Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya Askofu Shoo yaibua hoja ya mabadiliko ya sheria

14234 KAULI+PIC TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kauli ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo kwamba anasikitishwa na wanasiasa wanaohamahama vyama imeungwa mkono na viongozi wa dini na wanasiasa wakitaka kufanyika mabadiliko ya sheria.

Wakizungumza na mwandishi wetu jana, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mwalimu Nuhu Mruma wamesema vitendo hivyo vitadhibitiwa endapo kutakuwa na sheria imara.

Juzi, Dk Shoo alisema anasikitishwa na tabia ya wanasiasa wanaohama vyama jambo linaloligharimu Taifa pasipo tija yoyote.

“Sisi viongozi wa kidini tunafuatilia kwa umakini sana zoezi linaloendelea la kuhama vyama na gharama kubwa zinazotumika,” alisema Dk Shoo.

Askofu Nyaisonga alisema licha ya kuwa kuhama vyama ni suala la kidemokrasia, huenda Taifa linapoteza kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingetumika kwa shughuli za maendeleo.

“Unaona wanamichezo wanahama kutoka timu hii kwenda timu nyingine, kama kuna kitu kinamvutia mtu kuhamia sehemu nyingine ni haki yake ni “rule of the game” (sheria ya mchezo) na sioni haja ya kuwaza sana,” alisema.

Alisema endapo kiongozi amefanya uamuzi wa kuhama chama kutokana na kutoridhishwa na mambo fulani, watu hawapaswi kutunga maneno ya kumhisi vibaya au kukishutumu chama anachojiunga kwa kuwa hiyo ni haki ya kisiasa.

Mruma akizungumzia hilo, alisema kuhama chama ni haki ya msingi na haiwezi kuzuiwa.

Alisema suala la kuhama vyama limezikumba pande zote mbili kwa nyakati tofauti akitoa mfano wa kuhama waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye waliojiunga na Chadema wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na sasa upepo umegeuka.

“Ni suala la wakati tu na hali inaweza kubadilika wakati wowote, suala la msingi ni wananchi wenyewe katika maeneo ambayo uchaguzi unaporudiwa kufanya uamuzi ni yupi wamchague kulingana na sera zake, wao ndio wanasimamia demokrasia,” alisema.

Gharama uchaguzi mdogo

Askofu Nyaisonga alionyesha wasiwasi kuhusu gharama za uchaguzi mdogo akisema endapo fedha hizo zipo nje ya bajeti ya Serikali ni hasara kubwa kwa Taifa.

Alisema ipo haja kwa vyombo vya kisheria kuona namna sahihi ya kudhibiti matumizi hayo ikiwamo kupitia upya sheria zilizopo kwa masilahi mapana ya Taifa.

“Kama ni mwanya wa kisheria ndiyo unaotuingiza kwenye gharama hizi, basi kuna haja ya kufanya marekebisho ya kisheria. Bunge likae na lifanye marekebisho ya sheria ili kudhibiti hamahama ya viongozi,” alisema.

Mruma alisema hamahama hiyo ni suala la kidemokrasi ambayo ina gharama hivyo haiwezi kukwepeka.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliwahi kunukuliwa na Mwananchi akizungumzia gharama za uchaguzi mdogo akisema fedha za uchaguzi zipo.

“Pesa ya maji ipo, pesa ya kujenga barabara ipo, pesa ya kujenga reli ya kisasa ipo, pesa ya kununua ndege ipo, pesa ya kujenga shule ipo na pesa ya kuimarisha demokrasia ipo,” alisema.

Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema yaliyosemwa na viongozi wa dini yana umuhimu mkubwa.

“Tuweke sheria kama mtu ameacha ubunge asiruhusiwe kugombea kwa miaka hata mitano, hii itasaidia kudhibiti hawa viongozi ambao asubuhi wapo Chadema jioni wapo CCM,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz