Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAWAIDHA YA IJUMAA: Ewe mwanadamu mrejee Mola wako

45564 Pic+mawaidha MAWAIDHA YA IJUMAA: Ewe mwanadamu mrejee Mola wako

Sat, 9 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanadamu anajua jinsi umbile lake la mwili lilivyo zuri, lakini anashindwa kuifahamu ile Nguvu ambayo imesababisha umbile hilo liwepo.

Anauona mpango maridadi wa ulimwengu, lakini anashindwa kumuona Mpangaji wake. Anauona uzuri na uwiano mkubwa wa utendaji kazi wake, lakini hamuoni Muumba.

Anaiona sanaa nzuri ajabu katika maumbile lakini hamuoni Msanii! Je, mwanadamu aliyejitia upofu namna hiyo asiuone ukweli, anawezaje kuiona elimu sahihi? Je, mtu aliyeanza mwanzo wa upotevu namna hiyo, anawezaje kufikia mwisho mwema?

Mtu huyu atashindwa kuiona njia ya kuufikia ukweli. Njia sahihi itabaki ikifichikana kwake na hata kwa jitihada za sayansi na sanaa, kamwe hatoweza kuufikia ukweli na kupata hekima. Atakuwa anapapasa tu katika giza la ujinga.

Tunajua kuwa vyote vilivyomo ulimwenguni vinamtii Mungu. Kutii, kuishi kwa mujibu wa mpango wake na sheria yake, ni jambo lililopandikizwa katika umbile la vitu vyote. Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu mamlaka juu ya vitu vyote hivi, lakini ni shurti kuwa vitu hivyo vitumike kwa ajili ya kutimiza mpango wake na si vinginevyo.

Yeyote anayemuasi Mungu au anayeuendea ukafiri, huyo anafanya dhulma kubwa sana, kwani anatumia nguvu zake za kiwiliwili na akili yake kukiuka utaratibu wa maumbile na hivyo kuasi.

Anainamisha kichwa chake kusujudia miungu mingine badala ya MwenyeziMungu na anajenga moyoni mwake mapenzi, heshima na hofu juu ya nguvu nyingine bila kuzingatia msukumo wa silika wa viungo hivi.

Anatumia nguvu zake pamoja na vitu vyote hivyo alivyo na mamlaka kuupinga mpango ulio wazi wa Mungu na hivyo husimamisha utawala wa dhuluma.

Epuka dhulma ewe mwanadamu

Je, kuna dhulma kubwa, udhalimu mkubwa na ukatili mkubwa kuliko huo ulioonyeshwa na mtu huyu ambaye anakitumia vibaya kila kitu kilichopo chini ya jua na kuvilazimisha kufuata utaratibu unaokiuka maumbile na haki?

Kufuru sio dhulma tu; ni uasi, utovu wa shukrani na utovu wa imani. Tangu hapo ni ipi nafasi halisi ya mwanadamu? Uwezo na mamlaka yake yanatoka wapi? Je, yeye mwenyewe ndiye aliyeumba akili yake, moyo wake, roho yake na viungo vingine vya mwili? Au vyote hivi vimeumbwa na Mungu?

Na ni nani huyo anayetumia akili yake kufikiri dhidi ya Mungu; anayetia moyoni mwake mawazo dhidi ya Mungu na anayetumia vipawa vyake mbalimbali dhidi ya amri ya Mfalme?

Mtumishi anapomuasi bwana wake, tunamshtumu kuwa si mwaminifu (mtiifu). Kiongozi anapokosa uaminifu kwa nchi yake, tunamuita muasi na haini, na mtu anapomdanganya mfadhili wake hatusiti kumshtumu kuwa hana fadhila.

Lakini matendo hayo hayawezi kulinganishwa na lile ambalo kafiri analitenda kwa ile kufuru yake. Vyote alivyonavyo mwanadamu na vyote anavyotumia kwa manufaa ya wengine ni neema ya Allah.

Deni kubwa kabisa analodaiwa mwanadamu hapa duniani liko kwa wazazi wake. Lakini nani aliyepandikiza mapenzi ya watoto katika moyo wa wazazi? Nani aliyeyemjalia mama uchungu na uwezo wa kuwalea, kuwatunza na kuwalisha wanawe?

Yeye ndiye Muumba wake, Mola wake, Mlezi, Mkuzaji , Mfalme na Mtawala wake. Sasa basi upi ni usaliti, utovu wa shukrani, uasi na uhaini mkubwa zaidi ya kufuru ambayo kwayo mwanadamu humkana na kumuasi Bwana na Mtawala wake?

Msidhani kwamba kwa kufanya kufuru mwanadamu analeta au anaweza kuleta hasara hata kidogo kwa Mwenyezi Mungu. Kijichembe kiduchu kama mwanadamu juu ya uso wa kijigoroli kidogo ndani ya ulimwengu huu mkubwa, usio na kikomo cha mipaka, kitamdhuru nini Bwana wa ulimwengu huo ambaye mamlaka yake ya utawala yasiyo na ukomo, yameenea kote kiasi ambacho sisi bado hatujafaulu kuvumbua mipaka yake hata kwa msaada wa darubini kali?

Uasi wa mwanadamu hauwezi kumuathiri chochote, bali, kwa upande wake, yeye mwanadamu ndiye anayeiendea mwenyewe njia ya maangamizi na hizaya kwa huo uasi wake. Matokeo ya uasi na ukanushaji huo wa ukweli halisi ambayo ni muhali kuepukika, ni kushindwa kwa vigezo vikuu vya maisha.

Muasi huyo kamwe hatopata upenyo wa elimu na uoni sahihi; kwani elimu ambayo inashindwa kumbaini Muumba wake, haiwezi kuubaini ukweli.

Akili na uwezo wa kufikiri mtu huyo siku zote huenda kombo; kwani akili inayomkosea Muumba wake haiwezi kuangaza njia sahihi ya maisha.

Mtu huyo atakumbana na matokeo hayo ya kushindwa katika mambo yote ya maisha haya. Maadili yake, maisha yake ya kiraia na kijamii, harakati zake za kutafuta maisha na maisha ya familia yake na kwa kifupi maisha yake yote hayatokuwa shwari.

Mtu huyo hutibua ushwari na utulivu wa maisha katika dunia. Na katika maisha ya Akhera atatiwa hatiani kwa maovu aliyofanya dhidi ya umbile lake. Kila kiungo cha mwili wakem kitalalamikia udhalimu na ukatili aliovifanyia.

Kwa hisani ya www.islamictides.com



Chanzo: mwananchi.co.tz