Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya Mchungaji kwa Magufuli sasa yaibua mapya

42648 Pic+jpm Kauli ya Mchungaji kwa Magufuli sasa yaibua mapya

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Halmashauri ya wilaya ya Serengeti mkoani Mara imekerwa na kauli ya kiongozi wa dini mbele ya Rais John Magufuli kuwa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo hauna tija.

Katika kikao cha maaskofu, masheikh na viongozi wengine wa dini na Rais Magufuli kilichofanyika Januari 23 mwaka huu, katibu wa kanisa la Menonite Tanzania, Mchungaji John Wambura alisema ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo unatakiwa kuangaliwa upya kutokana na ubia uliopo baina ya Hospitali Teule ya Nyerere ambayo inamilikiwa na kanisa na Serikali.

Katika ubia huo, Serikali inawajibika kulipa mishahara watumishi na huduma mbalimbali, wakati masuala ya ajira na uongozi yakiwa chini ya kanisa hilo.

Akizungumza mjini hapa jana, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Juma Porini alisema kauli ya mchungaji huyo mbele ya Rais haiwatakii mema na inakinzana na lengo la Serikali la kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

“Mtumishi wa Mungu kutoa mawazo hayo ni kuegemea maslahi ya kanisa ambalo linanufaika na ubia huu kati yake na Serikali. Sisi tunaendelea na juhudi za kukamilisha ujenzi wa hospitali ya wilaya,” alisema Porini.

Akizungumza kwa njia ya simu akiwa jijini Dar es Salaam jana, Mchungaji Wambura alitetea kauli yake akisema ililenga kuwapo mchakato mzuri utakaotumika wakati wa kuvunja mkataba huo kati ya Serikali na kanisa hilo. “Hospitali ya Serikali ya wilaya ikikamilika inamaanisha baadhi ya watumishi wa umma waliopo watahamia huko hivyo kunahitajika njia muafaka na iliyo wazi kufikia hatua hiyo. Hiyo ndiyo ilikuwa hoja yangu tulipokutana na Rais Ikulu,” alisema.

Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Juma Hamsini alisema hakuna haja ya mvutano kuhusu suala hilo kwa sababu jambo hilo linalenga kuboresha huduma.

Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alisema dhamira ya Serikali ni kuona hospitali hiyo inaanza kazi Julai na kuzitaka pande hizo kuacha kulumbana badala yake waunganishe nguvu kufanikisha lengo hilo.



Chanzo: mwananchi.co.tz