Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumshambulia Kakrdinali Pengo ni kuinyanyasa demokrasia

86629 Pic+pengo Kumshambulia Kakrdinali Pengo ni kuinyanyasa demokrasia

Mon, 2 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rais John Magufuli alipokuwa ziarani Lindi na Mtwara alichombeza kuwa angetamani mwanamuziki Rajab Abdul ‘Harmonize’, awe mbunge wa Tandahimba.

Ukiichukulia kauli hiyo kwa uzito utakosea, mwenyewe alichombeza kuchangamsha mkutano na kweli ukachangamka.

Kwa Harmonize, kauli ya Rais Magufuli ilimjenga mno kibiashara na huwa anatangaza atagombea ubunge.

Polycarp Kadinali Pengo, hivi karibuni alisema kuwa huwa anawaza nchi hii akiondoka Rais Magufuli, nani mwingine mfano wake? Akasema angalau Paul Makonda, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam humpa matumaini.

Mitandaoni, Pengo anakosolewa kwa kauli yake. Pia kusanyiko la viongozi wa dini, ambalo lilitoa kauli chanya dhidi ya hali ya mambo inayoendelea nchini limepata ukosoaji.

Askofu Benson Bagonza wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, bila kutaja jina la mtu aliandika ujumbe uliosambaa mitandaoni, akikumbusha msamaha alioomba Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani,.

Aliandika kuwa Machi 2017, Papa Francis aliomba msamaha katika maeneo manne yaliyoonesha uhusika au mchango wa Kanisa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

Maeneo hayo manne ni, mosi, baadhi ya mapadri walifunga milango ya Kanisa kuwanyima hifadhi waliokuwa wakikimbia wasiuawe. Pili, baadhi ya mapadri waliwafungulia milango waliokimbilia kanisani, kisha waliwaita wauaji wawaue.

Tatu, kabla ya mauaji ya kimbari, baadhi ya mapadri na maaskofu walipaza sauti kusifia au kuunga mkono juhudi za aliyekuwa Rais wa Rwanda, Juvenal Habyarimana. Nne ni kwamba baadhi ya mapadri na maaskofu walikaa kimya kabla, wakati na baada ya mauaji hayo.

Kuhusu funzo baada msamaha wa Papa Francis, Askofu Bagonza alisema, kukaa kimya, kuunga mkono na kukaa katikati kunaua. Akashauri ukweli usemwe inapotakiwa kuliko kukaa kimya, na kwamba kukemea vibaya ni bora kuliko kupongeza vibaya.

Ukiweka ushauri wa Askofu Bagonza na msamaha wa Papa Francis pamoja, utaunganisha na maneno ya mwanafasihi wa Italia, Dante Alighieri, aliyeishi Karne ya 13 mpaka Karne ya 14.

Alighieri kupitia mfululizo wa mashairi yake ya Divine Comedy, aliandika: “The hottest places in Hell are reserved for those who in time of moral crisis preserve their neutrality.”

Kwa tafsiri yangu ya Kiswahili ni kuwa “Maeneo yenye kuunguza zaidi Jehanamu yamehifadhiwa kwa ajili ya watu ambao, kipindi kuna uvunjifu mkubwa wa maadili, hujifanya kutokuwa na upande.”

Kwamba uvunjifu wa maadili unapaswa kusemwa kama inavyotakiwa, si kuukalia kimya, haipaswi kusema huna upande kipindi cha uovu na dhambi iliyokubuhu, hiyo ni kupongeza uovu.

Hakuna dini inayoruhusu unafiki. Ushauri wa Askofu Bagonza ni wito kwa jumuiya ya viongozi wa dini na jamii kujitenga na unafiki. Papa Francis aliomba msamaha kwa sababu watu wengi waliuawa Rwanda chanzo kikiwa ni unafiki wa viongozi wa Kanisa. Alighieri akasema wanafiki sehemu yao Jehanamu ni yenye kuunguza zaidi.

Demokrasia isinyanyaswe

Mfano wa kilichotokea Rwanda ni funzo lakini si kifungo cha kidemokrasia na uhuru wa Kanisa na viongozi wengine wa kiroho kuipongeza Serikali iliyopo madarakani kama wanaona inafanya vizuri.

Kama Kardinali Pengo ameona Rais Magufuli amejenga viwango vya juu kiuongozi, kiasi ambacho si rahisi kupata mrithi wa kutosha viatu vyake, si kosa kusema. Na hiyo ndiyo haki ya kidemokrasia.

Ikiwa Pengo katika jicho lake, ametathmini na kujionea kuwa katika hivyo viwango vya juu vya kiuongozi vilivyowekwa na Rais Magufuli, ni Makonda pekee kwa sasa anayeweza kuvifikia, kumshambulia kwa kuusema ukweli wake ni kuinyanyasa demokrasia.

Falsafa ya demokrasia inataka ukweli uugawe katika makundi matatu; la kwanza ni ukweli unaoujua na kuuamini, pili ni ukweli anaoujua na kuuamini mwenzako, tatu ni ukweli ambao ndio ukweli halisi.

Je, wewe na mwenzako nani ambaye ukweli wake ndio ukweli halisi? Inawezekana ukweli unaoamini si ukweli, au mwenzako anachokisimamia si ukweli. Inafaa kabla ya kumshambulia ujishughulishe kuujua ukweli halisi. Na unapojiridhisha, kuwa ukweli wako ndio ukweli halisi, mwelimishe mwenzako.

Ukweli unaouamini unabaki kuwa ukweli wako kama huujui ukweli halisi. Na mwenzio ukweli wake anaona ndiyo ukweli, ikiwa hajui ukweli wenyewe. Dhambi ni kuujua ukweli halisi halafu unautetea ukweli wako unaopingana na ukweli.

Ni hivi, ukweli halisi unapodhihirika kwako, na kama ulichokuwa unakisimamia hakishabihiani na ukweli halisi, maana yake ulikuwa unasimamia uongo. Kuutetea uongo mbele ya ukweli halisi, ndio unafiki. Kuujua ukweli na kukaa kimya ukaacha uongo utawale ni unafiki.

Hivyo, kabla ya kumshambulia Pengo, vema kutambua kuwa anachokijua ni ukweli wake na ana haki ya kukitetea. Na inawezekana anachokisimamia ndio ukweli halisi, na wanaomshambulia, ukweli wao ndio uongo. Hivyo, hawezi kuuacha ukweli na kuushika uongo.

Kama ukweli wa wanaomshambulia ndio ‘ukweli halisi’, basi badala ya kumshambulia, vema kumwelewesha ili aujue ukweli. Ni kosa kumzodoa mtu kwa kusema anachokiamini ikiwa hajaeleweshwa vinginevyo.

Ni dhambi, ikiwa Pengo alisema kwa utani kuwa Makonda anafaa kuwa mrithi wa Rais Magufuli kama utani wa ubunge kwa Harmonize. Suala nyeti kama hilo halipaswi kufanyiwa utani na kiongozi mkubwa wa kiroho wa aina yake.

Endapo alichokisema sicho anachokiamini ni dhambi pia. Hivyo, kabla ya kumshambulia Pengo, ingekuwa vizuri kujiuliza kama maneno yake yalitoka moyoni? Kisha alindiwe heshima kwa anachokiamini.

Nyongeza ni kumkumbusha Pengo kuhusu uovu dhidi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi, kupotea mwandishi Azory Gwanda, kada wa Chadema, Ben Saanane, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye, kuuawa kwa risasi mwanafunzi, Akwilina Akwilini, nayo anapaswa kuyasemea. Ni mambo ya wazi kabisa.

Chanzo: mwananchi.co.tz