Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Sababu 10 za kuvunjika kwa ndoa za Kiislamu

53106 Pic+mawaidha

Fri, 19 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ndoa kwa mtazamo wa dini ya Kiislamu ni mkataba ambao ukikamilishwa inavyotakiwa, unaleta mambo makubwa matatu:

Mosi, uhalali wa mume au mke kwa mwenza wake, pili, kuthibiti kisheria nasaba ya mtoto na tatu, kurithiana kati ya mume na mke pindi mmoja akifa.

Matarajio kwa wanandoa ni kuishi kwa upendo na kuhurumiana na kila mmoja akijiaminisha kwamba hakuna kitakachowatenganisha ila kifo.

Pamoja na matarajio hayo mazuri, ndoa nyingi leo hii zimekumbwa na hali tatu ikiwamo zile zinazovunjika kwa haraka hata chini ya mwaka.

Zipo zinazodumu lakini si kwa kupendana bali ni kwa sababu wameoana ndugu au wamebarikiwa kupata watoto, sasa wanaamua kuishi huku hawapendani ila kudumisha udugu tu, kuwahurumia watoto au kutokana na heshima zao katika jamii au umri wao umekwenda hivyo wanashindwa kuachana. Katika hali hii wapo waliofikia hatua ya kutolala chumba kimoja.

Pia, zipo ndoa zinazodumu kwa sababu mwanamume anafahamu kwamba kitakachotokea baada ya talaka ni kibaya zaidi ambacho ni ‘vita’ ya kugawana mali.

Ndoa zinapodumishwa kwa mtindo huo zinakuwa si mfano bora wa ndoa inayopendwa na sheria. Sheria inataka ndoa idumishwe kwa kuwa ndani yake yapo mapenzi na kuhurumiana.

Zipo sababu kadhaa zinazochangia kuvurugika au kuvunjika kwa ndoa nyingi.

Moja, wanandoa kuingia katika ndoa bila ya maandalizi. Wanandoa hawaandaliwi kielimu kwa kuwa hakuna mfumo maalumu na madhubuti wa kuwapa elimu wanandoa ili kila mwanandoa ajue wajibu wake na haki zake. Kifupi hawana mwongozo.

Mbili, utafutaji wa wachumba kutozingatia maelekezo na mafunzo ya dini. Dini imefundisha pande mbili za mume na mke zizingatie dini ya mwanamke na dini ya mwanamume.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Mwanamke huolewa kwa mambo manne: kwa mali yake, kwa ukoo wake, kwa uzuri wake na kwa dini yake. Mpate mwanamke mwenye dini, (kama hukumpata mwanamke mwenye dini) imepata hasara mikono yako”.

Dini hapo inatajwa kama sifa kuu za kumtafuta mke.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) akasema tena: “Akikujieni ambaye mnairidhia tabia yake na dini yake muozesheni”. Hapo kupitia hadithi hiyo linadhihiri somo na umuhimu wa kuangalia dini kwa mposaji.

Tukitafakari vyema tunaona kwamba dini ipo kotekote kwa mke na kwa mume. Leo hii jamii inakosea haiangalii tena dini kwa mume na mke. Familia ya mume inalenga uzuri wa sura na maumbile ya mke. Na familia za wanawake nazo zinaangalia zaidi fedha na kazi za wanaume waposaji.

Tatu, mfumo wa uchumba usiozingatia mafunzo ya dini. Unakuta wachumba wanaachiwa uhuru kama vile ndoa imeshapita kumbe bado. Mchumba na mchumba wanaachiwa wanatembea pamoja wakati mwingine wanasafiri pamoja na mara nyingine wanafanya tendo la ndoa kabla ya ndoa yenyewe.

Nne, sherehe nyingi za ndoa kufanyika kinyume na maelekezo ya dini. Unakuta bibi harusi anaonyeshwa kifua wazi na urembo ambao mhusika pekee anayetakiwa kuuona ni mumewe. Pia, wanawake ambao wengi ni wake za watu wanavaa mavazi yasiyo ya stara na siku za harusi wanaacha swala, na wengine hawaombi ruhusa kwa waume zao. Madhambi yote hayo yanaleta mkosi katika ndoa.

Tano, mume kutojua tabia za kimaumbile za mkewe. Ndoa nyingi zinavunjika kwa mume kutojua hilo kwani hudhania kuwa mke wake ni mjeuri kumbe sio hiari yake ni tatizo la kimaumbile kama vile mwanamke akiwamo katika ada yake ya mwezi (hedhi) au akiwa mjamzito. Mabadiliko hayo yanahitajia busara kubwa kwa mume.

Sita, migogoro ya wakwe. Katika ndoa nyingi hutokea mke kumchukia sana mama wa mumewe na kumsingizia upungufu ambao hana. Pia, hutokea mama mkwe kumchukia sana mke wa mtoto wake kiasi cha kumzulia ambayo hana na mwisho kumlazimisha mtoto wake amuache mkewe bila sababu za kisheria.

Saba, mke kumlazimisha mumewe matumizi makubwa yaliyo nje ya uwezo wake.

Nane, mume kumdharau mke wake. Baadhi ya wanaume huwadharau wake zao kwa kiwango cha mtu kumfananisha mkewe na akili za watoto wake wadogo, au anawadharau ndugu wa mke wake au hata wazazi wa mkewe.

Pia, anaweza kudharau mpaka chakula alichokipika mke wake na kumtajia wanawake wengine wanaojua kupika zaidi yake.

Tisa, mke kujiamini katika ndoa. Baadhi ya wanawake hujiaminisha katika ndoa na kujenga mazingira kwamba mumewe kamwe hawezi kutoa talaka na kamwe hawezi kumkosa.

Anapojiamini hivyo huwa anapunguza huduma na kujipendekeza kwa mumewe kwani ameshajiaminisha kwamba mumewe hana ‘chaguo mbadala’.

Kumi, mwanamke kutumia njia mbaya katika kukabiliana na tukio la mumewe kuongeza mke au wake wengine.

Baadhi ya wanawake hutokea pindi akiyakinisha kwamba mumewe ameongeza mke mwingine anafanya matukio ambayo badala ya kumrejeshea faraja yanazidi kumuongezea machungu na wakati mwingine anaweza kuamua yeye aachike na atoke katika ndoa.

Ni vyema katika jamii zeu tukawa makini juu ya ndoa kwani ndoa ni taasisi inayotarajiwa kufikia ukomo wake kwa kifo cha mwanandoa mmojawapo au wote.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation.

0 754 299 749/ 0 784 299 749



Chanzo: mwananchi.co.tz