Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maaskofu wasisitiza amani Mwaka Mpya

D88491b9f380adee1936bdf75104f580.png Maaskofu wasisitiza amani Mwaka Mpya

Fri, 8 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATANZANIA wameaswa kuendelea kudumisha amani na upendo miongoni mwao na kumuomba Mungu kila wakati ili azidi kuwalinda dhidi ya majanga mbalimbali.

Rai hiyo imetolewa na viongozi mbalimbali wa kiroho katika nyumba za ibada wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya. Walisema kuwa licha ya mambo mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa Covid-19 kuikumba dunia, mwaka wa 2020 ulikuwa na baraka kwa Tanzania.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Azania Front, Chediel Lwiza alisema Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani, ilikumbwa na janga la Covid - 19 lakini kutokana na maombi ya watu wake na kumtanguliza Mungu, limeweza kuepushwa.

“Siyo hiyo tu, mwaka 2020 tulikuwa na Uchaguzi Mkuu, bado Mungu alisimama nasi na tukaweza kuvuka salama katika mchakato huo bila matatizo yoyote,” alisema Mchungaji Lwiza.

Aliwataka watanzania kuendelea kuwa wazalendo kwa taifa lao. Alisisitiza kuwa mwaka huu 2021, wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuliletea taifa maendeleo ambayo Rais John Magufuli amekuwa akiyasisitiza siku zote.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwa'ichi aliwataka Watanzania kuendelea kumuomba Mungu ili azidi kuendelea kulilinda taifa dhidi ya mambo mbalimbali.

Alisema mwaka 2020 ulikuwa wenye changamoto nyingi, ukiwemo ugonjwa wa Covid 19. Alisisitiza kuwa maombi pekee, ndiyo yaliyoweza kulinusuru taifa hili.

“Tumepita katika kipindi kigumu wakati huu ambao nchi zingine duniani bado zipo katika janga hilo, kwa ushuhuda huu inaonyesha wazi Mungu yupo na Watanzania, tunatakiwa kuendelea kumuomba Mungu ili azidi kutupa baraka zake,” alisema Askofu Ruw'aichi.

Alisema Watanzania wanapaswa kumshukuru Mungu, kwa kuwaweka salama katika kipindi chote cha mwaka uliopita na zaidi wanapaswa kuendelea kumuomba ili azidi kutulinda na kuwapa amani.

“Mwaka 2021 pia unaweza kuwa na changamoto zake, ila naamini pia utakuwa na baraka zake, kikubwa tuzidi kumuomba Mungu atupe neema zake wakati wote,” alisema Askofu Ruw'aichi.

Wakati huo huo Wakristo wa Kanisa Katoliki nchini wamekumbushwa maeneo manne muhimu, wanayotakiwa kuyaombea amani wanapouanza mwaka mpya wa 2021 na kuhimizwa kuombea amani ya mataifa, amani ya nchi yao, amani ya familia zao na amani ya nafsi zao.

Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima Jimbo la Geita, Padri Gerald Sengo alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu ya Sikukuu ya Mama Bikira Maria Mama wa Mungu kwa Kanisa Katoliki, iliyoambatana na maadhimisho ya ibada ya shukrani ya sikukuu ya Mwaka Mpya 2021.

“Maadhimisho ya leo (jana) yanatukumbusha kuombea amani katika vipengele mbalimbali ikiwemo amani kwa ajili ya ulimwengu, kwa sababu katika nyakati zetu hizi kuna vita, vita ipo karibu kila mahali, kila bara, kila nchi na tunaomba sasa amani hiyo iweze kupatikana katika mataifa mbalimbali na tunaamini sala zetu ni chachu ya amani.

“Amani tunaiomba pia kwa ajili ya taifa letu la Tanzania. Tumejaliwa kuwa nayo kwa muda mrefu, lakini wapo watu wanaoweza kuwa sababu ya kuvunjika kwa amani, hasa viongozi wenye uchu wa madaraka. Wale wanaotetea nafasi zao na wale wanaotafuta nafasi hizo wanaweza kuwa kisababishi cha kupotea amani hiyo… kwa hiyo tuombe ili amani tuliyonayo iendelee kudumu na tuendelee kuwa kimbilio la mataifa mengine kwani kukosekana kwa amani katika nchi zao, kumewafanya watafute hifadhi katika nchi yetu," alisema.

Padri Sengo alisema amani haiishii tu katika nchi na ulimwengu, badala yake inagusa familia, hivyo ni vyema wasali kuombea amani katika familia, maelewano na msamaha. Alisema tunapoanza mwaka 2021 amani inayotawala ndani ya familia iwe sababu ya amani inayopelekwa kwa majirani, na amani ipatikane kati ya mtu na mtu na kwa familia yote ya Mungu.

“Lakini ili amani iweze kupatikana kote katika mataifa, nchi na familia inapaswa kuanza moyoni mwa mtu binafsi, mtu mwenyewe utakuta ndani ya nafsi yake kuna vurugu nyingi, amani inakosekana katika mioyo yetu kwa sababu labda ya matatizo na magonjwa na mwanadamu akishavurugikiwa yeye binafsi siyo rahisi kuwa chanzo cha amani sehemu nyingine.

“Hata tunapowaalika watu kusherekea kwa amani, tunatambua kuwa yeye mwenyewe mtu binafsi anapaswa kuanza na hiyo amani, akiwa na amani yeye, hata wanaomzunguka wanapata amani, kwa hiyo tunatamani amani ianze katika mioyo yetu, mimi ninapokuwa na amani ninaweza sasa kuifanya ipatikane mahali popote inapotakiwa,” alisema Padri Sengo.

Sista Prisila Simba ambaye ni mtawa anayehudumu katika parokia hiyo, aliwaomba wazazi wakatoliki hasa wanawake wanapoadhimisha sherehe ya mama Bikra Maria na sikukuu ya Mwaka mpya, kukumbuka kuwajenga watoto katika malezi ya hofu ya Mungu ili wawe chachu ya amani ya familia na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini, wametakiwa kuongeza maombi kuiombea nchi ili kuwakinga Watanzania dhidi ya ugonjwa wa Covid 19.

Askofu wa Kanisa la TAG Msufini Mjini Kigoma, Omari Mlenda alisema hayo katika misa maalumu ya Mwaka Mpya iliyofanyika kanisani hapo. Alibainisha kuwa maombi yaliyofanywa na Watanzania ndiyo iliyoifanya nchi kuepuka janga la corona.

Alisema kuwa maoni ya Rais John Magufuli ya kutoa wito kwa Watanzania kufanya maombi maalum kwa siku tatu mfululizo, ndiyo yaliyofanya nchi kuepushwa na janga hilo, ambalo linaendelea kusumbua nchi nyingi duniani.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo, akiwemo Razalo Nkwavu na Jacob Ntemang'ombe walisema kuwa tahadhari juu ya corona inapaswa iendelee kuchukuliwa. Lakini pia alitaka maombi yaimarishwe, kwani ndiyo yaliyoinusuru nchi na kuifanya iwe hapa ilipo.

Muumini wa Kanisa la TAG, Janet Bubegwa alisema kuwa Rais Magufuli alipewa maono na Mungu na ndiyo maana aliona Watanzania wasimame na Mungu kwenye maombi, hali iliyofanya nchi kujikinga na ugonjwa wa corona, ambao sasa unasumbua nchi nyingi duniani.

Chanzo: habarileo.co.tz