Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAHUBIRI YA JUMAPILI: Mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu ni uzima wa milele

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Neno linasema ‘Bwana Mungu akapanda bustani upande wa Mashariki mwa Edeni akamuweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya’.

Tuombe; Mungu wetu baba wa Rehema wewe ndiye uliyefanya bustani ya Edeni na ukamuweka mwanadamu ili aitunze, aimiliki kwa utukufu wako nami ninaomba kwamba umemuweka mwanadamu katika ulimwengu huu na umemuweka Mtanzania katika nchi ya Tanzania ili aitunze kwa utukufu wako. Amen.

Mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu ni uzima wa milele.

Toka mwanzo Mungu aliweka mpango wa uhakika kwa mwanadamu na hii inathibitika na uumbaji wake ambao ni mkamilifu katika idara zote na kuwa ameweka uzima ndani ya mwanadamu.

Mungu aliumba nchi, anga na wanyama na akaweka kila kitu mahali pake.

Kila kitu ambacho Mungu aliumba kilikuwa chema na tunaona akamuumba mwanadamu mwenye mwili, roho na nafsi.

Sasa kuna kitu ambacho huwa nachunguza kwenye maandiko. Hivi ubaya wa mwanadau unaanzia wapi?

Sote tunajua kuwa Mungu ana upendo, haki na utakatifu. Ufahamu wa Mungu hakuna anayeweza kuupima.

Utukufu na heshima ni vyake Mungu kwa hiyo madaraka yote, usultani, mamlaka na enzi ni vyake Mungu.

Mungu aliwabariki Adam na Hawa na aliwapa vyote ambavyo walikuwa wanahitaji kwa hiyo akamuandalia mwanadamu bustani ya Edeni na kuwaweka humo.

Ni katika bustani hiyo mwanadamu alipata baraka akibarikiwa kwa uzuri. Alipata chakula chake, akaweza kufanya uchaguzi, kazi na shughuli mbalimbali.

Alipewa bustani alime na kuitunza na aliona si vema Adam awe peke yake akampatia mwenzi wake.

Tanzania inaweza kufananishwa na Edeni. Ukisoma mstari wa 10, kuna maneno. Ukatoka mto katika bustani ya Edeni na kuitilia bustani maji.

Tunaambiwa kwenye bustani ile kuna madini kama dhahabu safi na vito shoham.

Hapa umetajwa mto mmoja, Tanzania kuna mito mingapi? Kuna Ruvu, Wami, Pangani, Rufiji na midogo midogo isiyo pungua 60 ikitiririsha maji mwaka mzima.

Pamoja na kuwa na mito mingi, inakuwaje nchi ambayo haina mito mingi kama Israel imediriki kuwa na kilimo cha umwagiliaji maji mwaka mzima?

Ni nchi yenye jangwa wameleta udongo toka nchi nyingine na kuweka sehemu yenye jangwa. Nchi hii inaongoza kwa kuuza matunda matamu duniani. Huu ni mwaka ambao Tanzania itafunguka fikra zetu tuige kutoka mataifa yaliyofanikiwa au tukawapeleke vijana wetu wakajifunze masuala ya kilimo, madini.

Kama ni kutunza mazingira basi twende kujifunza kwenye nchi zilizofanya hivyo, tuna fursa ya kwenda kujifunza na kuja kuboresha hali ya kiuchumi, kiafya, kijamii hata michezo.

Katika somo hili tumejifunza kuwa kwenye ardhi kuna dhahabu safi. Tanzania kuna nini? Kuna nchi nyingine unaweza kukuta madini ya aina moja.

Tunayo sababu ya kuacha kujishughulisha na utajiri ambao Mungu ameweka kwenye nchi yetu? Kwa nini tunashughulika na mambo ambayo yanaturudisha nyuma?

Unaweza kukuta watu wanazusha mambo ambayo badala ya kutumia utajiri huu na kuboresha maisha ya Mtanzania aliye kalia utajiri huu, watu wanazusha mambo kukorofisha akili za watu zijadili mengine na watu waendelee kuwa maskini na kubaki katika hali mbaya.

Tunajishughulisha na nini? Nimeshuhudia hata katika miaka iliyopita sijaona msomi amegundua mambo fulani.

Tumetangaziwa Tanzania ya viwanda sijaona wasomi wamejiunga hata kufufua viwanda Rais atusapoti. Sioni, lakini watu wanajadili mambo yasiyo na mwanzo wala mwisho.

Tunayo sababu ya kulia njaa kweli? Katika nchi hii yenye utajiri wa kutosha?

Je kweli tunakosa kiwanda cha kuweka na kuchakata matunda? Adam na Hawa walichagua kutosikiliza wala kutii maagizo ya Mungu.

Uasi wa Adam na Hawa uliharibu uhusiano wake na Mungu. Lakini Mungu ana upendo, anazidi kumpenda Mtanzania, hawezi kukuacha uharibiwe.

Watanzania turudi kwake Mungu, tukae katika uongozi wake, Watanzania tunahitaji kupona katika roho na fikra zetu.

Usigombane na jirani yako, wanasiasa msigombane, watu wa dini msigombane, gombana na hali yako wewe inayosababisha hali mbaya kiuchumi.

Uzima ni kuishi kwa amani katika nafsi yako ukimpenda jirani yako, nchi yako, ukiwa mzalendo kwa imani yako na kudumu katika sala na Dua. Amen.



Chanzo: mwananchi.co.tz