Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Tumeumbwa kumuabudu Mwenyezi Mungu

32688 Pic+Mungu Tanzania Web Photo

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki iliyopita tuliona jinsi ambavyo wanasayansi wa elimu za Fizikia, Biolojia na Kemia walivyolielezea lengo la mwanadamu na tukahitimisha kwamba hakika walichokieleza, siyo lengo la kuumbwa mwanadamu.

Lengo la kuumbwa mwanadamu kwa mujibu wa Qur’an na Sunnah au mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W), ni kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu na kumtumikia.

Qur’an Sura ya 51 aya ya 56 inalieleza lengo hili wazi kabisa pale Allah aliposema: “Na hatukuwaumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu”.

Ibada ni nini katika Uislamu?

Neno ibada kwa mujibu wa Uislamu ni neno la Kiarabu linalotokana na neno ‘Abd’ lenye maana ya mtumwa. Kwa hiyo ibada maana yake ni kumtumikia Mwenyezi Mungu pasina ubishi kama afanyavyo mtumwa.

Kwa maana nyingine ni kukiri kwamba mwanadamu ni miliki ya Mwenyezi Mungu na ndiye anayepasa kumpangia mwanadamu mpango mzima wa maisha yake hapa duniani na kumfundisha jinsi ya kuutekeleza kwa namna aipendayo yeye.

Kwa hiyo ibada ni kitendo cha mwanadamu kujidhalilisha na kujinyenyekeza kwa hiari kwa Muumba wake kama alivyoamrisha kupitia mitume na manabii wake, kwa kutaraji malipo mema kutoka kwake.

Ndiyo maana mwanachuoni Sheikh Ibn Taymiya akaielezea ibada kwa maneno haya: “Ibada ni neno linalokusanya kila kitendo akipendacho Allah na kukiridhia miongoni mwa kauli, matendo yafanywayo wazi wazi na kwa siri”.

Kwa hiyo neno ibada katika Uislamu lina maana pana sana tofauti na jinsi neno hilo hilo linavyofahamika katika dini nyingine. Katika Uislamu ibada siyo kuswali, kufunga swaumu, kuhiji Makka, kutoa zaka, kusoma Qur’an, kuleta dhikr (maneno ya kumtaja au kumsifu Mwenyezi Mungu) na matendo yajulikanayo kama ibada na watu wengi.

Katika Uislamu, kila linalomridhisha Mwenyezi Mungu hata kama ni kufikiria juu ya maumbile yake mbinguni na ardhini, ili kuufahamu ukuu na Uungu wake, utukufu na sifa zake ni ibada.

Kufanya kazi ya halali ili kujipatia riziki ni ibada, kuishi na wanadamu wengine vizuri kwa masikilizano na upendo usiomuudhi Mwenyezi Mungu ni ibada.

Ikafikia mahali hata wanandoa kustarehe katika tendo la ndoa kwa mujibu wa Uislamu kufanya hivyo pia ni ibada tena watalipwa thawabu na Mweyezi Mungu, na kwa maana hiyo mmoja wao akimnyima mwenzake unyumba pasina sababu ya msingi atapata dhambi.

Mtume Muhammad alisema: “Kujamiiana na mke wako ni sadaka. Mmoja wa Maswahaba akauliza, ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, tutalipwa thawabu hata kwa kukidhi matamanio yetu? Akamjibu, je, waonaje kama angefanya hivyo na mwanamke asiye halali kwake angepata dhambi?

Yule swahaba akajibu ndiyo? Mtume akasema “mnakihesabu kitendo hicho kinapokuwa katika maovu tu hamkihesabu katika kheri?

Ibada ndiyo lengo la kuumbwa mwanadamu na ndicho kina cha maana ya neno ibada kwa mujibu wa Uislamu. Kuhusu tendo la ndoa kwa nini liwe ibada inaweza isifahamike kirahisi.

Lakini ni kwa sababu mume na mke wamehalalishiwa kitendo hicho ili kiwe njia ya kupatikana watoto ambao ni muujiza mkubwa wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu na ni neema kubwa inayosababisha kuendelea kwa kizazi cha mwanadamu.

Kitendo hicho pia ni ibada kwa sababu kinachangia kupatikana utulivu wa nafsi kati ya mume na mke wasiwe wenye kutamani wanawake au wanaume wasiokuwa halali yao na hivyo kuwafanya wawe wacha Mungu wenye kuogopa zinaa.

Mwanadamu ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu

Katika kulielezea lengo la kuumbwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ametumia neno Khalifa zaidi ya mara moja katika Qur’an.

Anasema katika Surat Al-Baqara aya ya 30: “Na (Muhammad) kumbuka Mola wako alipowaambia Malaika Hakika mimi ninataka kumuweka Khalifa katika ardhi”.

Neno Khalifa kwa Kiingereza ni Vicegerent ambalo limeelezewa kama “mtu anayetumia mamlaka aliyopewa na mtawala kwa niaba ya mtawala huyo”.

Kwa maana nyingine, kwa mujibu wa Uislamu lengo la kuumbwa mwanadamu siyo kama wasemavyo wanafalsafa ni kustarehe kisha kusubiri kufa.

Lengo kuu la kuumbwa mwanadamu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu na hadhi ya mwanadamu ulimwengu ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu, yaani anayeutawala ulimwengu kwa niaba ya Mwenyezi Mungu. Ili mwanadamu aweze kufikia lengo la kumwabudu Mwenyezi Mungu ni lazima aishi maisha ya ahadi aliyopewa kwamba yeye ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu duiani, cheo ambacho hata Malaika walikitamani.

Malaika walisema: “Wakasema utamuweka humo atakayefanya uharibifu na kumwaga damu na umetuacha sisi hali ya kuwa tunazisifu sifa zako na kukutakasa? Akasema mimi ninajua yale msiyoyajua” (Qur’an 2:30).

Tukifanya majumuisho tunachoweza kusema ni kwamba mwanadamu ameumbwa na Mwenyezi Mungu na kuumbwa kwa mwanadamu ni kwa lengo maalum ambalo ni kumuabudu yeye pekee pasina kumshirikisha.



Chanzo: mwananchi.co.tz