Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Uislamu unavyoamrisha utii kwa viongozi

44307 Pic+mahubiri MAWAIDHA YA IJUMAA: Uislamu unavyoamrisha utii kwa viongozi

Fri, 1 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika jamii yoyote ya wanadamu duniani, watu wake wanahitajiana. Kwa maneno mengine binadamu hawezi kujitosheleza na kujitegemea kwa kila kitu. Mwenyezi Mungu (Subhaanahuu Wataalaa) amewaumba wanaadamu katika maumbile ya kuhitajiana.

Kwa kuwa wanaadamu wanahitajiana ni lazima shida zao zitawakusanya pamoja na wanapokutana lazima pawepo uongozi. Bila ya kuwapo uongozi, mwenye nguvu anaweza kumdhulumu mnyonge.

Bila ya kuwapo uongozi, aliyedhulumiwa atakosa pa kudai ili arejeshewe haki yake au mwisho atajichukulia sheria mkononi, jambo ambalo ni baya na hatari. Kwa muktadha huo, uongozi unahitajika popote pale.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema katika kuonyesha kwamba hakuna mazingira ya hata jamii ndogo kuishi bila ya uongozi: “Wakitoka watu watatu kwenye safari yoyote (wanatakiwa) wamfanye mmoja kiongozi,’’ akaongeza tena kusema:

“Haiwi halali kwa watu wowote waliopo mbugani katika ardhi isipokuwa (wanatakiwa) wamfanye kiongozi mmoja wao.’’

Utii kwa uongozi

Hadithi zote hizo mbili zinafundisha na zinaelekeza wajibu na ulazima wa kuwapo uongozi. Na uongozi unapokuwapo hapo ndipo pia panapozaliwa wajibu wa kuutii huo uongozi. Uongozi hautokuwa na maana yoyote kama utii haupo kwa uongozi huo. Hivyo, Uislamu unaamrisha, unafundisha na unalazimisha kuwatii viongozi.

Mwenyezi Mungu anasema katika Quran Tukufu Sura ya 4 (An-nisaai) Aya ya 59: “Enyi Waumini mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka miongoni mwenu.’’

Kwa mafunzo yatokanayo katika aya hii, kuwatii viongozi siyo jambo la hiari. Msingi mkubwa wa Uislamu kufundisha utii kwa viongozi ni ili jamii isiende ovyo na iwe na wasimamizi.

Baada ya kuamrisha wajibu wa utii kwa viongozi, Uislamu ukaweka maangalizo matatu:

Mosi, kuwaonya na kuwataka viongozi wawe waadilifu wasionee watu wanaowaongoza wala wasiwadhulumu;

Pili, kutiiwa kwa viongozi kuwe na mipaka na siyo utii wa asilimia 100 kwa vyovyote au lolote wanaloliamrisha;

Tatu, kwa namna yoyote na vyovyote wawavyo viongozi hairuhusiwi kujitoa katika himaya ya uongozi.

Mwenyezi Mungu (Subhaanahuu Wataalaa) amesema katika Quran Tukufu Sura ya 4 (An-nisaai) Aya ya 58: “Na pindi mkihukumu kati ya watu hukumuni kwa uadilifu.”

Pia, Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Waswallam) amesema akiwatahadharisha viongozi: “Hakuna kiongozi yeyote anayewaongoza japo watu 10 isipokuwa ataletwa Siku ya Qiyama ilhali amefungwa pingu mpaka utamfungua yeye uadilifu (aliowafanyia raia wake) au itamuangamiza yeye dhulma (aliyowafanyia raia wake)”

Akaongeza tena Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) kwa kusema: “Mtu mwenye adhabu kali mno siku ya Qiyama ni kiongozi dhalimu.”

Hivyo, viongozi kabla ya kufurahia utii ambao Uislamu unawalazimisha raia kwao, waifahamu kwanza dhima ya uongozi.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) ametahadharisha kwa kusema: “Ewe Mola, yeyote mwenye kutawala katika mambo ya umma chochote kisha yeye akawatilia uzito na yeye mtilie uzito. Na yeyote mwenye kutawala katika mambo ya umma wangu chochote kisha yeye akawafanyia upole nawe mfanyie upole.”

Ni vyema basi kila aliye katika uongozi au anayetamani kuwa kiongozi afahamu kwamba anayo dhima mbele ya Mola Muumba.

Kuhusu kutiiwa kwa viongozi kuna mipaka nayo ni utii kwa dhati kama hilo lililoamrishwa halina ndani yake kumuasi Mwenyezi Mungu (Subhaanahuu Wataalaa).

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Hakuna kumtii kiumbe yeyote katika (jambo la) kumuasi Muumba.”

Hivyo, wanaotawaliwa wafahamu kwamba wanaamriwa kuwatii viongozi wao kama amri yenyewe haipingani na haiendi kinyume na amri au makatazo ya Mwenyezi Mungu.

Tunatakiwa kuwa makini sana katika maudhui hii ya utii kwa viongozi kwamba Uislamu unaamrisha kutii uongozi wowote madhali uongozi huo hauamrishi maasi.

Ieleweke kwamba ni wajibu kuwatii viongozi bila ya kuangalia dini za viongozi hao na bila ya kuangalia wameupata vipi uongozi huo. Hii ni kwa sababu uhalali wa uongozi wowote popote pale duniani hautegemei ridhaa za wanaoongozwa au kuutambua kwao kwamba umepatikana kihalali.

Uislamu hauruhusu kabisa kuukataa uongozi eti kwa sababu haukukidhi vigezo unavyoviamini kwani vigezo huwa vinatofautiana.

Dunia ya leo ‘imechafuka’ na imejaa vita na migogoro katika maeneo mengi kutokana na ‘dhambi’ hii ya kuukataa uongozi na kuhalalisha ‘uasi’ ili kuuondoa uongozi uliopo na hapo damu za wasio na hatia ikiwamo wanawake, watoo, wazee, wagonjwa, walemavu na kadhalika zikamwagwa kwa maelfu.

Wapiganaji wa aina hiyo wameingia katika dhambi ya makosa makuu matatu ambayo ni kutotii uongozi; kuanzisha mamlaka ndani ya mamlaka; na kupiganisha na kuua watu bila ruhusa ya kisheria katika dini.

Mwandishi wa makala haya ni mwenyekiti wa Al risaalah Islamic Foundation.

0 754 299 749/0 784 299 749



Chanzo: mwananchi.co.tz