Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maaskofu katoli washauri kinga ya viongozi kutoshtakiwa ifutwe

Viongozi Tec Maaskofu katoli washauri kinga ya viongozi kutoshtakiwa ifutwe

Thu, 23 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetaka watu wote kuwa sawa mbele ya sheria na kutaka mfumo wa hakijinai usiweke kinga ya kutoshtakiwa kwa baadhi ya viongozi umma.

Aidha, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limetaka sheria ya ndoa inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 ibakie kama ilivyo.

Viongozi hao wa dini walitoa maoni hayo Dar es Salaam jana mbele ya Tume ya Kurekebisha Mfumo wa Haki Jinai, inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Chande.

Mkurugenzi wa Hadhi ya Utu wa Mwanadamu kutoka TEC, Dk. Camilius Kassala, alisema Katiba inatamka kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria na wakati huo huo inaweka kinga ya kutoshtakiwa kwa baadhi ya viongozi.

Baadhi ya viongozi wenye kinga ya kutoshtakiwa ni Rais, Spika wa Bunge, mwendesha mashtaka wa serikali na majaji.

Alisema kinga ya kutoshtakiwa kwa baadhi ya watu ni kinyume cha utu kwa kuwa watu wote wako sawa mbele za Mungu bila kujali hadhi yao kidunia.

“Kuweka kinga ya kutoshtakiwa ni makosa ndiyo maana kuna vuguvugu la Katiba Mpya ili hiyo kinga iondolewe. Watu wameanza kuelewa kwamba sisi binadamu wote tuko sawa kama alivyotufundisha Baba wa Taifa Mwalimu (Julius) Nyerere. Uwe Rais usiwe Rais sote tuko sawa.

“Mwanadamu ni sura na mfano wa Mungu ana hadi yake. Awe gerezani kama mfungwa, mtuhumiwa, tajiri, bosi, kamanda wa polisi au rais…hadhi ya kila binadamu ni sawa,” alisema.

Alipendekeza kuwa mfumo wa hakijinai utoe mamlaka kwa wananchi kuishtaki serikali pale wanapoona haijatimiza wajibu wake ipasavyo hususani inaposhindwa kusimamia haki za raia.

Dk. Kassala alifafanua kwamba watendaji katika vyombo vya hakijinai kuanzia polisi, mahakama, magereza na mawakili, wanapaswa kuzingatia utu pale mtuhumiwa anapokamatwa hadi anapohukumiwa.

Kuhusu mahakama, alipendekeza kuwa mfumo uboreshwe ili uzito wa adhabu uendane na hadhi ya mahakama pamoja na uhalisia wa mtuhumiwa.

Alitoa mfano kwamba Mahakama za Mwanzo zinashughulikia makosa madogo pamoja na wananchi wa kipato cha chini, hivyo iwekewe ukomo wa faini kwani mara nyingi zinakuwa kubwa jambo linalotoa mwanya wa rushwa.

Kwa upande wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), imependekeza utu na haki vizingatiwe kwenye ngazi zote za haki jinai kuanzia polisi, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP hadi) na mahakamani.

Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Askofu Nelson Kisare, ambaye amewasilisha maoni ya CCT, alisema watuhumiwa waliopo mahabusu na wafungwa, wanapaswa kuhudumiwa kwa kuzingatia utu na haki zao bila kunyanyaswa.

“Mapendekezo yetu ni kuona mahakama ikitoa haki kwa uhuru bila kuingiliwa na chombo chochote itoe haki kwa usawa,” alisema.

Mwanasheria Mkuu wa BAKWATA, Hassan Athman, alisema baraza hilo limependekeza maboresho kwenye maeneo mengi ikiwamo ya mwenendo wa makosa ya jinai, ugaidi, uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kutaka sheria ya ndoa ibakie kama ilivyo.

Alisema imani ya Kiislamu inaruhusu mtoto kuolewa anapovunja ungo, hivyo sheria ya ndoa kutoa ruhusa ya mtoto kuolewa kwa ruhusa ya mahakama ni jambo wanaloliunga mkono.

“Kuna ukinzani katika sheria ya ndoa, sheria ya mtoto na katika imani…sisi Waislam tunaamini kijana wa kiume anapobalehe anaruhusiwa kuoa na binti anaruhusiwa kuolewa anapovunja ungo. Haijalishi kavunja ungo akiwa ana miaka 10, 12, 13. Kiimani sisi tunaruhusiwa,” alisema.

“Tumependekeza kwamba kifungu kinachoruhusu umri wa miaka 14 kibaki mtu aruhusiwe kuolewa,” alisema.

Pia alipendekeza sharti la dhamana ya mtumishi wa serikali kwa mtuhumiwa liondolewe, kwa kuwa wapo raia wengi waadilifu wanaweza kuwadhamini ndugu zao pale watakapokabiliwa na kesi.

Alisema BAKWATA pia imependekeza kwamba mfumo urekebishwe ili DDP asifungue kesi ya jinai mahakamani kama hajakamilisha upelelezi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live