Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kishki TV yapata tuzo kutoka Youtube

5ff3351add5dd1215245cdc05865ea72 Kishki TV yapata tuzo kutoka Youtube

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KITUO cha televisheni ya mtandaoni cha Kishki Online TV kimetajwa kuwa cha kwanza nchini kwa vituo vya aina hiyo vya dini ya Kiislamu kupata tuzo ya fedha kutoka Shirika la Youtube la Marekani.

Tuzo hiyo (Silver Award) imekuja baada ya kituo hicho kilichoanzishwa Machi mwaka jana kufikisha watu 100,000 waliojisajili (subscribers).

Akipokea na kutangaza tuzo hiyo, Muhubiri wa Kimataifa wa Dini ya Kiislamu, Shehe Nurdeen Muhammad Al-Ahdal, maarufu kwa jina la Kishki, amewahimiza Watanza kupenda kusikiliza, kutazama na kusoma vyombo vya habari vya dini.

Amefafanua kwamba kupitia vyombo vya dini, watu watajifunza masuala mbalimbali ambayo Mwenyezi Mungu anataka viumbe wake wayafanye au waache ili kuishi vizuri hapa duniani na baadaye ahera.

Kishki aliwashukuru watazamaji wa kituo hicho zaidi ya milioni nane na hususani wale waliojisajili ambao sasa wamefikia 120,000 kwa kufanikisha tuzo hiyo na kuahidi kwamba wataendelea kutoa vipindi murua huku wakijipanga kurusha matangazo yao kwa njia ya satellite na hivyo kuonekana pia kupitia visimbuzi.

“Kwanza kabisa ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu amesema kwenye Kuran tuanze kwa kumshukuru yeye kwa jambo lolote na kisha wazazi wetu. Mtume Muhammad (SAW) akasema asiyewashukuru watu anaowaona basi ni vigumu pia kumshukuru Mwenyezi Mungu asiyemwona,” amesema.

Amewataka watanzania, hususani waumini wa dini ya Kiislamu kutotumia muda wao mwingi kwa kutamaza mambo ya kidunia huku wanapoona jambo la dini wakilikimbia kwani wanakosa mafunzo muhimu kwa ajili ya dunia yao na ahera.

“Unapotumia bando lako kusikiliza maneno ya Mwenyezi Mungu kupitia Kishki TV au vituo vingine vya dini usidhani unapoteza. Unalipwa thawabu na siku ya Kiama utaona malipo yako,” amesema.

Mapema akielezea safari ya mahaburi ya Shehe Kishki ambaye ameshatembelea zaidi ya nchi 15 na mikoa yote ya Tanzania kasororo Ruvuma, Shehe Abdillahi Massawe amesema Shehe Kishki alianza mahubiri ya dini ya Kiislamu mwaka 1995.

“Shehe alianza mahubiri misikitini bila kurekodiwa, baadaye tukawa tunarekodi kwenye mikanda ya kaseti ambayo baadhi ya vijana wa leo hawaijui, kisha kwenye mikanda ile mikubwa ya Video Home System (VHS), kisha kwenye VCD na DVD na kwa jinsi teknolojia inavyobadilika sasa tuko kwenye online TV,” amesema Shehe Massawe.

Baadhi ya vipindi vinavyorushwa na Kishki Online TV ni Street Da’awa (Mahubiri mitaani), Uislamu Katika Vitabu vya Kale, Pamoja na Kurani, Bulugh al-Maraami, Riadh as Salihiin na kile kinachoendeshwa na Kishki kila Ijumaa saa mbili na nusu usiku cha Fadhakir (Ukumbusho).

Chanzo: www.habarileo.co.tz