Dar es Salaam. Papa Francisko ameridhia ombi la Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam nchini Tanzania, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo la kutaka kung’atuka madarakani.
Ombi la Kardinali Pengo mwenye miaka 75 la kustaafu majukumu ya kuliongoza jimbo hilo yameridhiwa leo Alhamisi Agosti 15, 2019.
Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima imesema nafasi ya Kardinali Pengo imechukuliwa na Askofu Mkuu Mwandamizi Yuda Ruwa’ichi.
“Askofu Mkuu Yuda Ruwa’ichi OFM Cap ambaye mpaka sasa ni Askofu Mwandamizi ndiye anachukua rasmi majukumu ya kuliongoza Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,” amesema Padre Kitima.
Askofu Mkuu Yuda Ruwa’ichi ni kati ya wanafunzi wa Kardinali Pengo aliowahi kuwafundisha wakati alipokuwa akifanya kazi hiyo katika seminari ya Kipalapala iliyoko Jimbo Kuu la Tabora.
Kardinali Pengo alianza kufundisha seminari hiyo mwaka 1977 baada ya kurejea toka Roma alikokuwa ameenda kujiendeleza kwa masomo ya juu katika masuala ya maadili.
Pia Soma
- Rais wa Shelisheli atua Tanzania kushiriki mkutano wa SADC
- TRA yawalima barua wamiliki migodi ya Tanzanite
- Mifuko ya plastiki yabainika K’koo, Waziri Simbachawene atoa maagizo
- Meya Kinondoni aelezea jinsi Coco Beach itakavyoboreshwa