Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Swaumu inavyowafundisha waumini kuwa wakarimu

56613 Pic+swaumu

Fri, 10 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni ibada yenye mafunzo na hekima nyingi.

Kwa leo hii ngoja tujikite katika funzo la ukarimu kupitia swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ili kila mfungaji ajipime yeye mwenyewe kama ameelimika na anatii somo la ukarimu kupitia ibada ya swaumu.

Ni vyema tukafahamu mapema kwamba swaumu inayokidhi vigezo ni ile ambayo miongoni mwa sifa zake inampamba mfungaji kuwa na tabia njema. Na miongoni mwa tabia njema zenye uzio mkubwa kwa Muislamu ni ukarimu.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu ameichagua dini hii yeye mwenyewe na wala haitotengemaa (haitokuwa nzuri) dini yenu isipokuwa kwa ukarimu na tabia nzuri”.

Kwa kuwa ukarimu ni sifa muhimu ambayo Muislamu hatakiwi kuikosa na ili aingie peponi ni lazima awe mkarimu, Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: ‘’Hakika ukarimu ni mti ulioko peponi, matawi yake yananing’inia ardhini, yeyote mwenye kushika tawi moja katika mti huo basi (tawi hilo) litamuingiza peponi”.

Pia, ni kwa sababu hiyo basi ndiyo umeletwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kumfundisha Muislamu ukarimu.

Ramadhani ni kweli inafundisha ukarimu kwa sababu:

Mosi, matajiri japo wenye kipato cha kati hawana mazingira yoyote ya kufahamu ukali na maumivu ya njaa, hivyo maskini anapokwenda kwa tajiri ili alalamikie ‘ukali’ wa njaa atakuwa analalamika mbele ya mtu asiyeelewa kadhia ya njaa.

Lakini baada ya kuletwa ibada ya swaumu ambayo tajiri anapofunga hupata ‘maumivu’ ya njaa kama yake aliyoyazoea maskini au pengine tajiri njaa yake ni kali zaidi, hapo tajiri baada ya kumaliza mfungo wa Ramadhani anakuwa ameelimika na amefahamu vyema uhalisia wa njaa na hapo akiombwa chakula ni rahisi kutoa.

Mwanaadamu kwa tabia yake huwa hahisi maumivu halisi katika tatizo ambalo halijamtokea.

Pili, Ramadhani inafundisha ukarimu baada ya kuwahimiza Waislamu wafuturishane japo kwa tende ‘tumba moja’ au maji ‘funda moja’ na ujira wake ni kusamehewa madhambi na kulipwa thawabu kwa idadi anayolipwa yule aliyefuturishwa pasi na kupungua katika ujira wa yule mfungaji.

Tatu, Ramadhani inafundisha ukarimu kwa kiwango cha kumhimiza mwajiri kumpunguzia kazi mfanyakazi wake na kumuahidi kuachwa huru ‘shingo’ yake na moto wa Jahannam.

Nne, Ramadhani inafundisha ukarimu siyo tu kwa ajili ya futari na daku pekee bali hata maandalizi ya sherehe ya sikukuu. Waislamu wanawajibishwa kutoa zaka maalumu ya kuwasaidia wanyonge ili nao wafurahie sikukuu ya Iddi kwa furaha timilifu ya kula na kunywa kama wengine.

Kwa muktadha huo, yeyote atakayefunga swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kisha bado akawa hana tabia ya ukarimu, huyo amepoteza faida kubwa ya swaumu yake.

Ni vyema wafungaji wote wakajipima na kuzipima swaumu zao kupitia ukarimu wao kwa familia zao, Waislamu wenzao na jamii kwa ujumla.

Je, wewe unapofuturu futari tofauti zaidi ya 15, umemfikiria jirani yako iwapo amepata hata futari moja? Kama hujafanya hivyo basi swaumu yako ina shaka kwani swaumu ya kweli inampamba mfungaji na tabia ya ukarimu.

Hivi sisi tunapochagua aina mbalimbali za vyakula wakati wa futari na daku, je, tumewafikiria wenzetu waliopatwa na mtihani wa kuwapo magerezani?

Ni swaumu gani hizi ambazo hazipambwi na huruma? Ni huruma hizi ambazo hazitufikishi katika ukarimu.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Haukusanyiki ubakhili na imani katika moyo wa mja yeyote milele”.

Hadithi hiyo inatufunza kwamba muumini hawezi kuwa bakhili na bakhili hawezi kuwa muumini. Aya iliyokuja kutuwajibishia swaumu imetutaja kwa jina la imani kwa kutuita “Enyi Waumini mmefaradhishiwa kufunga…”. Kumbe ili tuwe na sifa ya kuitwa Waumini lazima tuwe wakarimu na asiye mkarimu huyo si muumini hata akidai kuwa ni muumini.

Niwakumbushe wafungaji wenzangu kila mmoja kwa nafasi yake kwamba:

Moja, twendeni magerezani tukawatembelee wafungwa na mahabusu tuwasaidie tutakavyojaaliwa japo kwa kuwapa maneno mazuri na kuwaonyesha kuwa tumewakumbuka na tunawakumbuka na iwapo tukikosa uwezo wa papo kwa papo basi japo tuziangalie familia zao kwa hii Ramadhani.

Mbili, twendeni katika vituo vya yatima tupeleke futari na tufuturu nao pamoja, tuwafariji na tuwaondolee unyonge wa kukosa wazazi. Na tukishindwa yote basi tuwabwagie japo nusu ya futari ambazo ndizo tunazofuturu sisi majumbani mwetu.

Tatu, twendeni hospitalini na katika hosteli za shule na madrasa kwani kuna vijana wanafunga na wako mbali na wazazi wao.

Haya shime ukarimu! Ibada ya swaumu inafundisha ukarimu na kama huna ukarimu tafakari upya swaumu yako.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. 0754 299 749



Chanzo: mwananchi.co.tz