Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAHUBIRI YA JUMAPILI: Mazingira yaliyolizunguka kanisa

55701 MAHUBIRI+PIC

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mada ya leo inaongozwa na kichwa kinachosema “Mazingira yanayolizunguka Kanisa”.

Pia tunaongozwa na neno kutoka Mathayo 13:25 linalosema, “lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

“Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika katika bonde lako? Limepata wapi basi magugu?. Akawaambia, adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, la; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno.”

Wakristo kote ulimwenguni wanakumbana na mambo ambayo huwa yanawavuruga mno.

Hakika mengine hawayapendi kabisa, lakini hawana nguvu ya kuyashinda yaani hayana mbinu za kuushinda uovu na udanganyifu huu hawana, na wakati mwingine hawajui elimu hii inatoka wapi?

Mfano huu kuhusu ngano na magugu unasisitiza kwamba shetani na malaika waovu atapanda uovu sambamba na wale wanaopanda neno la Mungu.

Shamba linawakilisha ulimwengu na mbegu njema inawakilisha waaminifu wa ufalme wa Mungu waliopo duniani.

Injili na waumini wa kweli watapandwa kwenye ulimwengu wote.

Naye shetani pia atapanda wafuasi wake ambao ni wana wa mwovu kati ya watu wa Mungu ili kuzuia ukweli wa Mungu.

Hapo kazi kubwa ya wajumbe wa shetani ndani ya ufalme wa Mungu inaonekana wazi kwamba ni kudhoofisha mamlaka ya neno la Mungu.

“Nyoka akamwambia mwanamke hakika hamtakufa…”, tunausoma huu mstari kutoka kwenye kitabu cha Mwanzo 3:4.

Ni katika uongo huu Shetani aliweza kupokonya mamlaka aliyopewa mwanadamu.

Shetani na wafuasi wake wana kazi moja tu kuendelea kucheza na akili ya mwanadamu kwa kusambaza mafundisho ya uongo.

Shetani hana kitu chochote anachokitumia zaidi ya kuchezea akili ya mwanadamu ili aamini na kufuata yale mafundisho yake yanayompinga Mungu.

Wapo watu leo wanaotumia alama za kishetani kwa kujua au wakati mwingine bila kujua.

Usishangae ukiwaona Wakristo nao wamo katika makundi haya wakitumia alama hizo.

Hali hii katika dunia inakuwepo kwa sababu kuna makundi mawili, watu wa shetani na watu wema wa Mungu.

Kwa maana hiyo ni Mungu peke yake atakayewatenganisha watu wa jinsi hii.

Wakristo wengi wanajiuliza, kwa nini Bwana Yesu akasema viacheni vyote vimee pamoja?

Yapo mambo ya kuangalia kwenye hili eneo. Katika kipindi cha injili hali ya kuishi kwa pamoja itakuwepo.

Mungu hataamuru malaika zake waangamize wana wa yule mwovu hadi siku ile ya hukumu ya mwisho.

Fumbo hili kamwe halipingani na mafundisho ya Biblia kuhusu kutenga washarika wanaoendelea katika dhambi na kuwatenga wasiotubu.

Waumini wa kweli, na wale waaminifu ni lazima wawe macho kutambua kila kitu kitumikacho katika ulimwengu huu.

Haitoshi kulifahamu gugu, je wewe ni ngano? Swali hili unatakiwa kujiuliza binafsi.

Pamoja na kwamba wanadamu wote wanafanana utawatambua kwa matendo yao, wewe mtoto wa Mungu ni mfalme, ni kuhani, mahali ulipo lazima upamiliki na kutawala.

Maombi ni moja ya silaha ambayo inapaswa kutumiwa na Mkristo ili kuzuia mambo mabaya yasitendeke katika jamii.

Kuna mambo gani ambayo yanakukera katika maisha? Je ukiona vitu vikifanyika katika ulimwengu wa roho na ule wa mwili; kisiasa, kijamii, kiutamaduni, kikanisa havikupendezi kabisa unachukua hatua gani?

Tunatakiwa kumuomba Mungu ili afungue ufahamu wetu kuweza kukabiliana na haya.

Hekima aliyotupa Mungu na maarifa vinatakiwa kutumika katika kukabiliana na mazingira yanayotuzunguka ili tumzalie Mungu matunda.

Unachopaswa kujua ni kwamba, hapo ulipo unatakiwa kuwa ngano kwa sababu neno la Mungu linasema mtamea pamoja, lakini mtajulikana baadaye kwamba nani ni gugu na nani ni ngano.

Utakuwa ngano kwa kutenda mema na unaweza kutenda mema kwa kumkaribisha Yesu kwenye maisha yako.

Mahubiri haya yataendelea Jumapili ijayo nitakapokufundisha alama za utambulisho wa shetani.

Imeandaliwa na Tumaini Msowoya



Chanzo: mwananchi.co.tz