Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maaskofu KKKT waja na salamu nzito za Krismasi

89773 Maaskofu+pic Maaskofu KKKT waja na salamu nzito za Krismasi

Tue, 24 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wametoa salamu za Krismasi na mwaka mpya, huku mkuu wa kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo akijikita katika imani, elimu na siasa hususani uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka huu.

Pia katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) na viongozi wa baadhi ya mikoa nao wametoa ujumbe wao wa mwaka mpya.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga alienda mbali na kuielezea Noeli au Krismasi kuwa ni jibu kwa wenye nguvu na mamlaka wanaodhani dunia na vyote vilivyomo ni mali yao.

Salamu hizo zitasomwa rasmi keshokutwa Jumatano katika Dayosisi za makanisa hayo.

Katika salamu zake kwa waumini wa KKKT nchini, Askofu Shoo alisema mwaka 2019 uliobakiza siku tisa kumalizika haukuwa mteremko na raha bali ulikuwa na changamoto nyingi za kimaisha.

“Tumeshuhudia baraka nyingi za Mungu kwetu, lakini pia magumu na changamoto nyingi za kimaisha. Wapo waliouguliwa sana na hata kuondokewa na wapendwa wao,” alisema Askofu Shoo.

“Wengine wamepata wakati mgumu hata jinsi ya kulipa gharama za elimu za watoto wao pamoja na kuwapatia mahitaji mengine muhimu kutokana na changamoto za kiuchumi,” alisisitiza Dk Shoo.

“Mwaka huu pia tumeona uchaguzi wa serikali za mitaa ukifanyika. Kama kawaida ilivyo kwa nchi za Afrika, uchaguzi huu haukupita bila kuwapo kwa changamoto,” alisema.

“Tumeshuhudia sintofahamu kadhaa katika mchakato mzima jambo lililosababisha tukaingia katika uchaguzi bila kuwa na muafaka wa pamoja wa wadau mbalimbali muhimu vikiwamo vyama vya siasa,” aliongeza Askofu Shoo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 24, baadhi ya vyama vya upinzani vilisusia uchaguzi huo wakipinga walizoita hujuma walizofanyiwa wagombea wao wakati wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu.

Vyama vilivyojitoa ni Chadema, CUF, ACT-Wazalendo, UPDP, Chaumma na NCCR-Mageuzi na kuiacha CCM ikijipatia ushindi mnono wa zaidi ya asilimia 99.

Hata hivyo, Askofu Shoo alisema kuzaliwa kwa Yesu Kristo inakuwa ni habari njema na ya furaha kuu kwa waumini wote wa Kikristo; matajiri, masikini, yatima, wajane, wasomi na wasio wasomi.

“Mwokozi wetu Yesu Kristo anazaliwa kwa ajili ya watu wote. Anakuja kuleta nuru mahali penye giza, haki pasipo na haki, matumaini mapya tulipokata tamaa na furaha penye huzuni,” alisema Askofu Shoo.

Ujumbe wa matumaini

Askofu Munga alisema ujumbe uliomo katika salamu zake za Krismasi na mwaka mpya ni wa matumaini kwa sababu Mungu anadhihirika kama bwana wa historia.

“Mungu hakai nje ya historia ya ulimwengu. Haki ndiye anayeitengeneza na kuitawala. Noeli ni jibu kwa wenye nguvu na mamlaka wanaodhani dunia na vyote vilivyomo ni mali yao,” alisema.

Dk Munga alieleza Noeli ni kumbushio kwamba Mungu anaujia ulimwengu na kuukomboa toka mamlaka dhalimu ya shetani na maswahiba wake.

“Noeli ni alama ya kuonyesha mwisho wa ufalme wa giza na tishio lake la uvuli wa mauti kwa uumbaji. Noeli ni kuja kwa uhuru na kufunguliwa toka mamlaka zenye ishara na alama za umauti,” aliongeza.

Kuheshimu utu wa mwanadamu

Kama walivyo maaskofu wenzake, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk Benson Bagonza alisema mwanadamu hawezi kumpenda Mungu kisha akamdharau na kumtesa mwanadamu mwenzake.

“Kumpenda Mungu huku tukiwatesa na kuwadharau wanadamu ni ibada ya sanamu na Mungu hawezi kuwa upande wetu hata kama tunamuimba kila siku na kula viapo kwa jina lake,” alisema Askofu huyo.

“Tunaalikwa kuheshimu utu wa mwanadamu kama Mungu alivyouheshimu na kufanyika mwili. Kumtesa mwanadamu ni kumtesa Mungu aliyefanyika mwili,” alisisitiza Askofu Bagonza.

Askofu Bagonza aliongeza kuwa, “kumdhulumu, kumbeza, kumbagua, kumnyanyasa mwanadamu ni sawa na kumtendea Mungu mambo hayo kwa sababu Mungu yupo ndani ya mwanadamu.”

Askofu Bagonza alisema kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulileta mtazamo mpya katika hali ya dunia na thamani ya binadamu iliongezeka kwa kubeba sura ya Mungu na ukweli ulipata mmiliki halisi.

Viongozi mbalimbali wa dini nchini, hususan maaskofu wamekuwa wakitumia sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, kufikisha ujumbe kwa waumini wao kupitia ibada za siku hizo.

Dk Kitima

Akitoa maoni yake binafsi, katibu mkuu wa TEC, Dk Charles Kitima alitaja maeneo matatu yanayowahitaji Watanzania na Serikali kujitafakari upya kupitia sikukuu hizi.

Jambo la kwanza, Dk Kitima aliwataka Watanzania hususani Wakristo nchini kuhakikisha wanaipokea na kuitafsiri sikukuu ya Krismasi katika kuimarisha amani kwa mwaka ujao wa 2020.

Pili, Dk Kitima alisema mwaka ujao 2020 unatakiwa kuwa mwaka wa kufanya tathmini ya Taifa linakotoka na linakoelekea katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwamo ajira kwa vijana.

“Pia kuna changamoto ya wakulima kupata masoko ya nje, hii inafanya wakulima washindwe kujikwamua katika dimbwi la umaskini,” alisema Dk Kitima.

Wakuu wa mikoa

Naye mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila aliwaomba wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanaendelea kuimarisha amani katika mwaka wa 2020.

“Niwatakie kila la kheri katika sikukuu, lakini kikubwa ni kulinda amani katika mkoa wetu kwani ndiyo msingi wa kila kitu, nawaomba kuongeza ushirikiano kwa maslahi ya mkoa wetu,” aliongeza Chalamila.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliwapongeza wakazi wa mkoa huo wakiwamo viongozi wa dini na wanasiasa kwa kufanikisha utulivu wa matukio ya uhalifu mwaka 2019 sanjari na hamasa ya kushiriki shughuli za maendeleo.

“Niwatakie wakazi wa mkoa wangu sikukuu njema lakini tujikite kufanya kazi zaidi ili kujiletea maendeleo yetu binafsi na taifa, ni jambo la msingi mwakani,”alisema Profesa Lipumba.

Chanzo: mwananchi.co.tz