Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Tujiulize, kwa nini ibada hazitubadilishi tabia zetu?

50625 Pic+ibada

Fri, 5 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ibada ni msamiati unaojumuisha utii kwa Mola wetu Muumba. Maana ya utii huu ni kufuata maamrisho ya Mola wetu Muumba na kuacha makatazo yake.

Ibada kwa tafsiri ya kutenda maamrisho na kuacha makatazo ya Mola wetu Muumba huwa zinambadilisha yule anayeabudu. Mtu anayefanya ibada huwa anabadilika kutokea kwenye tabia mbaya na kuwa na tabia nzuri zinazopendwa na kupendeza katika jamii.

Mwenyezi Mungu anasema katika Sura ya 29 (Al – Ankabuut) Aya ya 45: “Na simamisha Swala, hakika Swala inakataza machafu na madhambi.”

Aya hiyo inaonyesha kwamba anayeswali atakatazika na machafu na maovu mengine kutokana na ile nguvu ya swala.

Katika ibada ya saumu, Mwenyezi Mungu anasema katika Sura ya 2 (Al – Baqarah) Aya ya 183: “Enyi Waumini mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishwa (kufunga) waliokuwa kabla yenu ili mpate kuwa wacha-Mungu.”

Aya hiyo inaonyesha kwamba anayefunga atakuwa mcha-Mungu kwa mana ya kuwa na tabia ya kujikinga na madhambi.

Katika ibada ya Zaka, Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) anasema: “Zijengeeni ngome mali zenu kwa kutoa Zaka.”

Hadithi hiyo inabainisha kwamba anayetoa Zaka pamoja na faida aliyoipata kwa kusimamisha ibada, lakini pia ameijengea ulinzi mali yake haitopatwa na madhara, maangamivu wala hilaki yoyote.

Katika ibada ya Hijja, Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) anasema: “Yeyote mwenye kuhijji na asiseme maneno machafu na asifanye madhambi, atatoka katika madhambi yake (atasamehewa) kama siku anazaliwa na mama yake (alivyokuwa hana dhambi).”

Hadithi hiyo inaonyesha kwamba ili ibada ya Hijja ikubaliwe lazima anayehijji awe na tabia njema, na tabia njema ni jambo endelevu linalotakiwa kuwapo kwa muumini. Hivyo, ibada huleta matokeo chanya kwa anayeifanya.

Jambo la kutafakari na kujiuliza ni kwa nini tunaabudu lakini hatubadiliki? Kwa nini baadhi yetu tunaswali lakini hatujaweza kuacha dhambi ya uongo, zinaa na wizi? Kwa nini baadhi yetu kila mwaka tunafunga saumu ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani lakini baada ya kumalizika mfungo jamii inarudi kulekule katika kutenda maovu na machafu? Kwa nini muumini amefanikiwa kutekeleza ibada ya Hijja lakini hajabadilika kitabia?

Zipo sababu tano ambazo zinasababisha ibada yoyote isilete tija nazo ni: Moja, kufanya ibada bila ya kuwa na elimu ya ibada husika. Ieleweke kwamba ibada ni kazi inayohitaji elimu ya namna ya kuitekeleza.

Sasa ibada iliyokosewa kutokana na kukosa elimu kamwe haiwezi kuleta tija iliyotarajiwa. Ukweli ni kwamba mtu anapokosa elimu anaweza kufanya ibada kwa maana ya kushiriki ibada lakini katika uhalisia ibada husika hajaifanya.

Pili, kufanya ibada kwa kutumia mavazi, vyakula, vifaa vilivyopatikana kwa njia ya haramu. Unakuta mtu anaswali lakini amevaa nguo zilizopatikana kwa haramu, amekula chakula cha haramu na kadhalika.

Mtu wa aina hii hata akiswali kamwe hawezi kupata ile tija na baraka ya swala. Au unakuta mtu anafunga saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani lakini daku alilokula ni la haramu au hata futari anayofuturu ni ya haramu.

Kwa muktadha huo, tuelewe kwamba kuitumia haramu katika ibada kunaleta udhaifu katika ibada husika.

Tatu, kufanya ibada wakati fikra na moyo wote haupo pale kwenye ibada. Ibada yoyote ambayo yule anayeifanya anaifanya kimwili lakini fikra na moyo wake haupo katika ibada hiyo haiwezi kukubaliwa na Mwenyeezi Mungu, hivyo kamwe haiwezi kuleta tija inayokusudiwa.

Nne, kuzitekeleza ibada nje ya wakati au kuzitekeleza ibada baada ya kuchoka (kustaafu) na kwamba sasa hana kazi eti ndio anaona wakati wa kumuabudu Mwenyezi Mungu.

Swala inayoswaliwa nje ya wakati au swala zote za mchana zinakusanywa wakati wa Magharibi au Ishaa kisha zinaswaliwa kwa mpigo. Au swala zenyewe zinaswaliwa kama hakuna shughuli ikitokea kukiwa na shughuli ya maana swala inaachwa.

Ibada ya Hijja mtu anaamua kuitekeleza kwa kuwa sasa eti amestaafu na madhambi yote amepumzika. Utendaji ibada kwa mfumo huu hauwezi kuleta ile faida ya ibada.

Tano, kufanya ibada kwa kukidhi matakwa ya msimu au wakati sio kuabudu kwa lengo la kumuabudu na kumuogopa Mwenyezi Mungu. Unakuta mtu amefunga saumu lakini anatukana kama kawaida hana hofu hata chembe ya huyo Mola anayemyabudu.

Mtu amekwenda Umra au Hijja lakini huoni athari ya ibada katika uso wake na hana hofu hata moja ya huyo anayemuabudu.

Sababu hizi tukizichunguza na tukijichunguza tutagundua kwamba zimetuondolea ‘ukali’ wa ibada zetu. Tujirekebishe ili Mola wetu Muumba aturekebishie hali zetu na mambo yetu.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation.

0754 299 749/ 784 299 749



Chanzo: mwananchi.co.tz