Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Namna dini ya Uislamu isivyokubaliana na ugaidi

41919 Pic+uislam MAWAIDHA YA IJUMAA: Namna dini ya Uislamu isivyokubaliana na ugaidi

Sat, 16 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uislamu ni mfumo kamili wa maisha yote ya mwanaadamu; mfumo uliopangika kimwili na kiroho. Mafunzo ya Uislamu yanamfikisha mwanaadamu katika kuyajua yatakayomfaa hapa duniani na kesho akhera.

Miongoni mwa mafunzo ya Uislamu ni ‘kupeana amani’. Maamkizi ya Kiislamu ni kumtamkia mwenzako: ‘Amani iwe kwako’. Katika ibada ya Swala mwisho wake kuna kitendo cha kuwatakia wenzako amani.

Pepo ya Mwenyezi Mungu pamoja na raha zake zote, lakini kubwa zaidi imesifiwa kwamba ni ‘Nyumba ya Amani’.

Kutokana na muktadha huo, Muislamu hana hiyari kuwa ‘mtoa amani’ bali analazimika kuwa hivyo. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema:

“Muislamu ni yule ambaye wamesalimika Waislamu wengine na (madhara ya) mikono yake na (madhara ya) ulimi wake”

Akaongeza tena kwa kusema: “Muumini ni yule ambaye wamesalimika watu na shari zake”.

Kwa kuwa Uislamu ni amani na Muislamu analazimishwa kumpa amani Muislamu mwenzake na hata binadamu wote kwa ujumla, hivyo basi mazingira yoyote ya kumnyima mtu amani hayakubaliwi.

Uislamu na ugaidi

Ugaidi tafsiri yake ni kutumia nguvu ili kulazimisha matakwa fulani. Na magaidi siku zote wanasukumwa kufanya ugaidi kutokana na mambo makubwa mawili: kulazimisha matakwa ya kiimani au kulazimisha matakwa ya kisiasa.

Magaidi hutumia ugaidi kama ‘nyenzo’ ya kufikia matakwa na malengo yao hawaangalii tena uhai wa mwanadamu, viungo vya mwanaadamu na mali ya mwanaadamu.

Kwa kuwa ugaidi hauangalii na hauheshimu uhai, athari za viungo na mali; na Uislamu unaangalia vitu hivyo vitatu kwa jicho kubwa la uangalizi, ni dhahiri kwamba Uislamu haukubaliani na ugaidi.

Mwenyezi Mungu (Subhaanahuu Wataala) anakemea vikali mauaji kupitia Quran Tukufu katika Sura ya 4 (An-nisaai) Aya ya 93:

“Na yeyote mwenye kumuua muumini hali ya kukusudia malipo yake ni (kuingizwa katika moto) Jahannam atakaa milele humo na Mwenyezi Mungu amemchukia na amemlaani na amemuandalia adhabu kubwa.”

Amesema tena Mwenyezi Mungu katika Sura ya 17 (Israa) Aya ya 33:

“Na msiue nafsi ambayo ameharamisha Mwenye ezi Mungu (kuiua) ila kwa haki”

Akasema tena Mwenye zi Mungu katika Sura ya 4 (An-nisaai) Aya ya 29 (nanukuu):

“Na wala msijiue hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwahurumia.’’

Aya zote hizo tatu pamoja na nyinginezo ambazo sikuzitaja zinatufundisha ubaya wa kuua nafsi ambayo haina hatia ikiwemo mtu kujiua mwenyewe.

Ugaidi kwa mitazamo yake yote miwili (ugaidi wenye msukumo wa kiimani na ugaidi wenye msukumo wa kisiasa) ni jambo baya lisilokubaliwa na Uislamu.

Kwa upande wa ugaidi kwa misingi ya kiimani, msingi wake mkubwa ni kulazimisha watu waingie kwa nguvu katika dini au imani fulani. Mfumo huo tayari Mwenyezi Mungu ameukataa na ameukemea.

Mwenyezi Mungu amesema katika sura ya 2 (Al-Baqarah) Aya ya 256: “Hakuna kulazimisha katika (kuingia katika) Dini…”

Dhana ya kulazimisha na kuwataka watu waingie katika Dini ya Kiislamu kwa nguvu haikubaliwi na Uislamu wenyewe. Mwenyezi Mungu anasema katika Sura ya 10 (Yuunus) Aya ya 99:

“Na lau angetaka Bwana (Mola wako) wangeliamini walioko ardhini wote, Hivi wewe unataka kuwalazimisha watu mpaka wawe wote ni waumini?”

Kwa muktadha wa aya hizi, kuwaua watu na kuwadhuru kwa namna yoyote ile kama njia ya kuwaita katika dini, hilo halikubaliani na Uislamu. Hivyo basi anayefanya ugaidi kwa misingi ya kiimani huyo anakosea na Uislamu haukubaliani naye.

Amma ugaidi kwa msukumo wa kushinikiza matakwa ya kisiasa, hilo pia halikubaliwi na Uislamu kwani Uislamu hautaki kuuondoa utawala kwa misingi ya fujo na umwagaji wa damu kwa kuwa huko kwanza kunamaanisha kujiondoa katika utii wa mtawala na Uislamu unakemea vikali kujianzishia mamlaka mpya ndani ya mamlaka halali.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Yeyote ambaye ametawala kwake mtawala akamuona anatenda jambo la kumuasi Mwenyezi Mungu na alichukie jambo hilo, lakini asijitoe katika utii (wa mtawala huyo).’’

Ni vyema tukafahamu kwamba ugaidi kwa sura zake zote haukubaliani na Uislamu kabisa, na baya zaidi ni pale gaidi anapoamini na kuaminishwa kwamba anapoua au kujiua katika kadhia ya ugaidi anapata Pepo. Malipo mema anayapataje mtu aliyepoteza uhai wa wenzake wasio na hatia?

Na kama gaidi anaamini kwamba yeye ni mchamungu, kwa nini anahalalisha kujiua badala ya kubakia ili aendeleze ibada za Swala, Zaka, Hijja, Swaum,kulea familia, kuwahudumia wazazi, yatima, wajane na kadhalika? Kwa nini anaona kufa tu au kuua ndio ibada?

Ni vyema tukasahihisha uelewa kwamba kosa lolote likifanywa na mtu au kikundi cha watu ambao ni wafuasi au waumini wa dini fulani, hilo jambo madhali dini husika haifundishi na haielekezi hivyo basi ifahamike kwamba huo sio msimamo wa dini bali ni udhaifu wa mtu huyo tu na dini yake haihusiki.

Ipo mifano kadhaa katika kadhia hii. Kwa mfano, Adolf Hitler ambaye alikuwa mtawala wa zamani wa Ujerumani, mauaji aliyoyafanya yatabakia kuwa ni kosa lake yeye na utawala wake wala sio dini yake.

Mwandishi wa makala haya ni mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation.

0754 299 749/ 255 784 299 749.



Chanzo: mwananchi.co.tz