Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Uislamu ni dini kamili ya kijamii

39498 Pic+uislam MAWAIDHA YA IJUMAA: Uislamu ni dini kamili ya kijamii

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uislamu ni dini inayojengwa kwa nguzo tano ambazo ni:

(1) Kutamka kwa ulimi na kuamini kwa moyo kwamba: Hapana Mola mwenye kuabudiwa kwa haki ila Mungu mmoja na kwamba Muhammad (amani zimfike) ni Mtume wake.

(2) Kusimamisha Swala tano.

(3) Kutoa Zaka.

(4) Kufunga Mwezi mtukufu wa Ramadhani. (5) Kuhijji Makkah.

Pamoja na kwamba nguzo hizo ndizo zinazoujenga Uislamu kuwa msingi, lakini zipo nguzo nyingine ambazo zinaziimarisha nguzo hizo (ambazo ni nguzo za Ihsaani na nguzo za Imani).

Yenyewe Ihsaan nguzo yake ni moja tu ambayo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu kama vile unamuona na kama humuoni yeye anakuona.

Kuhusu Imani, nguzo zake ni sita ambazo ni:(1) Kumuamini Mwenyezi Mungu (kuamini uwepo wa Mungu). (2) Kuamini Malaika wake. (3) Kuamini Vitabu vyake. (4) Kuamini Mitume wake (5) Kuamini Siku ya Mwisho. (6) Kuamini Qadar (mpango wa Mwenyezi Mungu) kheri zake na shari zake.

Kwa kuwa Uislamu ni dini na yule anayeutekeleza ndiye Muislamu, ifahamike kwamba Muislamu kwa upande wa pili ni mwanaadamu anayehitaji kula, kunywa, kuvaa, kusafiri, kulala, kupumzika, kuoa au kuolewa, kuzaa na kadhalika. Hivyo atawajibika kujihusisha na jamii yake kwa kufanya kazi, biashara, kilimo, kusafiri na kadhalika.

Uislamu ni dini ya kijamii

Tukiyatazama namna Uislamu unavyojali mambo hayo na kuyawekea muongozo, tunayo haki ya kuweka wazi kwamba Uislamu ni dini ya kijamii.

Dhana zilizoko mitaani zinauona Uislamu kama dini ya kiroho tu na mambo yote ya kijamii katika jamii zetu kama vile kuuziana, kukodishana, kuazimana, kuwekeana rehani, kukopeshana, kuwekeana mikataba ya ushirika katika kazi au huduma; hayo hayana majibu katika Uislamu.

Ukweli ni kwamba Uislamu unatambua ibada na pia unatambua miamala na umebainisha usahihi wa kila kimoja ili jamii iweze kuishi salama kwa upendo.

Endapo jamii ingeamua kufuata miamala kama ilivyoelekezwa na Uislamu, basi jamii ingepunguza mifarakano inayochangiwa na matatizo ya miamala kwa zaidi ya asilimia 90. Lakini hata katika ibada za kawaida kama vile Swala, Swaumu, Hijja na Zaka, Uislamu umeweka usahihi wa ibada hizo katika kukubaliwa kwake uzingatie kwanza maisha ya Muislamu katika jamii yake na hata utekelezwaji wenyewe pia uiangalie jamii. Na hapo ndipo hubainika wazi kwamba Uislamu ni dini ya kijamii.

Ibada yoyote ndani ya Uislamu ambayo Muislamu ameitekeleza itakiwavyo na akaandikiwa ‘ujira’ wake, ieleweke wazi kwamba anaweza kunyang’anywa ujira huo kama ameishi ‘vibaya’ na jamii yake.

Mtume Muhammad (amani zimfikie) amesema: “Je, mnamjua mtu mufilisi? Maswahaba wakajibu Mufilisi ni yule asiye na pesa. Mtume akasahihisha kwa kusema: Mufilisi katika umma wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyama na ujira wa Swala, Zaka, Swaumu na Hijja lakini (kule duniani hakuishi vyema na jamii) alimtukana huyu, alimdhulumu huyu, alimwaga damu ya huyu. Atanyang’anywa malipo ya ibada zake ili wapewe wale ambao aliwadhulumu au aliwatukana.’’

Hapo tunajifunza kwamba pamoja na ibada anazozifanya Muislamu, kama ataishi vibaya na jamii yake, ibada zake hazitomfikisha katika malengo ambayo ni kupata radhi za Mola wetu Muumba.

Jamii imepewa kipaumbele na Uislamu

Tukiiangalia ibada ya Swala, yule Imamu anayeongoza ibada anaelekezwa na Uislamu kwamba asirefushe sana Swala kwa sababu ile jamii inayoswali nyuma yake baadhi yao ni wagonjwa, wasafiri na wengine wana shida zao mbalimbali.

Uislamu unamtazama yule Imamu anayeswalisha Swala kwa kuirefusha kwamba analeta fitina, kwa kuwa atawafanya wale anaowaongoza waharibikiwe na mambo yao na hapo wataichukia ibada ya Swala ya jamaa, na huyu Imamu kamwe hatoruhusiwa kurefusha Swala mpaka ile jamii iridhike.

Pia tukiangalia ibada ya Zaka ni ibada ya kijamii zaidi yenye jukumu la kuona wale wasionacho wanafaidika japo kwa uchache kutoka kwa walionacho ili kupunguza chuki kati ya walionacho na wasionacho.

Ibada ya Swaumu pamoja na kwamba ni ya kiroho lakini kwa jicho la pili ni ibada ya kijamii, kwani aliyefunga atapata uhalisia wa ukali wa njaa hivyo mwezi mtukufu ukiisha ataongeza kasi ya kusaidia maskini ili awapunguzie ‘njaa endelevu’ aliyoishuhudia katika mfungo.

Lakini ibada hiyo ya Swamu haitopokelewa na haitokuwa na ujira kama aliyefunga ataishi vibaya na jamii yake kwa kutukana, kuapa kwa uongo, kusengenya, kufitini na kadhalika.

Vilevile ibada ya Hijja ni ibada ya kijamii kwani anayehijji ni lazima ajichunge sana kuwakera Mahujjaji wenzake kwa namna yoyote ile.

Kwa muktadha huo, jamii imepewa nafasi kubwa na Uislamu hivyo Muislamu wa kweli kipimo cha Uislamu wake kitazamwe ni namna gani anaishi na jamii yake.

Muislamu anapofanya matendo mabaya kama vile wizi, kutukana, kupiga, kuudhi kwa namna yoyote ile na kadhalika, huyo haujui bado Uislamu. Muislamu wa kweli ni lazima jamii ifaidike kwake na isipate madhara yoyote kupitia yeye na ninaposema jamii namaanisha Waislamu, Wasiokuwa Waislamu na hata wanyama.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. 0754 299 749



Chanzo: mwananchi.co.tz