Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Waislamu tunawajibika kutoa zaka ya mali na zaka ya fitri

60651 Pic+waislam

Fri, 31 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Muundo wa dini ya Kiislamu ni kuvunja ubinafsi katika kumiliki mali na manufaa yake. Muislamu wa kweli ni yule ambaye kamwe hafurahii shida za mwanadamu mwenzake.

Kwa muktadha huo, yapo mafunzo kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad (SAW) ambaye amesema: “Si muumini wa kweli yule ambaye anashiba na ilhali jirani yake ubavuni kwake ana njaa”.

Hivyo basi, Uislamu umempa mtihani mwenye imani ajipime kwa yeye kumtakia mema jirani yake.

Akarudia tena Mtume Muhammad (SAW) kwa kusema: “Hawi muumini wa kweli mmoja wenu mpaka ampendelee ndugu yake apate lile ambalo nafsi yake inapenda apate”.

Hivyo yeyote mwenye mali hatakiwi kuwa mbinafsi bali anatakiwa apanue wigo wa manufaa ya mali yake uenee katika jamii. Ili kukidhi hilo, Uislamu umefundisha umuhimu na faida ya kutoa sadaka mara kwa mara.

Sadaka ni mali chache anayoitoa mtu kumsaidia mwenzake mwenye shida na haina kima maalumu, lakini kila mtoaji vile anavyotoa kingi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyomkirimu kwa mali nyingi sana tena yenye baraka na ulinzi timilifu.

Pia Soma

Dawa kubwa ya kulinda mali ni kutoa sadaka. Mtume Muhammad (SAW) anatupa habari akisema: “Hakuna siku yoyote ambayo waja wanaingia asubuhi ila kuna malaika wawili wanashuka, mmoja anaomba anasema: “Ewe Mola wetu tunakuomba umpe kila anayetoa sadaka umpe mbadala (umzidishie asipungukiwe) na kila anayezuia mali yake umpe kuharibikiwa”.

Kwa mafunzo hayo, sadaka ni jambo ambalo hatakiwi mtu yeyote kulipuuza.

Pia, Uislamu ukawajibisha kutoa zaka. Zaka ni kiasi kidogo cha mali anachokitoa yule anayemiliki mali ili kutekeleza agizo la Mwenyezi Mungu.

Zaka inahusisha maeneo mengi kwani kuna zaka ya biashara, zaka ya fedha, zaka ya mifugo, zaka ya madini, zaka ya mavuno, zaka ya Fitri na kadhalika. Kwa leo tuzungumzie kwa muhtasari zaka za biashara, fedha na fitri.

Kuhusu zaka ya biashara, mfanyabiashara anatakiwa azingatie tarehe yake aliyoanzia biashara. Biashara ya siku ikitimiza mwaka mmoja afanye hesabu ya bidhaa zake zote kwa bei ya ununuzi (sio bei anayotarajia kuuza), akipata jumla kuu ya mali yake yote ndipo atatoa kiwango cha zaka katika mali hiyo.

Kwa mfano, ameanza biashara kwa mtaji wa Sh10 milioni na leo ametimiza mwaka mmoja, amefanya hesabu bidhaa zake zote zina thamani ya Sh40 milioni, hiyo ndio jumla kuu.

Hiyo jumla aigawe kwa 10 kisha moja ya 10 aigawe kwa nne na hiyo moja ya nne ndio aitoe zaka. Kwa hiyo zaka ya mali yenye thamani ya Sh40 milioni ni Sh1 milioni.

Kwa mintaarafu hiyo, zaka ya bidhaa zenye thamani ya Sh100 milioni ni Sh2.5 milioni.

Zaka ya biashara na zaka ya fedha zinafanana katika mahesabu lakini ieleweke kwamba fedha inayotolewa zaka ni ile iliyotulia kwa kukaa mwaka mzima. Kwa mfano, zaka ya fedha kiasi cha Sh200 milioni zilizokaa benki mwaka mmoja ni Sh5 milioni.

Kuhusu zaka ya Fitri, hii hutolewa tarehe za mwisho za mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kiwango chake ni kutoa kilo mbili na nusu za mchele ulio safi au fedha zinazolingana na bei halisi ya kilo mbili na nusu kwa kila mmoja. Na kama mtoaji ataongeza atapata malipo na fadhila zaidi.

Mtoaji zaka ya fitri ni kila Muislamu aliyefunga na hata ambaye hakufunga lazima ajitolee zaka ya fitri yeye mwenyewe kisha awatolee wote ambao anawajibika kuwalisha mpaka mtoto mchanga pia atatolewa zaka ya Fitri kwa kiwango hicho hicho anachotolewa mtu mzima.

Hivyo kwa mtu mwenye familia ya watu kumi wakubwa na wadogo atawajibika kutoa kilo 25 za mchele ulio safi kwa maana kila mtu mmoja atamtolea kilo mbili na nusu.

Wanaopewa zaka yoyote ile iwe ya mali au fitri ni maskini, mafakiri, wasafiri wenye dhiki, watu wanaodaiwa, watu wanaojishughulisha na dini, mtu aliyeingia katika Uislamu na wote wanaojishughulisha na kuzikusanya hizo zaka.

Pia, wanaopaswa kutoa zaka ya Fitri ni wote ambao wana uhakika wa kutimiza chakula chao usiku wa kuamkia Iddi na mchana wote wa Iddi. Hivyo basi yeyote ambaye tayari anacho chakula chake cha siku ya Iddi na usiku uliopita wa kuamkia Iddi, lazima atoe zaka ya Fitri hata kama yeye mwenyewe pengine naye amepewa.

Kwa muktadha huo, ieleweke kwamba kutoa zaka ya fitri sio hiari.

Miongoni mwa malengo ya zaka ya Fitri ni kusafisha makosa madogomadogo tuliyoyafanya tukiwa tumefunga, kuzinyanyua swaumu zetu kwani swaumu ya mwenye uwezo wa kutoa zaka ya Fitri haipandi mpaka atoe zaka hiyo, kumtosheleza maskini ili naye siku ya Iddi apumzike na kazi ya kuombaomba.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. +255 754 299 749, +255 784 299 749.

Chanzo: mwananchi.co.tz