Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) nchini Tanzania, Charles Kitima amesema mataifa mbalimbali yamefanikiwa kamaliza unyanyapaa kwa wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa kuhusisha suala hilo na sayansi ya dini.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 6, 2020 na Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), imeeleza kuwa Kitima ametoa kauli hiyo leo katika mkutano na wadau mbalimbali uliowahusisha viongozi wa dini.
Katika mkutano huo wamejadiliana namna watakavyotekeleza mpango mkakati wa kupunguza unyanyapaa.
Mpango huo unatekelezwa na Nacopha, wakishirikiana na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo uliwajengea uelewa viongozi mbalimbali wa dini, wadau na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya Ukimwi.
Akichangia katika mkutano huo, Kitima amesema sayansi na dini vinakwenda pamoja na kwamba viongozi hao wa kiroho wanaaminika kwa sababu wanaonekana walinzi wa uhai unaohusishwa na Mungu.
Pia Soma
- Kamati ya Bunge yalia na ongezeko la ukatili nchini
- Kamati ya Bunge yashauri kuundwa tume ya elimu Tanzania
- TRA yashauriwa kuendelea kuwekeza kwenye teknolojia za kisasa kukuza mapato
“Ndiyo maana kiongozi wa dini akisema nikikuweka mkono utapona, watu watakuja na wataacha kwenda kupima sambamba na kuacha kunywa dawa. Yote hii kwa sababu sayansi haijaweza kupenya na teknolojia,” amesema Kitima.
Amesema baadhi yao wamesoma kwenye elimu ya chini na uwezo wao mdogo huku akitolea mfano Taifa la Marekani ambalo raia wake ni wagumu kudanganywa, kwamba huwezi ukawaambia waombewe bila kupima kwanza.
Katibu mkuu Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaj Nuhu Mruma ameungana na Kitima na viongozi wengine waliochangia katika mkutano huo akisema afya ya waumini wa dini mbalimbali ni muhimu kama Serikali unavyojenga uchumi wa nchi.
Msimamizi wa mradi ya USAID , Gray Saga amesema changamoto iliyopo ni namna gani ya kushirikiana viongozi wa dini na mashirika akisema mwanzoni mchakato huu ulikuwepo lakini kipindi cha siku za hivi karibuni umekuwa ukisuasua.
Meneja wa uhamasishaji wa miradi ya jamii ya Nacopha, Mathew Kawogo aliwaeleza washiriki hali ya Ukimwi na unyanyapaa pamoja na malengo na vipaumbele kuhusisha taasisi na viongozi wa dini.