Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Lengo la mwanadamu kwa mujibu wa Quran na Sayansi

31623 Pic+mawaidha TanzaniaWeb

Fri, 14 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Huko nyuma tumeona kwamba swali muhimu kwa mwanadamu ni nini chanzo changu? Tumeona jibu la swali hili kwamba mwanadamu ni kiumbe wa Mwenyezi Mungu. Swali linalofuatia kwa umuhimu ni je nini lengo la kuumbwa mwanadamu?

Kwa maneno mengine ni lipi lengo la maisha haya ya dunia? Sambamba na umuhimu wa swali hili la pili kwa umuhimu ni swali la tatu; nani amjulishe mwanadamu juu ya lengo hili?

Kimsingi, swali la tatu lingepaswa kuwa ndiyo swali la pili lakini huwezi kutoa jibu la nani amjulishe mwanadamu lengo la kuumbwa kwake wakati lengo lenyewe halijui. Kwa mantiki hiyo tutaanza na kujibu swali, je ni nani amjulishe mwanadamu kuhusu lengo la kuumbwa kwake.

Siku moja katika uhai wa Mtume Muhammad (S.A.W) bwana mkubwa mmoja wa kabila la Kikureshi pale Makka aitwaye Umayyah bin Khalef alikwenda makaburini akaokota mfupa uliooza akaja nao mbele ya Muhammad. Akamuuliza hivi, “ewe Muhammad, unasema tukishakufa na kuoza kama mifupa hii tutarejea tena kuwa hai? Mtume Muhammad hakumjibu bali Malaika Jibril (Gabriel) akateremka na aya isemayo,

“Na ametupigia mfano na akasahau uumbaji wake. Amesema ni nani ataifufua mifupa hii hali ya kuwa imeoza? Sema ataifufua yule aliyeianzisha mara ya kwanza, naye naye ni mwenye kuwajua viumbe wote” (Qur’an 36:79).

Nimeileta aya hii kwa mnasaba wa kuyachukua maneno haya; “...naye ni mwenye kuwajua viumbe wote”. Hapa ndipo lilipo jibu la swali letu kuhusu nani amjulishe mwanadamu lengo la kuumbwa kwake.

Tunapata jibu kwamba ni yule aliyemuumba mwanadamu ambaye ni mwenye kuvijua viumbe wake wote. Na hili linaingia akilini kwamba mtengenezaji wa mtambo fulani ndiye mwenye uwezo wa kutoa maelekezo ya jinsi ya kuutumia mtambo huo.

Ukinunua gari kutoka Japan ya aina fulani au hata modeli fulani, utataka upate kitabu cha maelekezo ya jinsi ya kuiendesha gari hiyo, kuifanyia matengenezo na kadhalika.

Huwezi kuchukua kitabu cha maelekezo ya jinsi ya kutumia gari gari yoyote tu. Kitakachotokea ni ama kushindwa kuitumia gari hiyo, kuiharibu au wewe mwenyewe kuhatarisha maisha yako.

Hivyo basi, anayestahiki kumwelekeza mwanadamu lengo la kuumbwa kwake au uhai wake ni Mola Muumba, kwa sababu si tu anamjua mwanadamu bali pia kwa kuwa ndiye muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo. Yeye Ndiye anayevijua hivyo ambavyo mwanadamu atavitumia ili kulifikia lengo lake.

Lengo la uhai wa mwanadamu kisayansi

Kwa wale wanaoamini nadharia ya “kuumbika kwa kubahatisha” au chance creation inayohubiriwa na wanasayansi kupitia nadharia ya Darwin ya mabadiliko ya viumbe maarufu kama ‘Theory of evolution, maisha ya mwanadamu hayana lengo.

Kuna majawabu 25 ya swali ni lipi lengo la maisha ya mwanadamu yanayopatikana kwenye tovuti www.quora.com. Moja ya jibu hilo ni lile litokanalo na Fizikia. Hili linasema hivi.

“According to Physics, we are no different than lifeless rocks, in a way, we are all just matters (energy)”. Maana yake ni kwamba kwa mujibu wa Fizikia, sisi hatuna tofauti yoyote ile na mawe yasiyo na uhai na kwa namna fulani, sisi sote ni maada (kani) tu”.

Kama unashangaa jibu hili la Wanafizikia, soma jibu hili la Wanakemia. Wao wanasema, tafsiri ni yangu, “Sisi ni gunia la nyama la hatua za kikemikali (reactions) na tunapokufa miili yetu huoza na kurejea kuwa chembe za kujengea upya uhai”.

Kama vile jibu hilo halitoshi, Wanabiolojia nao wametoa ainisho lao la lengo la uhai wa mwanadamu. Wanasema: “lengo la maisha ni kuzaliana (au kuendeleza vinasaba vya uhai) kwa njia ya mwenza afaaye”.

Hivi ndivyo wale wasioamini mwanadamu kaumbwa na Mwenyezi Mungu wanavyolielezea lengo la uhai wa mwanadamu hapa duniani. Ukiyatazama majibu yao yote, utagundua kwamba hayo wanayoyaita malengo si malengo kamwe bali ni nyenzo za uhai.

Kwa hiyo basi pamoja na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, mwanadamu hawezi kuelezea lengo la kuumbwa kwake, kwa sababu suala hilo linaangukia katika ulimwengu nje ya ulimwengu wa mwanadamu yaani ‘metaphysical world’.

Hapo ni lazima mwanadamu arejee katika vitabu vya dini tena dini yenyewe iwe ile iliyotoka kwa Muumba na haikutiwa fikra za wanadamu; hapo anaweza kulijua lengo la kuumbwa kwake na hata jinsi ya kuliendea.

[email protected]

Chanzo: mwananchi.co.tz