JANA Wakristo kote duniani wameanza mfungo wa Kwaresma wa siku 40, ikiwa ni kipindi muhimu cha kiimani cha kufanya toba, kujitafakari na kuongeza juhudi katika kutenda mema.
Ni kipindi ambacho kinabeba taswira ya mateso aliyopitia Yesu Kristo katika siku 40 alipojaribiwa jangwani, kifo chake na hatimaye ushindi wa ufufuko wake ambao Wakristo wanaita Pasaka.
Kiimani, hiki ni kipindi cha kuvuka kutoka sehemu moja ya maisha ya kuishi katika dhambi na kudhamiria kuishi upande wa pili wa kutenda mema, kutubu kila wakati na kujitoa sehemu ya mali zetu na tulivyonavyo kwa wahitaji.
Kwa ufupi hiki ni kipindi kinachotukumbusha kujijenga katika maisha ya kujinyima na kujitoa kwa ajili ya wengine hasa wahitaji.
Hii ndio sababu Kanisa limeweka utaratibu wa mfungo kuwa wa namna nyingi ili kusudi la mwisho liwe kuwasaidia wengine kupitia matoleo kwa njia ya sala, mali na fedha kwa ajili ya yatima, wajane, wazee na wahitaji wengine kwa maana maandiko yameeleza wazi kuwa, hiyo ndio Dini ya kweli.
Kutokana na hilo, ni dhahiri Kwaresma inapaswa kutusaidia kuwa watu wema daima na si kwa msimu huu wa kufunga tu, bali tuwe na maisha yenye hofu ya Mungu, ya toba na msamaha kwa wanaotuudhi hata kama ni mara ngapi wanatutendea mabaya nasi pia kukumbuka kuomba msamaha watu tunaowaudhi na kuwakosea kwa kuanzia katika familia zetu, mitaani na vijijini na maeneo yetu ya kazi na biashara.
Natamani Kwaresma hii itusaidie kuwa sehemu njema katika jamii yetu. Tuweze kweli kujitoa kwa ajili ya wenzetu wanaohitaji msaada wetu na kufanya kazi kwa bidii tukiuweka mbali uvivu kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Mfungo kama huu unapaswa kuwakumbusha wenye dhamana ya uongozi popote kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa kuwa, dhamana hiyo tumepewa na Mungu na tuifanye kwa moyo wa upendo, busara na hekima badala ya kuwa sababu ya kuwavunja moyo watu unaowaongoza na kuharibu ndoto zao (hasa watoto majumbani).
Tuwasaidie wengine kufikia ndoto zao kwa kuthamini uwezo wao na matamanio yao. Kwaresma hii iwe sababu ya mtu mmoja kuguswa na funga yako ili ilete maana chanya badala ya kubaki kama kipindi tu kinachokuwapo kila mwaka na kupita.
Inasikitisha kuona kipindi cha Kwaresma kama hiki wizi na uporaji wa mali za umma na binafsi mitaani unapungua, lakini kikiisha, unarudi pale pale. Au mtu anaacha kabisa kulewa kwasababu ni mfungo, ukiisha anaokotwa mtaroni kalewa chakari. Hii haileti maana hata kidogo.
Kuna mambo mengine yapo ndani ya uwezo wetu kuyaacha na kubadilika na kuna mengine yanahitaji nguvu ya ziada ya Muumba. Hivyo mfungo huu utusaidie kunyenyekea na kumuomba Mungu atuwezeshe kuacha yalio chukizo mbele yake na kuishi maisha yanayompendeza yeye na wanadamu.
Tukumbuke kuwa Kwaresma ipo kutukumbusha kutenda mema si tu kwa watu tunaowafahamu, bali kwa jamii na Taifa zima kwa kila mmoja kuwajibika katika nafasi yake kuanzia mtoto hadi mzee, kiongozi na anayeongozwa.
Kwaresma njema.