Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAHUBIRI YA JUMAPILI: Saumu inayokubalika mbele ya Mungu kipindi hiki cha Kwaresima

49647 MAHUBRI+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Leo ni Jumapili nyingine njema ya mwaka huu wa 2019 tukiwa katika kipindi ambacho wengi wetu tumeamua kutubu na kurejea kwa Mola wetu.

Huu ni wakati mzuri wa kutafakari neno la Mungu ambalo peke yake lina uwezo wa kutupa utulivu mbele zake.

Siku ya leo tunaongozwa na Neno kutoka Kitabu cha Nabii Isaya 58: 6-9 “Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?

Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, Na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; Wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?”

Nabii Isaya anatajwa katika Biblia kama nabii aliyeleta nabii za hukumu na karipio.

Ujumbe wa Nabii Isaya unalilenga taifa lake mwenyewe, na pia mataifa mengine.

Anawaeleza ukweli juu ya maovu wanayoyafanya, na yale watakayoyapata kwa uovu huo.

Katika Roho ya kinabii, Isaya anatabiri yale yatakayotokea na anawaeleza wana wa Israeli kuwa atawatoa utumwani nao watakuwa huru.

Nabii Isaya anaweza kufananishwa leo na kiongozi yeyote yule katika jamii ambaye anayaona mateso ya watu wake wakiishi katika umaskini sugu na huku wageni wanaitafuna nchi, kwa kuvuna rasilimali za nchi bila woga wowote ule.

Ndipo kiongozi jasiri anainuka na kukemea tabia hiyo ovu na kuwarudishia watu wake msingi wa kuijenga nchi na kurejesha tumaini.

Nabii Isaya anapogeukia mambo ya kiroho, hasa katika suala la kufunga anabainisha mambo ambayo watu wamekuwa wakilalamika kwamba Mungu hawasaidii.

Lakini Mungu alijua kuwa kufunga kwao ni kwa unafiki, anawaambia kwamba hakuna kitendo chochote kile cha kidini ambacho kina thamani kwake kama hakitoki kwa wale ambao kwa unyenyekevu wanajitahidi kutii maagizo yake na ambao kwa huruma huwafikia wale wenye mahitaji.

Je Mungu amechagua saumu gani? Saumu ambayo Mungu anaikubali ni ile inayoandamana na upendo wake na kuwajali kwa kweli wale wanaoonewa.

Waumini ni lazima waelewe kwamba ndiyo wanatoa mafungu ya kumi, wanatoa sadaka mbalimbali, tendo hili pekee haliwaweki mbali na wajibu wao wa kuwapatia wahitaji mahitaji yao.

Tunatakiwa kushiriki chakula chetu na wahitaji, wenye njaa tuwape chakula, wasio na nguo tuwape nguo.

Hebu jiulize katika kabati lako la nguo una idadi ya nguo ngapi ambazo huzitumii, na wala hutarajii kuzitumia.

Mkristo hata na wewe ambaye sio mkristo lazima uchukue hatua ya dhati kuyaangalia mahitaji ya wengine kanisani kwenu, na kujitoa kuwasaidia kwa njia yoyote ile.

Kunapokuwa na upendo wa kweli kwa Mungu na kujali kwa kweli ustawi wa wengine, mkondo hufunguliwa kwa ajili ya baraka kamili za Mungu kuja katika maisha yetu.

Thawabu za watu wa Mungu ziko wazi, nuru ya Mungu na uponyaji na wokovu huwapata watu wake.

Ulinzi wa Mungu unakuwa juu ya maisha yetu na yeye hutatua shida zetu.

Pamoja na faida binafsi za kufunga, Mungu anatuimarisha kiimani, miili yetu inaimarika na tunakuwa na afya bora ya mwili na roho hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima.

Wengi wetu tunatubu makosa yetu, lakini ni vema zaidi kuiendeleza tabia hii ya kumheshimu Mungu, hata na wale tunaoishi nao.

Mtu mzima hapaswi kuwa na tabia mbaya na ufahamu hata kama unaweza kuamua kufanya uovu wako mbali na nchi yako kumbuka hati hiyo ya mashitaka ataishikilia shetani na atakusumbua nayo sana.

Mungu atusaidie kufunga midomo yetu na kutoa maneno yenye baraka kwa wengine kama wazazi wetu, wanaotuzunguka na kwa nchi yetu.

Toa maneno ya baraka kwa viongozi wetu mbalimbali wakiwamo wa dini, Serikali na mahali pengine kwa sababu tunapaswa kuwaheshimu.

Kama ukifanya hayo yote, saumu yako itapata kibali mbele za Mungu.

Amen.

Imeandaliwa na Tumaini Msowoya



Chanzo: mwananchi.co.tz