Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lwiza: Malasusa hakufanya kampeni

Kkkt Askofuuuuu.jpeg Lwiza: Malasusa hakufanya kampeni

Tue, 29 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Msaidizi wa Askofu Kanisa Kuu la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Azania Front jijini Dar es Salaam Chediel Lwiza amesema Mkuu wa Kanisa mpya mteule Askofu Dk Alex Malasusa alishinda kwa haki katika uchaguzi uliofanyika usiku wa Agosti 24, mwaka huu.

Amesema haikuwa rahisi kutengeneza ushawishi wa maaskofu 27, makatibu 27 na maofisa watano wa kanisa waliokuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu iliyotoa dhamana ya kila mjumbe kupendekeza majina matatu kabla ya kufanya mchujo wa majina matatu yaliyokuwa yamejirudia kwa kura nyingi.

Lwiza ambaye hakutaja jina lolote lililohusika kusambaza taarifa hizo , ametoa kauli hiyo leo Agosti 28, 2024 wakati wa Ibada ya shukrani maalumu ya Dk Alex Malasusa kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa mkuu wa kanisa hilo kupitia Mkutano Mkuu wa 21 wa KKKT uliofanyika jijini Arusha.

Katika Ibada hiyo iliyoanza saa 4:00 asubuhi, Askofu Malasusa aliyekuwa ameongoza na familia yake amemshukuru Mungu kwa kupokea jukumu hilo.

Waumini wameshiriki pamoja naye kutoa shukrani ya pekee akiongozana na familia yake, wachungaji wa sharika mbalimbali za Dayosisi hiyo na maofisa wa kanisa.

Lwiza amesema Malasusa hakupiga kampeni wala kufanya ushawishi wowote kama inavyopotoshwa na baadhi ya watu aliodai kufanya uwakala wa kusambaza ushawishi wa uongo, ambayo ni kazi ya shetani.

“Hao wajumbe 60 wa halmashauri wakipata majina zaidi ya matatu yaliyopata kura nyingi, basi watapiga kura tena kati ya hao wengi waliopendekezwa ili kupata majina matatu, baada ya hapo wanapeleka kwenye mkutano mkuu kama majina pendekezwa,” amesema Lwiza.

“Kamati ya uchaguzi inaundwa kwenye mkutano mkuu baada ya halmashauri kuu kupitisha majina matatu, sasa wanaosema kampeni ilifanyika, ilifanyika vipi?,”amehoji Lwiza kifafanua:

Askofu Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani anachukua nafasi ya Askofu Fredrick Shoo aliyemaliza muda wake wa uongozo wa awamu mbili.

Anarejea tena kwenye nafasi hiyo aliyoihudumu kuanzia 2007-2015 alipomaliza na nafasi yake ikiongozwa na Askofu Shoo.

“Shetani ni baba wa uongo, bahati mbaya miongoni mwetu ni sisi wakristo hata watumishi kabisa wa kanisa tunaingia kumsaidia shetani kusema uongo. Ninaomba washarika wenzangu tusitende dhambi hiyo, nashukuru Mungu Baba Askofu (Malasusa) alinituma kuingia halmashauri kuu.”

“Kwa hiyo Askofu Malasusa hata angefanya nini, hata sisi tungefanya nini, hatukuwa na uwezo wa kupendekeza jina lake likapita. Nawahakikishia hapakuwa na kampeni. Mpaka tunaenda kwenye uchaguzi, hatukujua kama litaletwa jina la Malasusa, mpaka tuna-break halmashauri kuu hatukusikia.”

“Sisi tulishangaa tu majina matatu yanasomwa mkutano mkuu, tunaambiwa tumemleta Askofu Malasusa na waliomleta ni maaskofu wenzake 27, makatibu wakuu 27, maofisa watano, mkutano mkuu ulikuwa na haki ya kuchagua majina yaliyoletwa.

Amesema wakati wa kupiga kura pia katika mkutano mkuu uchaguzi ulikuwa wazi kwa makundi kupiga kura kwa awamu. “Katibu mkuu yule pale (akionyesha) alipita mbele akaita majina ya wajumbe 14 wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Baba Askofu Malasusa akaulizwa hawa ndio wajumbe? Akasema ndio.”

Katika ufafanuzi wake, Lwiza amesema wajumbe wa Dayosisi 16 wa kaskazini pia waliitwa mbele kwa uwazi wakapiga kura kama ilivyo kwa makundi yote ndani ya mkutano huo mkuu. “Kura zikapigwa na kila duru ya kura iliyopigwa Baba Askofu (Malasusa) aliongoza tena kura zilikuwa zikiongezeka kila duru.”

“Hapakuwa na kampeni, hapakuwa na ushawishi. Niliona namna ilivyokuwa ikimsumbua, nimeamua kusema hivi ili waelewe na tuondoke kwenye dhambi ya uongo na ushawishi wa uongo.Neno la Mungu linasema usimsingizie jirani yako uongo ila usemee mema.”

Amesema inasikitisha kazi iliyotakiwa kufanywa na shetani mwenyewe, lakini baadhi ya washarika wamekuwa wasaidizi wa kusaidia kusambaza uongo hatua iliyosababisha kugawa kanisa.

“Hiyo dhambi imetugawa kabisa inatupasua kwa maeneo, Yesu Kristo hajawahi kupasuliwa na waliopo ndani ya Yesu hawajawahi kupasuliwa. Tutashinda tu na kanisa litakuwa moja. Tuna Mungu mmoja, bwana mmoja anayeitwa Yesu Kristo.”

“Utafanya dhambi ya uongo, ushawishi kwa kitambo tu lakini utaishia kubaya. Sisi tutamuombea Baba Askofu (Malasusa) kwenye madhabahu zetu mpaka kieleweke. Hatutanyamaza. Na tutaomba kwa kumaanisha.Hatutaomba kwa kushindana.”

“Ndio maana katika ibada hii tumeandaa cha bwana ili tupate nguvu katika mwendo huu tunaoendea. Ninawasihi washairika tumuombee Baba Askofu (Malasusa) na Baba Askofu anayemaliza muda wake Dk Shoo, maaskofu wote na makatibu wakuu wote.

Kipindi kigumu

Katika ufafanuzi wake Lwiza ameamua kuweka wazi hisia zake kuhusu hali ya kanisa. “Niliseme tu hili neno ambalo sikupanga kulisema mbele yenu.”

“Hakuna kipindi kigumu kama kuongoza KKKT, ukubwa wa kanisa hili, misingi ya neno la Mungu na misimamo iliyowekwa na waanzilishi wetu ilijengwa katika neno la Mungu. Nyie mliofika hapa mnaweza kufikiri ni raha, furaha, kicheko .Mimi niwaombe msifikiri hivyo,” amesema Lwiza.

“Kuongoza KKKT siyo jambo jepesi bila maombi na bila kuomba. Alimaliza muda wake (Askofu Malasusa), tukafanya ibada ya shukrani na tukadhani ni muda wa kula pensheni.”

“Lakini Mungu akasema njoo umalizie kipande chako (kazi ya kuongoza kanisa), tunahitaji kumuombea hilo, kuombea Dayosisi na kanisa letu na viongozi wetu wote.”

Chanzo: mwanachidigital