Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kardinali Pengo aacha alama 7 Dar

08ad80511c630b16c7b3a2faeccf3c4f Kardinali Pengo aacha alama 7 Dar

Mon, 21 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

ASKOFU Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amepongezwa kwa kuliachia jimbo hilo mambo mengi yakiwamo makubwa saba ya kiroho.

Mambo hayo ni kuanzisha Seminari Kuu ya Segerea, kuanzisha mfumo wa kuchangia jimbo wa Tegemeza Jimbo, shirika la Kipapa la Watoto, Wanawake Wakatoliki (Wawata), kulea Seminari ya Visiga na Utume wa Wanaume (Uwaka) na kulea masista wa Dada Wadogo, Mbagala.

Mengine ni kuanzisha mkakati wa kutafuta mapadri wa mashirika mengine kutumikia jimboni humo, kuratibu mshikamano wa kichungaji ulioondoa tofauti ya mapadre wa mashirika na wa jimbo na kuwezesha kupatikana kwa parokia 118 na sasa zipo 126.

Aliyekuwa Askofu Msaidizi wa jimbo hilo na ambaye sasa ni Askofu wa Jimbo la Mpanda, Eusebius Nzigilwa jana alisema Mwadhama Kardinali Pengo atakumbukwa kwa mengi mazuri na makubwa aliyoyafanya kwa kanisa hilo.

“Mwaka 1994 alianzisha utaratibu wa Tegemeza Jimbo na wakati huo zilipatikana Sh milioni 17, mwaka 2019 wakati anastaafu Tegemeza Jimbo zilipatikana Sh bilioni tatu. Fedha hizo zimesaidia kuendesha shughuli za kichungaji jimboni na kuondoa utegemezi na sasa majimbo yote 34 yana mpango huo,” alisema Askofu Nzigilwa.

Alisema mwaka 1996, Kardinali Pengo alianzisha Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu.

“Alianzisha utaratibu wa Wawata kulea seminari ya Visiga mwaka 1992 na sasa zaidi ya wanawake 14,000 hushiriki. Pia alianzisha Uwaka kulea masista wa Dada Wadogo mwaka 2008,” alisema.

Kwa mujibu wa Askofu Nzigilwa, Kardinali Pengo ndiye muasisi wa mkakati wa kutafuta mapadre wa mashirika mengine na wa kujitolea kufanya utume katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam na aliwezesha kupatikana parokia mpya 98 kutoka 20 alizozikuta wakati akipokea jimbo hilo.

“Sasa Jimbo Kuu la Dar es Salaam lina parokia 126 na linaongoza katika ukanda wa Amesea, likifuatiwa na Jimbo Kuu la Nairobi lenye parokia 114,” alisema Askofu Nzigilwa.

Alisema Pengo ametengeneza mshikamano wa kichungaji na umoja wa mapadre wa jimbo na mashirika ya kitawa kiasi cha wote kujisikia kuwa Dar es Salaam ni nyumbani kwao.

“Ulikuwa ukienda kuomba likizo, ukikosea ukasema unataka kwenda nyumbani kwenu kusalimia hupati likizo, lakini ukisema unakwenda kusalimia marafiki, hata kama ni Marekani utaenda sababu alisema unaenda nyumbani wapi? Dar es Salaam ndio nyumbani kwako,” alisema Askofu Nzigilwa.

Kwa upande wake, Kardinali Pengo aliwashukuru waliomuombea na kumtia moyo katika utume wake na kueleza kuwa, wakati alipoteuliwa kwenda Dar es Salaam akitoka Tunduru- Masasi, alitii tu kwa sababu ya kiongozi mkuu wa kanisa lakini aliogopa sana.

“Niliwaza mimi mtu kutoka Tunduru-Masasi nitawaeleza nini wataalamu wa mambo wa Dar es Salaam? Lakini niliwahi kuwaambia na ninasema tena nilitii tu kwa sababu ya kutii ila niliogopa sana. Lakini Wana- Dar es Salaam mlinitia moyo sana, mapadre, masista na waumini, mlishiriki utume wangu kwa sala zenu. Asanteni sana wana-Jimbo Kuu la Dar es Salaam,” alisema.

Kardinali Pengo ni daktari wa kanisa wa maadili na alipata shahada hiyo katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Alphonsiano, Roma.

Italia. Alizaliwa mwaka 1944 Sumbawanga mkoani Rukwa na alipata daraja takatifu la upadre akiwa na miaka 27 Juni 20 mwaka 1971.

Aliteuliwa kuwa Askofu mwaka 1983 na kuwekwa wakfu mwaka 1984 kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya (wakati huo) la Tunduru-Masasi.

Kardinali Pengo aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam mwaka 1990 na mwaka 1992 alianza rasmi kuliongoza jimbo hilo.

Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Kardinali na mpaka anastaafu amefanikiwa kuacha Parokia 118, asasi za huduma za kijamii kama elimu na afya. Kwa sasa jimbo hilo lipo chini ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi na lina Parokia 126.

Chanzo: www.habarileo.co.tz