Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Hivi ndivyo Sheria ya Ndoa inavyowakwaza Waislamu

88315 Pic+ndoa MAWAIDHA YA IJUMAA: Hivi ndivyo Sheria ya Ndoa inavyowakwaza Waislamu

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika dini ya Kiislamu, ndoa ni ibada kwa sababu ina nguzo zake, masharti yake na mfumo wake mpaka kufikia ukamilifu wa watu kuitana mke na mume.

Pamoja na Serikali kutoa uhuru wa kuabudu kwa raia wake, lakini uhuru uliotolewa katika ibada ya ndoa kwa Waislamu si timilifu.

Kukosekana kwa ‘uhuru timilifu’ katika ibada ya ndoa kunawakwaza sana Waislamu. Hivyo, ni juu ya Serikali kupitia vyombo vyake vya kurekebisha sheria ilitupie macho tatizo hili ili lipatiwe ufumbuzi kwa njia za hekima na busara.

Ndoa ya Kiislamu ambayo ikishafungwa kwa utaratibu sahihi za dini ya Kiislamu inaleta mambo makuu matatu: Uhalali na uhusiano wa kimwili kati ya mke na mume; kuthibiti nasabu ya mtoto anayezaliwa ndani ya ndoa kwa kiasi cha kumrithi baba yake au kama ni mwanamke baba kuwa na uwezo wa kumuozesha kisheria; na kurithiana mke na mume mmoja wao akitangulia mbele ya haki.

Mambo yote haya matatu yanayozaliwa na ndoa ya Kiislamu ni mambo yanayojengeka kiibada, kiimani na kisheria.

Utulivu uliopo katika jamii ya Kiislamu juu ya upungufu ya Sheria ya Ndoa ya Serikali inayoitambua sheria ya ndoa ya Kiislamu, unachangiwa na kutojua uhalisia wa tatizo na kutofuatilia matatizo ya kisheria mahakamani na katika mabaraza ya usuluhishi.

Ukweli ulio wazi ni kwamba yanahitajika marekebisho katika sheria ya ndoa ya Serikali, kutokana na sheria iliyopo sasa kuwakwaza Waislamu wa Tanzania katika maeneo na mifano ifuatayo:

Kwanza, Muislamu inatambuliwa ndoa yake lakini haitambuliwi talaka yake. Inapotokea mume Muislamu amemtamkia mkewe kwamba “amemuacha”, kidini mke huyo ameachika na yale mambo matatu tuliyotaja awali (yaani uhalali wa tendo la ndoa, kuthibiti nasabu ya mtoto na kurithiana) yameondoka yote.

Lakini kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Tanzania, talaka hiyo ya Muislamu haina uzito wala thamani yoyote katika vyombo vya sheria vya nchi mpaka kipatikane cheti cha talaka kutoka Mahakamani. Hivyo, hapo talaka ya Muislamu kwa mkewe haitambuliwi.

Pindi ikitokea mke aliyeachwa akaenda kudai mirathi au stahiki za ndoa mahakamani, mume Muislamu hawezi kuifanya talaka yake kuwa ni ushahidi kwani mwenye nguvu na mamlaka ya kutoa talaka ni Mahakama.

Hapo tunaona dini ya Kiislamu inasema huyo aliyetamkiwa kuachwa si mke tena wa huyu aliyetamka hilo, lakini sheria ya ndoa ya nchi inasema huyo bado ni mkewe mpaka kitakapopatikana cheti cha talaka cha Mahakama. Mkanganyiko huu unahitaji marekebisho.

Pili, Muislamu kupangiwa vipi ndoa ifungwe na nani afungishe ili itambuliwe na sheria za nchi. Kwa mujibu wa Uislamu, mwenye mamlaka ya kumuoza binti yake ni baba, babu, kaka, mtoto wa kaka au ammi (kaka au mdogo wa baba). Hao wanaitwa Mawalii wanaweza kuozesha au kuwakilisha na ndoa ikakamilika.

Hata kwa mujibu wa sheria za nchi, mwenye mamlaka ya kuifungisha ndoa ya Kiislamu ni Sheikh anayetambuliwa na sheria za nchi tena awe na leseni. Mwingine yeyote akifungisha ndoa, ndoa hiyo inaweza isitambuliwe kwani haina mashiko katika sheria za nchi, kwa kuwa imefungishwa na ambaye hana mamlaka hayo kwa mujibu wa sheria za nchi. Mkanganyiko huu nao unahitaji marekebisho.

Tatu, Muislamu anaweza binti yake kuozeshwa na Serikali kwa mume bila ya kutaka kwake baba (ridhaa ya Walii), wakati mwingine mume si Muislamu na Serikali inailinda ndoa hiyo.

Katika nchi iliyotoa uhuru wa kuabudu na kuyaacha mambo ya dini na kiimani kwa wananchi wenyewe, ni vipi inajiingiza katika kusimamia na kufungisha ndoa?

Mgogoro unakuja kujitokeza kwamba katika jicho la dini ndoa hiyo ya Serikali ni ‘uzinifu’ kwa kuwa hakuna ndoa (haikufuata taratibu za ndoa ya Kiislamu), lakini katika jicho la Serikali ndoa hiyo inatambulika kuwa ndoa sahihi tena inayoheshimika.

Anapofariki binti wa Kiislamu ambaye kaolewa kiserikali tena wakati mwingine na mume ambaye si Muislamu, yule mume ambaye si Muislamu atakapodai kurithi mali za mkewe kwa mujibu wa sheria za nchi kutazuka mgogoro mkubwa kwa kuwa sisi hatumtambui kidini kuwa ni mume.

Kitendo cha Serikali kufungisha ndoa wakati ndoa ni jambo la ibada na la kiimani, huko ni kuwaingilia wanadini. Serikali hapo imeingilia uhuru wa kuabudu wa Waislamu wa kukataa kumuozesha binti wa Kiislamu kwa mume asiye Muislamu mpaka asilimu.

Suluhu ya tatizo hili ni Serikali kupitia vyombo vyake vya sheria kuandaa mchakato wa rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya Mwaka 1971.

Katika marekebisho hayo, jambo la kwanza ni Serikali kujitoa katika suala zima la kufungisha ndoa na kuacha kadhia ya kuozesha kwa wanadini wenyewe.

Pili, marekebisho hayo yaitambue ndoa ya Kiislamu kwa ujumla wake na utimilifu wake. Isiwe kama ilivyo hivi sasa kwani Waislamu wamepewa uhuru wa ndoa lakini wamenyimwa uhuru wa talaka.

Serikali itambue kwamba tatizo hili ni kubwa kwani linaathiri mfumo wa mirathi ya Kiislamu ambayo pamoja na mambo mengine inazingatia uhalali wa ndoa ili mume na mke warithiane na ili baba na mtoto warithiane. Hekima na busara ni muhimu sana katika kuliendea suala hili.

Mwandishi wa makala haya ni mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. 0754 299 749

Chanzo: mwananchi.co.tz