Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania – KKKT, Injinia Robert Kitundu, amesema Kanisa hilo linafanya kazi kwa karibu na Baraza la Kiislamu Tanzania – BAKWATA, licha ya kwamba wao kazi yao kubwa ni kueneza Injili Duniani kote.
Injinia Robert Kitundu, ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) katika Chuo cha Tumaini Makumira – Arusha leo tarehe 21 Agosti, 2023, ambayo yamehudhuriwa na Mgeni rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Baraza la Kiislamu Tanzania – BAKWATA Sheikh Jabir Nuhu Mruma alisema, “Sisi Baraza Kuu la Kiislamu Tanzania (Bakwata), tunashirikiana kwa karibu kabisa na madhehebu ya dini mbalimbali likiwamo hili la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Nichukue nafasi hii kufikisha salamu za Mufti wa Tanzania Sheikhe Abubakar Zuber Bin Ally.”
Amesema, “Mufti anawatakia kheri KKKT katika maadhimisho yao ya miaka 60 tangu kuzaliwa kwake. Sisi kwa pamoja tunawaombea mema viongozi wote wa serikali na kuitakia mema nchi yetu. Sisi viongozi wa dini tutaendelea kuwa mstari wa mbele kuishauri serikali na kushirikiana na serikali ili ifanye kazi nzuri ya kuwatumikia Watanzania.”