Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Wanaofunga kwa ibada, maigizo watajibainisha baada ya Ramadhan

59424 Pic+kufunga

Fri, 24 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao Waislamu walio wengi hufunga kwa kuacha vyakula na vinywaji vyao kuanzia alfajiri mpaka magharibi, ndio huu ambao tayari sasa tumeshaingia katika nusu ya pili.

Pamoja na Waislamu wengi kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani tena kwa hiyari yao, ni vyema tukakumbushana mapema kwamba watakaofaidika ni wale tu watakaofunga kwa malengo ya ibada na si maigizo.

Kwa kuwa ibada ya swaumu ni miongoni mwa ibada zenye usiri mkubwa hata kutambua malengo ya mfungaji kama ni funga ya kweli au maigizo ni vigumu sisi kutambua kwa kuwa sote tunaungana kwa kutokula wala kunywa chochote mchana wote.

Hivyo basi njia pekee yenye uhakika ni kusubiri baada ya Ramadhani na kisha kuyatazama maisha baada ya funga kwa wale waliokuwa wakifunga ndipo hapo tafsiri iliyo wazi itaonekana.

Kabla mwezi mtukufu wa Ramadhani haujamalizika ni vyema nikaziweka wazi sifa bainifu za anayefunga kwa ibada na anayefunga kwa maigizo ili huenda kwa haya masiku machache yaliyosalia kila mmoja akajirekebisha hasa yule anayefunga kwa maigizo.

Ni vyema tukakumbushana kwamba ibada kwa Muislamu inatafsirika katika kufuata maamrisho (kutenda mema) na kuacha makatazo (maovu na machafu). Yeyote anayeabudu kwa mtazamo mmoja tu huyo kamwe hawezi kufaidika na ibada.

Pia Soma

Ibada kwa upande wa kwanza ni kuyafuata yale maamrisho ya Mola wetu Muumba yatendwe, basi kule kuyatenda hiyo ndio ibada, na yale aliyoyakataza yasitendwe, basi kuyaacha ni ibada pia kwa upande wa pili.

Yeyote anayeabudu kwa kufuata maamrisho tu (kutenda mema) lakini haachi makatazo, huyo hawezi kufaidika na mema yake kwani mabaya na maovu yake ‘atayatafuna’ na kuyameza mema yake. Na yeyote anayeabudu kwa kutotenda yaliyokatazwa lakini hafanyi mema kabisa yaliyoamrishwa, huyo hatafaidika na kuacha kwake mabaya kwani ‘atadaiwa’ mema ambayo aliamrishwa kuyatenda.

Kwa ufafanuzi huu, kuacha mabaya na kutenda mema ni ibada mbili zinazohitajiana na zinazotakiwa kwenda pamoja.

Kwa muktadha huo, wanaofunga swaumu ya Ramadhani huwa pia wanajikinga na kutenda yaliyokatazwa na sheria kama vile ulevi, wizi na zinaa.

Kwa mtazamo wa wazi, swaumu inaonekana ni swaumu ya kweli na ‘imekolea’ kwa kiasi cha kumkanya mfungaji asifanye maovu na machafu. Hiyo ndio hali ambayo takriban Waislamu wote wanajionyesha na wanaonekana kuwa nayo ndani ya Ramadhani.

Hata hivyo, Ramadhani ikiisha bado jamii itaendelea kuwatazama Waislamu hawa kwa jicho la kwamba ni wachamungu na yale yote waliyokatazwa na wakakatazika kwayo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, wataendelea kukatazika katika miezi mingine kwani Mola aliyewakataza maovu na machafu waliyoyaacha ndani ya Ramadhani bado yupo tena habadiliki na kamwe hatobadilika.

Kwa Waislamu watakaojionyesha na wakaonekana kwamba wameyarudia maovu na machafu yao waliyoyaacha ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, hao ndio wale waliofunga kwa maigizo kwani swaumu ya kweli itamfikisha mfungaji katika uchamungu endelevu.

Swaumu ambayo inamfikisha mfungaji katika uchamungu unaokomea katika mwezi wa Ramadhani tu, hayo ni maigizo na mfungaji wake hakuwa akifunga kama ibada bali alikuwa amejifananisha na wafungaji wa kweli ilhali alikuwa anaigiza tu na wala hakuwa na dhamira ya dhati ya swaumu yenyewe.

Sasa wafungaji wenzangu kila mmoja ajitafakari kwamba yale maovu na machafu aliyoyaacha akiwa katika swaumu ataendelea kuyaacha hata baada ya Ramadhani kumalizika? Kama atayarejea atakuwa anajibainisha na kujitambulisha mwenyewe kwamba hakuwa anafunga kama mchamungu kwani uchamungu ni sifa endelevu.

Hivi wafungaji wenzangu tutachagua nini baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani? Je, tutajibainisha kuwa tulifunga kiuchamungu au tulikuwa tunafanya maigizo na pale mwezi wa maigizo ulipokwisha, sasa tunarudia uhalisia wetu?

Haya shime kila mmoja wetu ajitafakari na afanye tathmini hiyo hivi sasa ili mwezi mtukufu wa Ramadhani ukiisha achague mwenyewe iwapo atajibainisha katika jamii kama mfungaji au muigizaji.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation.

0754 299 749/ 0784 299 749.

Chanzo: mwananchi.co.tz