamu,” alisema Dk Shoo.

Hivi karibuni Dk Shoo alitoa waraka maalumu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya utakaosomwa leo katika dayosisi zote 26 za KKKT yenye zaidi ya waumini milioni 6.5 nchini.

Ujumbe huo unaeleza jinsi changamoto ya umaskini nchini inavyosababisha manung’uniko na watu kukosa matumaini.

Katika waraka huo, Askofu Shoo amesema jamii imeshuhudia jinsi ambavyo wanawake, watoto, vijana na jamii ya Watanzania kwa ujumla inavyopitia katika changamoto mbalimbali.

“Kwa mfano vipo vitendo vya kikatili kama vile ubakaji, ukeketaji, ndoa za utotoni na ukatili wa kila aina,” amesema Dk Shoo ambaye pia ni askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini.

“Zipo changamoto mbalimbali zinazotokana na umaskini zinazosababisha watu kuwa na manung’uniko na kukosa matumaini. Ujumbe wa Krismasi na Mwaka Mpya utukumbushe sote kutokata tamaa.”

Mbali na Dk Shoo, Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza alisema Yesu alizaliwa wakati Taifa la Israel likiwa limepoteza matumaini chini ya utawala wa Warumi (Italia).

“Yesu alizaliwa wakati Wayahudi wakiwa wamekata tamaa kutokana na utawala wa Warumi. Akaleta matumaini na maisha bora, wakajua kesho itakuwa bora kuliko jana,” alisema Dk Bagonza.

“Hata sasa watu hawana matumaini, wamekata tamaa katika nyanja zote za uchumi, kijamii na kiroho. Kristo aliyefufua matumaini awafufue waliokata tamaa.”

Vilevile aliitaka Serikali kutenda haki kwa wananchi ili kudumisha amani, huku akisisitiza kuwa watu wengi wamekata tamaa kutokana na kukosa haki zao.

“Amani haiwezi kuletwa na vyombo vya dola, bali inaletwa na haki. Haki na amani vinakwenda pamoja. Kilichopo, amani ni utulivu siyo amani. Watu wanakuja kutubu kwetu tunawaona. Sisi tulioko huku vijijini mtu analima mazao yake, halafu mwingine ndiyo anaamua bei,” alifafanua Askofu Bagonza.

Katika waraka alioutuma kwa makanisa ya Dayosisi ya Karagwe, Desemba 3, Dk Bagonza aliwataka waumini kuepuka kiburi cha uzima.

“Tunaonywa kuwa na kiburi cha uzima, kiburi cha madaraka na roho ya kutoshauriwa ili tuepuke anguko. Shoka limeshawekwa shinani, mti usiozaa unyenyekevu mbele ya Yesu Kristo aliyezaliwa utakatwa,” imesema sehemu ya waraka huo.

Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk Barnabas Mtokambali alizungumzia ugumu wa maisha akiwataka Watanzania kuishi kwa amani kwa kuwa nyakati hazifanani.

“Tanzania ni kama nyumba au ni kama familia na wewe unajua hata nyumbani siku huwa hazifanani kwenye familia. Kuna wakati tunakuwa nazo (fedha) na wakati mwingine tunakosa, labda wale matajiri tu. Nashauri tudumishe tu amani hata wakati huu,” alisema Askofu Mtokambali.

“Kitabu cha Isaya (katika Biblia) kinasema aliyezaliwa ni Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele na mfalme wa amani, kwa hiyo tudumishe amani.”



Chanzo: mwananchi.co.tz