Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAHUBIRI YA JUMAPILI: Kwaresma ni kipindi cha kutafakari zaidi juu ya maisha yetu na uhusiano wetu na Mungu

47160 PIC+KWARESMA

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Naitwa Askofu Jackson Sosthenes Jackson kutoka Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam.

Ni wakati mwingine tena nakutana na wasomaji wa Mwananchi katika eneo hili la kujifunza neno la Mungu.

Tupo katika kipindi cha Kwaresma. Neno Kwaresma ni la kiitaliano lenye maana ya “Siku arobaini za kufunga”.

Kipindi hiki kwa majira ya kanisa, wakristo huwa wanaanza kufunga siku ya Jumatano ya majivu yenye kuambatana na tendo la kupakwa majivu na kuhitimishwa Jumamosi Kuu kabla ya Pasaka yaani kufufuka kwa Yesu Kristo.

Kumekuwa na mitazamo mbalimbali juu ya dhana nzima ya Kwaresima hata wengine kuona kama si fundisho la kibiblia.

Ni kweli katika maandiko hatuwezi kuona neno Kwaresma likitajwa hata hivyo hatuwezi kupinga dhana ya kufunga kwamba ni jambo geni katika maisha ya taifa teule na katika historia ya ukombozi wetu tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya.

Maandiko yanatuonyesha katika kitabu cha Ester 4:1, Wayahudi walifunga na Mungu akawaokoa katika maangamizi ya maadui zao.

Watu wa Ninawi pia walitubu wakifunga na kuvaa magunia hata ghadhabu ya Mungu ikageuka kwao wasiangamie, tunasoma katika kitabu cha Yona 3:5-6.

Katika wakati wa huduma ya Yesu na maisha ya kanisa la kwanza, dhana ya kufunga ilikuwa ni moja ya tamaduni ya msingi kwa maisha ya ushindi kwa huduma na kanisa.

Hii ni kuthibitisha kwamba hata kama neno kwaresma halitokei katika maandiko lakini ni utamaduni na amana ya urithi iliorithiwa vizazi kwa vizazi na kuleta matokeo chanya kwa kanisa, taifa na hata maisha ya mtu binafsi.

Ni katika msingi huo katika karne za kwanza kanisa liliweka na utaratibu wa kufunga siku tatu kabla ya Sikukuu ya Pasaka ikiwa ni sehemu ya maandalizi katika kusherehekea siku hiyo muhimu kwa ukombozi wa maisha ya mwanadamu.

Hali hii iliendelea na baadaye siku ziliongezwa kuwa majuma mawili kabla ya Pasaka hadi kufikia mwaka 325 baada ya Kristo (BK).

Kupitia mkutano wa Nikea ziliazimiwa ziwe siku 40 kwa kufuata kama alivyofunga Mwokozi wetu siku 40, hata hivyo mnamo mwaka 601 BK ilipitishwa siku za Bwana (Jumapili) zisihesabiwe hivyo kufanya kuwa siku 46.

Yanaweza yakawepo malengo mengi mahususi kwa ajili ya Kwaresima hata hivyo tunaweza kuyaangalia machache na kuona jinsi gani Kwaresima inaweza kuwa na msaada katika maisha ya mkristo, kanisa, jamii na taifa tunapoendelea kufunga.

Kwanza Kwaresma ni kipindi cha kutafakari zaidi juu ya maisha yetu na uhusiano wetu na Mungu.

Kwaresima inatupa nafasi ya kila mmoja kusogea mbele za Mungu kwa karibu zaidi na hasa kwa toba na kufunga ili kuendelea kufanywa upya tukijivua utu wa kale na kuvikwa utu mpya ili tumuangalie Yesu na tuone utimilifu wa dhabihu yake msalabani.

Mtume Paulo anaandika, “Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho na nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa na MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli” (Efeso 4:22-24)

Hii ni kusema kufanywa upya kwetu ni pamoja na kuona waliokuwa hawapatani wakipatana, walioishi bila uadilifu wafanywe upya mioyo yao ili wakatae matendo ya rushwa na ufisadi, hata waliodhulumu na kuonea wanyonge watubu na kusema kama alivyosema Zakayo “…na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne” (Luka 19:8b)

Jambo la pili, Kwaresima ni kipindi cha kufanyika baraka kwa wengine hasa walio wahitaji. Wakati huu wa kufunga ni kipindi cha kuwajali wengine. Ni kipindi cha kujihoji kabla ya kuhitaji kupokea baraka kutoka kwa Mungu ni mara ngapi sisi wenyewe tumefanyika Baraka kwa wengine.

Ni rahisi watu wengi kutaka kupokea Baraka lakini si wepesi kutaka kufanyika baraka kwa wengine.

Maneno ya nabii Isaya yanatuasa; “Je! Saumu niliyoichagua, si ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umuonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; (Isaya 58:6-7)

Jamii yetu tumezungukwa na watu wengi walio wahitaji wakiwemo yatima na wajane. Hospitalini wapo watu wengi wenye kupungukiwa dawa na vifaa mbalimbali vya mahitaji muhimu. Mara ngapi tumeguswa na uhitaji wao? Mara nyingine tumedhulumu haki za yatima na wajane. Walio chini yetu katika dhamana mbalimbali tulizowekewa wakiwemo wasichana wa kazi majumbani, haki zao zimedhulumiwa na sauti za vilio vyao asiwepo wa kuwasikiliza. Kwaresima hii itutafakarishe kwa upya juu ya kufanyika kwetu Baraka kwa wengine kabla ya kutaka sisi kupokea Baraka.

Jambo la tatu, hiki ni kipindi cha kuiombea Serikali na nchi yetu. Ni lazima kuiombea nchi yetu na kumsihi Mungu juu ya ustawi na maendeleo mazima ya taifa hili kama ahadi ya Mungu inavyosema kwetu;

“Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya, basi, nitasikia toka mbinguni na kuiponya nchi yao”. (2Nyakati 7:14)

Imeandaliwa na Tumaini Msowoya.



Chanzo: mwananchi.co.tz