Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanisa kubwa Katoliki mbadala wa St. Joseph kujengwa Dar

Kanisa Kubwa Katoliki Mbadala Wa St. Joseph Kujengwa Dar Kanisa kubwa Katoliki mbadala wa St. Joseph kujengwa Dar

Sun, 17 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kanisa katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam linatarajia kujenga kanisa kuu mbadala litakaloendana na ongezeko kubwa la idadi ya Wakristo katika jimbo hilo sambamba na kutumika kwa shughuli nyingine za kanisa.

Kanisa hilo litakalojulikana kama Kanisa la Bikira Maria Mama wa Mungu, litajengwa kwa nguvu za waumini wenyewe na litakuwa na ukubwa mita za mraba 13,000 na uwezo wa kubeba watu 9,816 na pia litakuwa na handaki.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi amesema sababu kubwa ya kujengwa kwa kanisa hilo ni kutokana na ongezeko la watu katika jimbo hilo na kanisa la sasa ni dogo.

“Kanisa kuu la Mtakatifu Joseph linatimiza miaka 120 mwaka huu, lilipojengwa, Dar es Salaam ilikuwa na wakristo 248, kwa hiyo likajengwa kanisa la watu 500. Leo Dar es Salaam ina wakristo takribani milioni 2, je linatosha? amehoji Askofu Ruwa’ichi.

Amesema kutokana na udogo wa kanisa hilo, ndiyo unawafanya waende ukumbi wa Msimbazi kwa shughuli mbalimbali za kikanisa.

“Naomba niwatie moyo kwamba ninalotamka halileti vurugu wala mabadiliko kwa kanisa la Mtakatifu Joseph. Litaendelea na heshima yake, historia yake, litaendelea kuwa kanisa kuu la jimbo kuu la Dar es Salaam.

“Lakini kwa kuzingatia hali halisi, tumeamua kujenga kanisa kuu mbadala. Tumenunua eneo kule Gezaulole kwa ajili ya maadhimisho ya kijimbo, sasa hatupendi kwenda kule tuwe tunazagazagaa, kwa hiyo tumeamua kujenga kanisa kuu mbadala kule Gezaulole,” amesema.

Amesisitiza kwamba lile kanisa kuu la Mtakatifu Joseph lilijengewa na watawa wa Benedictine kutoka Ujerumani na kwa hela zilizotoka kwao. Ameongeza kwamba kazi iliyo mbele yao wataifanya wao wenyewe.

Askofu Ruwa’ichi amebainisha kwamba usanifu wa majengo hayo umekamilika na muda wowote wataanza ujenzi huku ushiriki mkubwa wa waumini unahitajika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live