Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanisa lataka watanzania kuendelea kumtegemea Mungu

6faea95450f233fa3e4034623255d487.jpeg Kanisa lataka watanzania kuendelea kumtegemea Mungu

Sat, 27 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KANISA Katoliki limeishauri serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kumtegemea Mungu na kuhakikisha nchi haiingii kwenye maovu yanayoendelea duniani kama ilivyokuwa msimamo wa Dk John Magufuli alipokuwa madarakani.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande, alitoa ushauri huo jana wakati akitoa mahubiri katika Misa Takatifu ya kumuombea Dk Magufuli iliyofanyika jana katika Uwanja wa Magufuli, mjini hapa.

Misa hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga na kuhudhuriwa na maaskofu zaidi ya 10 wa kanisa hilo, mapadri, watawa na maaskofu wengine wengi kutoka makanisa ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na makanisa ya Pentekoste na Sabato.

Askofu Mkuu Nkwande alisema Magufuli alimpenda Mungu na hakusita kuonesha hadharani imani yake hata kama angedhihakiwa na wanasayansi wenzake wasioamini kuwa Mungu yupo na kupinga uovu wowote waziwazi.

Alisema majitoleo yake kwa taifa na kazi kubwa aliyofanya itadumu milele katika mioyo ya Watanzania kama kumbukumbu ya majitoleo ya sadaka za ajabu.

Askofu Mkuu huyo alimuusia Rais Samia kuendelea kumtegemea Mungu na kuhakikisha ajenda ovu zinazoendelea duniani hasa Ulaya na Marekani za kuhamasisha utoaji mimba na ushoga haziingii nchini na nchi haifiki huko kama alivyokuwa akipinga Dk Magufuli.

Huku akinukuu maandiko matakatifu, Askofu Mkuu Nkwande alisema Mungu huruhusu mtu mwenye haki asiye na umri mkubwa kufariki ili asiharibiwe na uovu katika siku za baadaye kwa kuwa anakuwa ametenda mema mengi kwa muda mfupi kama ilivyokuwa kwa Magufuli.

“Rais Magufuli amekufa akiwapigania Watanzania watoke katika lindi la umaskini na unyonyaji wa rasilimali ndiyo maana wakati wote alisisitiza kuwa Tanzania si masikini,” alisema.

Aliwashukuru pia viongozi waliopita kabla ya Magufuli kuwa walikuwa wachungaji wema waliohakikisha wananchi wapo mikono salama.

Alisema Magufuli alikuwa Mchungaji mzuri ambaye hata wakati wa mlipuko wa janga kubwa la Covid-19, alidhihakiwa kwa kuonesha bila kificho kuwa anamtegemea Mungu na ni urithi pekee unaopaswa kuigwa na viongozi wa sasa.

“Leo wanasayansi ambao wameendelea kutokana na Mungu huyo huyo, wanataka kutuaminisha kuwa hakuna Mungu. Wanahamasisha utoaji mimba, ushoga. Ni upuuzi na vikao vyao kuhusu hayo ni mambo ya kipuuzi. Viongozi tusifike huko kwani walitoa mimba hizo nchi leo wanatafuta kuzaa hawawezi,” alikemea.

Askofu Mkuu aliwasihi Watanzania wafanye kazi kwa bidii huku wakimtanguliza Mungu na kuongeza kuwa anaamini siku moja Watanzania watakuwa watu wa kutoa msaada kwa wengine pamoja na kuwahimiza Watanzania waendelee kumuombea Magufuli apumzike kwa amani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz