Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanisa laeleza maneno ya mwisho ya Rais Magufuli

Fe71f9f91d0ef94014d5a33309e49a4a Kanisa laeleza maneno ya mwisho ya Rais Magufuli

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Walei Parokia ya St Peter Oysterbay Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Dk Adelhelm Meru ameeleza maneno ya mwisho ya kutia moyo waumini aliyotoa Rais John Magufuli aliposali kanisani hapo mwezi uliopita.

Dk Meru alisema hayo jana kwenye ibada ya kumwombea Magufuli iliyofanyika kanisani hapo kabla ya kwenda kuagwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

“Kwa kweli hatukujua kama Rais Magufuli alikuwa anatuaga, alilipenda kanisa, alipenda kusali na alimpenda sana Mungu,” alisema Dk Meru.

Mwenyekiti huyo alisema aliposali kanisani hapo kwa mara ya mwisho Februari 21, mwaka huu, walimwomba awasalimie waumini kwa kuwa ilikuwa muda mrefu umepita tangu asali nao ombi ambalo Dk Magufuli alilikubali.

Alisema ujumbe mkubwa aliowapatia ni kuwatia moyo waumini wenzake na Watanzania kwa ujumla kuwa wasiogope kwa kuwa Mungu yupo na anaweza kila kitu.

Kwa mujibu wa Katekista wa Parokia hiyo, Abel John, Rais Magufuli alikuwa baba mwenye maono kwa sababu kifo chake kimewafanya wakumbuke maneno aliyowaambia mara ya mwisho aliposali kanisani.

“Rais Magufuli alitutia moyo Watanzania kwamba kweli ugonjwa wa Covid-19 upo lakini tumtegemee Mungu kwa kuwa kifo kipo na kila mmoja atakufa na hata yeye pia atakufa, hatukujua kama alikuwa anatuambia fumbo la kifo chake,” alisema Katekista John.

Akimwelezea Dk Magufuli na ushiriki wake kanisani hapo, Dk Meru alisema “kabla hajawa Rais alikuwa anapenda sana kukaa pale nje ya mlango wakati wa Ibada ya Misa Takatifu na mara chache alikuwa anakaa nyuma ya kanisa.”

“Alipokuwa Rais, siku moja nikamtania Mheshimiwa Rais tukuwekee kiti chako pale nje, akasema napenda lakini kwa sasa haitawezekana itifaki hairuhusu,” alisema Dk Meru na kuonesha kiti alichokuwa akikaa kanisani hapo baada ya kuwa rais ambacho jana kilikaliwa na mkewe Janet Magufuli.

Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu kwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na atazikwa Machi 26, mwaka huu nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

Chanzo: www.habarileo.co.tz