Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA KIISLAM: Uhusiano wa Mwislamu na Mola wake kiimani

34791 Pic+muislam Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanadamu ni kiumbe wa maisha ya kijamii na si kiumbe wa kijima au kuishi maisha ya upweke. Jinsi mwanadamu anavyohusiana na wanaomzunguka ni kipimo kimojawapo cha utu, uungwana na ustaarabu wake.

Lakini kwa Muislamu, uhusiano wa kwanza kabisa kuingia akilini mwake ni ule kati yake na muumba wake. Ni kwa sababu anatambua kwamba pasi na muumba wake, yeye si chochote kile mbele za watu.

Ni muhimu basi kujua ni vipi uhusiano kati ya Muislamu unapaswa uwe ili asije kujikuta amekata mawasiliano na muumba wake na kuunga mawasiliano na viumbe.

Awe muumini aliye macho

Jambo la kwanza ambalo Uislamu unamtaka muumini wa dini hii awe nalo ni kuwa macho au hadhiri. Maana yake awe muumini wa kweli kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad (Rehma na Amani Ziwe Juu Yake).

Anapaswa kumkumbuka Mola wake kila wakati kwa kumtaja (dhikri) na kutambua uwepo wake katika kila sekunde katika maisha yake. Atambue ukuu wa Uungu wake kwa kujiangalia mwenyewe na kuangalia viumbe vinavyomzunguka.

Anasema Mweyezi Mungu: “Na katika ardhi kuna dalili (za Uungu wake) kwa wenye yakini. Na katika nafsi zenu, basi je, hamuoni”? (Qur’an 51:20-21).

Kwa hisia hizi, muumini humtegemea Mwenyezi Mungu pekee katika maisha yake huku akijitahidi kutafuta sababu za mafanikio na kumuomba Mwenyezi Mungu amfanyie wepesi na ampe baraka zake katika kila jambo alifanyalo.

Kutambua kwake kuwa yeye ni kiumbe wa Mwenyezi Mungu asiye na uwezo wowote wa kujiletea mafanikio, muumini huhisi ndani kabisa ya moyo wake nguvu kuu za Mwenyezi Mungu na jinsi anavyohitajia nguvu hizo.

Ni hapo ndipo unapomkuta muumini akiwa haogopi nguvu zozote zile za viumbe, huku akiyakumbuka maneno ya Mtume wake aliposema kumwambia Abdallah ibn Abbasi (Mwenyezi Mungu amridhie);

“Ewe kijana, hakika mimi nakufundisha maneno. Mhifadhi Mwenyezi Mungu atakuhifadhi. Mhifadhi Mwenyezi Mungu utamkuta mbele yako.

Na tambua kwamba kama watu wote watakusanyika ili wakunufaishe kwa kitu hawawezi kukunufaisha isipokuwa kwa kitu ambacho Mwenyezi Mungu alikwisha kuandikia. Na kama watakusanyika ili wakudhuru, basi hawawezi kukudhuru isipokuwa kwa kitu ambacho Mwenyezi Mungu alikwisha kukuandikia. Kalamu (zinazoandika mambo yatakayowatokea viumbe) zilikwishainuliwa na kurasa zilikwisha kauka wino” (Imepokewa na Tirmidhy).

Uhusiano imara kati ya mja na Mola wake humfanya awe na yakini kwamba hata afanye juhudi kiasi gani na atumie mbinu gani, mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu kufanikiwa au kutofanikiwa kwake ni Muumba wake.

Imani hii ndiyo ijulikanayo katika Uislamu kama ‘Qadar’ na ni nguzo ya sita katika Nguzo Sita za Imani ya Kiislamu ambazo muumini anapaswa kuziamini.

Nguzo hizo ni kuamini kwamba hakuna Mola apasaye kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na ardhi, kuamini Malaika wake, Vitabu au Ufunuo wake, Mitume wake, kuamini Siku ya Malipo (Kiama) na Qadar.

Muumini wa kweli Muislamu si mwenye kughafilika na kumkumbuka Mwenyezi Mungu nyakati zote za maisha yake na hisia kuhusu Mola wake ziko moyoni mwake katika hali yoyote ile aliyoko.

Mwenyezi Mungu anauelezea uhusiano huu kati ya muumini na Mola wake pale aliposema: “Hakika katika kuumbika mbingu na ardhi na mabadiliko ya usiku na mchana yenye kufuatana, kuna mazingatio kwa watu wenye nyoyo zinazofanya kazi.

“Ni wale wanaomtaja Mola wao wakiwa wamesimama wima, wakiwa wamekaa kitako au wamelala kwa mbavu zao na wanatafakari juu ya kuumbika kwa mbingu na ardhi (kisha husema) ewe Mola wetu hukuumba yote haya burebure tu (pasina lengo) “Qur’an 2:190-191).

Awe muumini mtiifu kwa Mola wake

Kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu Muumba mwenye nguvu mwenye kutawala maisha ya viumbe wote, hakutoshi iwapo mja hatomtii kwa kufuata maamrisho yake na kuacha makatazo yake.

Kwa hiyo katika kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya mja na Muumba wake uko salama, mja daima hutaka kujua Mola wangu ameniamrisha nini na amenikataza nini.

Muumini anapaswa kusalimu amri kwa Mola wake na ndiyo maana ya neno “Uislamu” yaani kujisalimisha kwa amri za Mwenyezi Mungu.

Huu ndio Uislamu na hakuna Uislamu wa kuishi kwa imani pekee bila ya matendo kama wafanyavyo wengi wanaojiita Waislamu.

Uislamu ni kutamka kwa ulimi kwamba hakuna Mola wa kuabudiwa isipokuwa Mola Muumba, kuamini imani hiyo kwa dhati kabisa moyoni na kuitafsiri kwa vitendo.

Wale wasiotafsiri imani hii kwa vitendo na kufuata amri za Mwenyezi Mungu na kuacha makatazo yake, wanaishi nje ya maana ya Uislamu hata kama wanajiita Waislamu. Katika Uislamu, imani huzidi kwa kumtii Muumba na hupungua kwa kumuasi Muumba.

Katika kuboresha uhusiano wake na Muumba wake, muumini hutambua kuwa ana wajibu kwake ikiwa ni pamoja na kuihubiri haki iliyomfikia na kuwatendea wema viumbe wote wa Mwenyezi Mungu.

Mtume Muhammad (Rehma na Amani Ziwe Juu Yake) anasema: “Kila mmoja wenu ni mchungaji na ataulizwa juu ya uchungaji wake” (Bukhari na Muslim).

Nasaha zangu kwa kila Muislamu ni kujitahidi kuishi maisha yenye uhusiano mzuri kati yetu na Mola wetu na uhusiano mzuri na viumbe wenzetu pamoja na tofauti zetu.



Chanzo: mwananchi.co.tz