Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuolewa kunavyowatatiza wanawake nchini

81007 Kuolewa+pic Kuolewa kunavyowatatiza wanawake nchini

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kwa wiki nzima iliyoisha, video iliyosambaa kwa kasi mitandaoni hadi kuibua ‘msemo mpya’ ni ya Mchungaji Getrude Rwakatare wa Kanisa la Mlima wa Moto, anayeonekana akizungumzia nguvu ya “upepo wa kisulisuli” wakati wa mahubiri kuhusu ndoa.

Mchungaji huyo anaonekana akiomba upepo huo uwasombe wanaume huko kokote waliko na kwenda kwenye kanisa lake ambako alikuwa amewataka wanawake wanaotaka kuolewa kujongea mbele ili afanikishie nia zao kwa nguvu ya upepo wa kisulisuli.

“Wanaume kutoka mashariki, magharibi, kaskazini, kusini waletwe na upepo wa kisulisuli. Wawaangalie wasichana wetu, wawaoe,” anasema Mchungaji Rwakatare katia video hiyo.

“Kama kuna msichana anahitaji kuolewa kimbia hapa mbele. Kuna upepo wa kisulisuli unamleta mume wako.”

Baada ya wito huo, video hiyo inaonyesha wasichana wakinyanyuka vitini na kumiminika eneo la mbele la kanisa hilo kwa ajili ya kupata baraka hizo za kuwa na mwenza.

Leo, Mchungaji Rwakatare atakuwa na maombi hayo anayoyaita ya “upepo wa kisulisuli”, akiwa amewaalika wanawake kwa wanaume kufika kwa wingi katika kanisa lake lililopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Video hiyo inawakilisha sehemu tu ya mikakati mingi ya kujaribu kusaidia wasichana ambao hawajapata waume mapema inayofanyika katika nyumba za ibada na sehemu nyingine.

“Nimekuwa na utaratibu wa kufanya maombi ya aina hii baada ya kuona kuna tatizo katika jamii la wanawake waliofikisha umri wa kuolewa kukosa wenza,” alisema Mchungaji Rwakatare katika mahojiano na Mwananchi.

“Sisi wachungaji huwa tunakutana na watu wenye matatizo hayo wengi, ukiangalia kanisa robo tatu ya wanaohudhuria ni wanawake na kila mmoja ana matatizo yake.

“Wapo ambao wanakuja kuniambia mama nahitaji kuolewa, naomba uniombee kwa Mungu nimpate mwanaume wa maisha yangu. Nikiwa kama mama huwa naumia sana kuona mabinti wanateseka na kuhangaika kupata wenza.”

Mchungaji huyo aliyataja mambo kadhaa yanayosababisha tatizo hilo kuendelea kutokea katika jamii kuwa ni vijana wa kiume kutokuwa tayari kuingia kwenye ndoa kwa kuogopa majukumu.

“Wapo wengine ambao hawaoni sababu za kuoa kwa kuwa kila wanapohitaji wanawake wanawapata. Wanasema kuna haja gani ya kufuga ng’ombe wakati maziwa unapata. Hii ni mbaya sana. Inatakiwa uwe na mke mfunge ndoa kabisa,” alisema.

“Labda sisi wanawake wenyewe tukiwa expensive (ghali) inaweza kupunguza tatizo hili. Mwanaume akikufuata, mwambie sawa tufunge ndoa kwanza. Hii itasaidia kupunguza matukio ya kuchezewa na kuachwa.”

Lakini Mchungaji Christosiler Kalata aliyekuwa Usharika wa Mbezi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), anaona tatizo la kukosa wenza linatokana na nguvu za giza.

“Mwanamke ambaye amepewa nguvu ya kuzaa hukumbwa na mapepo yanayomfunga ashindwe kumpata mwenza sahihi kwa wakati sahihi,” alisema.

“Ndio maana wakigundua wamefungwa, hukimbilia kwenye maombi na wanapoombewa wengine huanguka hivyo, baada ya maombi wengine huwa hawachukui muda mrefu hupata wachumba sahihi na kuolewa.”

Mchungaji Samweli Lwiza wa Kanisa la Joy Tample, Tabata Kimanga anasema idadi ya wanawake ni kubwa kuliko wanaume.

“Hakuna jinsi, ndiyo ilishakuwa hivyo. Jaribu kupiga hesabu kanisani wanawake wangapi na wanaume wangapi? Lakini nilichogundua wasichana wengi wanachagua sana,” alisema Mchungaji Lwiza.

Hata hivyo zipo, takwimu zinaonyesha kuwa kuna tofauti ndogo ya idadi ya wanawake na wanaume duniani. Dunia ina takriban ya watu bilioni 7.59 na kati yao wanwake ni bilioni 3.76 wakati wanaume ni bilioni 3.83.

“Mimi huwa nawaombea kisha nawatia moyo na nawaambia hali halisi ilivyo kwamba hata uko nje ya kanisa wasioolewa ni wengi tu na wanahitaji kuolewa,” alisema Lwiza.

“Huwa nawashauri vijana waoe, lakini jambo la ajabu vijana wanapenda kula nje kuliko kula ndani ya kanisa ambako mabinti wao wapo tayari.”

Maoni kama hayo yametolewa na Sheikh Alhadi Mussa Salum wa Dar es Salaam ambaye alisema kwamba idadi ya wanawake duniani ni kubwa kuliko wanaume ndio maana uislamu unaruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja.

Lakini Sheikh Mussa alisema baadhi ya vijana wanasita kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya changamoto za kiuchumi.

Katibu wa Baraza la Ulamaa kutoka Baraza Kuu la Kiislamu (Bakwata), Hassan Chizenga alisema takribani ndoa 10,000 za Kiislamu hufungwa kwa mwaka nchini.

Alisema idadi hiyo ni zile ndoa ambazo zimeingizwa kwenye kanzidata na kwamba zipo zile ambazo wanandoa wanachukua vyeti lakini hawavirudishi Bakwata aidha wengine hufunga ndoa bila vyeti.

Wanasaikolojia wanasemaje

Lakini mwanasaikolojia Modesta Kimonga alisema shauku ya kuingia kwenye ndoa inachangiwa na makundi rika na wengi hutamani kufanya kila wanachofanya wenzao wanaolingana nao.

“Baadhi ya wanawake na wasichana wamekuwa na shauku ya kuingia kwenye ndoa kwa sababu labda wenzake wote aliosoma nao wameolewa au wafanyakazi wenzake wameolewa,” alisema.

“Viongozi wa dini wamelitambua hilo na hiki kinachofanyika ni kuwapa faraja ili mtu asijione yuko peke yake. Ukweli ni kwamba huwezi kulazimisha vitu. Subira ni muhimu na kila kitu kinapaswa kufanyika kwa wakati.”

Simulizi za vijana

Simulizi za wasichana waliohojiwa na Mwananchi zinathibitisha kuwepo kwa tatizo hilo.

“Wasichana wengi huanza kulilia ndoa wanapogundua umri wao unasogea wakati hakuna mwanaume anayezungumzia ndoa,” alisema Anitha Mgezi, mkazi wa Tabata.

“Hii inatokana na tabia ya kuchagua wanaume. Kuna umri fulani wasichana huwa wanachagua wanaume wenye uwezo, wasomi au wenye maisha ya juu na wanakuja kustuka miaka 30 bado hawajaolewa. Hapo huanza kukimbilia kwa wachungaji,” alisema.

Lakini Mariam Kilyenyi anasumbuliwa na aliyoyaona.

“Nimewahi kushuhudia karibu ndoa tano za rafiki zangu ambao waliamua kujilipia mahari ili tu wafunge ndoa,” alisema.

“Kusema kweli wasichana wanapenda mno kuolewa kiasi wengine hujilipia posa na mahari, Nimeshuhudia kwa macho yangu, ujinga huo sifanyi.”

Kwa upande wake, Agnes Mangu alisema uhalisia ni kwamba wanaume hutaka mpaka wawe na uwezo mkubwa kimaisha ndipo waoe.

“Mwanaume anaweza kukaa hata miaka 40 na akitaka kuoa anaoa msichana mdogo kabisa lakini mwanamke ukichelewa kuolewa ni shida,” alisema.

Mtangazaji wa EFM, Maona Thobias pia anasema ndoa nyingi zimekuwa mfano mbaya kwa vijana kwa namna wanandoa wanavyoishi kwa migogoro huku baadhi yao wakisalitiana.

Aidha alisema, wasichana wengine wanahangaika kupata wachumba kutokana na tabia zao.

“Unakuta msichana usiku mkubwa yupo klabu anacheza muziki, akirudi asubuhi ni kulala tu na kibaya zaidi mavazi yake yanakuwa nusu uchi, huyo ataolewa na nani?” Alihoji.

Waziri Ummy: Kuna tatizo

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ambaye pia anahusika na ustawi wa jamii, alisema watu wengi wana changamoto katika maisha zinazowaathiri kisaikolojia ambazo huamini zitatatulika kwa maombi.

Alisema ili kuondokana na tatizo hilo, ustawi wa jamii na wataalamu wa afya ya akili lazima wafanye kazi yao.

“Wizara ya Afya inakusudia kuja na muswada wa sheria ili kuwafanya wataalamu wa magonjwa ya akili na wa ustawi wa jamii, waanze kutoa huduma kwa watu wanaohitaji huduma ya phsycho social surport,” alisema.

Waziri Ummy alisema wiki mbili zilizopita alitoa maelekezo kwa wataalamu wa afya ya akili wa Mirembe na Hospitali ya Taifa Muhimbili kuacha kusubiri wagonjwa mpaka wafike hospitali na badala yake waanze kutoa huduma kwa wahitaji mapema.

“Matatizo ya akili si lazima aje kichaa, msongo wa mawazo. Matatizo mbalimbali husababisha matatizo kisaikolojia, nimewaambia waondoke katika dhana ya kutibu wagonjwa wa akili,” alisema.

“Kuna mtu ana heshima yake anaweza kupata matatizo kama kuachishwa kazi. Huyu anafaa counceling. Hospitali iwe ni taasisi ya magonjwa ya akili ili waweze kutibu kisaikolojia kushirikiana na hospitali za rufaa za mikoa na wilaya kuanzisha phsycho social support.”

Imeandikwa na Herrieth Makwetta, Elizabeth Edward, Tumaini Msowoya na Asna Kaniki.

Chanzo: mwananchi.co.tz