Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAHUBIRI YA JUMAPILI: Unavyoweza kupona kupitia damu ya Yesu

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shaloom! Shaloom wana wa Mungu, jina langu naitwa Mtume Dk Peter Nyaga kutoka Kanisa la RGC - Miracle Center Tabata-Chang’ombe (Dar es Salaam).

Wapenzi wasomaji wa gazeti hili la Mwananchi, leo nimekuja na habari njema kwa mwaka huu mpya 2019.

Habari hizi ni somo linalohusu ‘Nguvu ya damu ya Yesu Kristo katika maisha yako.’

Jambo la kwanza ambalo mtu anapaswa kujua ni kwamba damu ya Yesu Kristo ipo hai na kupitia hiyo mwanadamu anapata uponyaji. Damu ya Yesu ilimwagika msalabani wakati aliposulubiwa kwa ajili ya makosa yetu wanadamu.

Tangu wakati huo damu ya Yesu imekuwa ikifanya mambo mengi sana kwenye maisha yetu na ndio maana hata Wakristo tunapofanya maombi yetu huwa tunatumia nguvu ya damu ya Yesu.

Nataka nikuambie kwamba damu ya Yesu ndio inayoweka agano kati yetu na Mungu, inaweza kuondoa dhambi, magonjwa, laana, mikosi na mabalaa.

Kiuhalisia dhambi huwa inatutenganisha na Mungu wetu na ni damu ya Yesu inaweza kurejesha uhusiano huo baina yetu na Mungu. Kabla ya kuongea zaidi kuhusu umuhimu wa hiyo damu ya Yesu acha kwanza tuangalie madhara ya dhambi kwa wanadamu.

Katika kitabu cha Isaya 56:2, Biblia inasema: “Lakini maovu yetu yametutenganisha na Mungu.”

Kama dhambi inaweza kukufarakanisha na Mungu ni nini sasa kinaweza kurejesha uhusiano wako na Mungu tena wakati unapokuwa umefanya dhambi? Bila shaka ni damu ya Yesu.

Jambo la pili unapofanya dhambi unajiona kuwa ni mtu mwenye hatia. Dhambi inatufanya tujione watu wenye hatia. Katika Zaburi 38.4 imeandikwa ‘Maana dhambi zangu zimenifunika kichwa kama mzigo mzito.’

Mstari huu wa Biblia unamaanisha kuwa unapofanya dhambi inakufunika, wakati ule wa agano la kale watu walikuwa wanatumia damu za wanyama, kama ukitenda dhambi unaenda kwa kuhani na anakumwagia damu ya kondoo kisha anakuambia dhambi zako zimefunikwa.

Lakini katika agano jipya, damu ya Yesu Kristo haifuniki dhambi isipokuwa inaondoa dhambi.

Jambo la tatu, dhambi inamruhusu shetani kutushtaki. Ukisoma Ufunuo 12:10 imeandikwa kuwa yeye anawashtaki mbele za Mungu usiku na mchana.

Hii inamaanisha kuwa shetani amekuwa akitushtaki kila siku kwa Mungu pale tunapotenda dhambi, lakini damu ya Yesu inaondoa mashtaka.

Mpenzi msomaji, mashtaka unayoweza kushtakiwa kwa Mungu kwa sababu ya dhambi, nimekuja na habari njema kwamba hayo yote yanaweza kusafishwa kupitia damu ya Yesu Kristo kwa sababu ingali ipo hai. Kumbuka tofauti ya damu hiyo na nyingine ni kwamba mtu yeyote anapokufa au kuchinjwa damu yake huoza na kuanza kunuka lakini damu ya mwokozi wetu ingali ipo hai, inanena mema.

Kwenye Biblia tunasoma Kaini alivyomuua Habel na damu yake ikaanza kuongea kwenye ardhi mpaka Mungu akasikia.

Ndio maana Mungu alimuuliza Kaini, yupo wapi ndugu yako? Hata kama Kaini alijibu mimi sio mlinzi wake bado Mungu alisikia damu ikimlilia, ndivyo Biblia inasema.

Kiuhalisia damu ina tabia tatu, inaweza kuzungumza laana, kuzungumza baraka lakini pia inaweza kulia. Ndio maana mwanadamu akiuawa mwisho wake huwa anaonekana kwa sababu damu yake huendelea kulia kwenye ardhi.

Napenda kukuambia kuwa damu ya Yesu ukiitumia vizuri inaweza kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako.

Inaweza kukuponya, kuondoa laana, kufuta dhambi na hatia. Jambo pekee unalopaswa kufanya ni kuamini kwamba damu hiyo ina nguvu na ndio iliyomshinda shetani.

Nikuambie tu ukweli kwamba kuna nguvu kubwa unapoamini na kwa mwaka huu 2019 unaweza kuvuka vizingiti vingi ikiwa utaamua na utaweza kutumia damu yake katika kila unalofanya.

Nakuombea sana kama kuna aliyetenda dhambi yoyote akatoa damu wakiwamo waliotoa mimba wajue tu kwamba damu hizo hunena na ni damu ya Yesu inaweza kuzuia mambo hayo kwa sababu tunao ujasiri wa kumkaribia Mungu kupitia damu yake. Sisi ni wanadamu tunaweza jaribiwa na kutenda dhambi mara nyingi, je tunawezaje kujisafisha? Ni kupitia damu yake kwa sababu tayari tunajua nguvu iliyopo.

Sasa naomba nikuombee ili damu hiyo sasa ianze kunena mema katika maisha yako, ndoa yako, kazi yako na kila unachopitia ili ukafanikiwe.

Naamuru damu ya Yesu iondoe mikosi yote, laana na tabu. Nimalizie kwa kusema neno hilo. Kama ukiamini yote yanawezekana kwa yeye aaminie.

Imeandaliwa na Tumaini Msowoya



Chanzo: mwananchi.co.tz