Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAHUBIRI YA JUMAPILI: Kuvunjika moyo haraka sio mapenzi ya Mungu, jua namna ya kushinda majaribu

Video Archive
Sun, 26 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jumapili ya leo nataka kuzungumza nawe kuhusu kukata tama.

Kuna watu wamepoteza mwelekeo kwenye maisha yao kwa sababu matarajio makubwa waliyodhani wangeyafikia hawakufikia.

Pia kuna watu wamepoteza mwelekeo kabisa na kujikuta wakikata tamaa baada ya kumaliza masomo yao na kubaini kuwa kazi walizotarajia kuja kufanya hazijatokea wala hakuna dalili ya kuzipata.

Wengine wamepoteza mwelekeo kwenye maisha yao walipogundua kwamba madeni makubwa waliyokopa benki imeshindikana kulipa na wale waliokuwa wakifanya nao biashara wamewadhulumu.

Wapo baadhi ya watu walipogundua kwamba watu wao wa karibu na wanaowazunguka kila siku kwenye maisha yao ni wasaliti na wanafiki, wamepoteza mwelekeo wa maisha yao kabisa.

Habari njema ninazokuletea Jumapili ya leo ni kwamba haijalishi umekata tamaa kaisi gani, umeumizwa kiasi gani, jua jaribu utalivuka salama na lazima utafika mwisho. Sema moyoni mwako kwamba neno hilo ‘nitafika tu’ Ukweli ni kwamba kuvunjika vunjika moyo haraka kutokana na mambo magumu unayopitia si mpango wa Mungu.

Pia Soma

Biblia katika kitabu cha Zaburi 23: 4 imeandikwa ‘Naam nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti sitaogopa mabaya kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji.

Mungu anataka hata unapopita katika bonde la uvuli wa mauti, usikate tamaa wala kuvunjika moyo. Kuna tofauti kubwa kati ya kupita na kukaa kwenye bonde la uvuli wa mauti. “Biblia inasema nipitapo, sio ukaapo na leo nataka niwahubirie msikubali kukaa kwenye majaribu lakini kubalini kupita tu.” Mtu anayepita kwenye jaribu ni yule mwenye tumaini kubwa kwamba eneo hilo atalivuka na lazima atafikia mafanikio yake pasipo kukata tamaa.

Mtu anayekaa ndani ya majaribu kuna hatari atafia pale lakini anayepita ataendelea na safari na lazima atafika mwisho.

Wapo baadhi ya watu walifia kwenye majaribu kwa sababu walipokutana nayo walikaa pale pale lakini kama ukiamua kupita hautakufa, ilimradi tu umtangulize Yesu na umwambie, nataka kupita sitakaa.

Tafadhali unaposoma ujumbe wangu leo jisemee moyoni mwako ‘Bwana Yesu naomba neema yako juu ya maisha yangu, roho mtakatifu anitawale, aniongoze, anifunike nisife ndani ya majaribu haya lakini nitapita, nitashinda na nitafika mwisho’.

Wapo wanaosema kwamba ukiwa na Mungu hautapita kwenye majaribu, sio kweli kwa sababu watu wa Mungu, huwa wanajaribiwa sana.

Anayempenda Mungu sana na Mungu anampenda zaidi hivyo majaribu kwake ni lazima. Mungu mwenyewe alisema wakati Yesu anabatishwa kuwa ‘huyu ndiye mwanangu mpendwa ninayependezwa naye msikilizeni yeye’.

Angalia kazi ya msalaba, majeraha na namna alivyowambikwa msalabani. Ukijaribiwa sana na ukiwa na Mungu jua kwamba utashinda sana.

Ni sawa na mwanamke aliyekutwa na uchungu mkali, akipita kwenye jaribu hilo hupata mtoto mzuri na mwenye afya.

Kamwe usije ukafikiri kwamba mtu akilia sana amekataliwa na Mungu, kumbuka kuwa Yesu alilia sana mpaka akauliza Mungu wangu, mbona umeniacha? Ukweli ni kwamba Mungu hakumuacha.

Katika maisha si kila kilio ni cha laana vipo vingine vya Baraka. Unaweza kupata pesa nyingi ukaingia ndani kulia kwa sababu hukutarajia, Baraka nyingine zinaweza kukuletea machozi ya furaha.

Anayechafuka sana huoga sana, nguo iliyokunjika sana hunyooshwa sana kwa hiyo unapojaribiwa sana usikate tamaa utabarikiwa sana. Kuna watu wanapitia majaribu mazito mpaka ukimuona unaweza hisi amelaaniwa, hapana hajalaaniwa Mungu ameamua kumpitisha kwenye majaribu mazito ili amuandae kupokea muujiza na asicheze na hizo baraka.

Haleluya! Hakika Mungu hawezi kukupatia hela nyingi kama hujajiandaa ni lazima kwanza akuandae. Hujawahi kujiuliza kwanini Mungu hakuwahi kuisahau fimbo Misri? Mungu alijua kama angesahau fimbo ile bahari isingefunguka.

Kuna watu Mungu anaruhusu wakuambie maneno ya kukuchoma moyo, kukukatisha tamaa, wakuambie kinyume na ulivyotaka kusikia kumbe Mungu amewatuma wakuandae kupokea Baraka zinazokuja mbele yako.

Usije kufikiri watu wanaokuzunguka ambao wamekuwa mwiba kwako ni mashetani hapana, hao wanakunoa uweze kufikia ndoto zako za mafanikio, kikubwa usikubali kuvunjwa moyo kwa sababu hiyo.

Watu hao ni muhimu kando yako wanakusaidia uombe sana, uinue imani na ujisemee kuwa pamoja na yanayokuzunguka lazima ufike. Mtu ambaye anaweza kukujaribu na kukuumiza ni yule uliye naye karibu.

Ayubu alijaribiwa na mtu wa karibu sana akimsihi amkufuru Mungu wake. Usimtafute adui yako mbali, yupo hapo karibu na huyo ndiye anakusaidia unoe imani yako.

Kuna wasichana wamejaribiwa na wachumba zao, walipowapenda waliwaamini lakini matokeo yake walijeruhiwa na kuwaachia maumivu makali. Usikatishwe tamaa na jaribu hilo, Mungu anakunoa cha msingi usije sahau kwamba yeye ndiye mkuu na anaweza kukuvusha.

Chanzo: mwananchi.co.tz