Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanisa Katoliki latangaza Machi 17 Siku ya Magufuli

Magufuli Kaburi Ghs Kanisa Katoliki latangaza Machi 17 siku ya Magufuli

Sat, 18 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, limetangaza rasmi kuadhimisha kila mwaka, Machi 17 ambayo ni  siku aliyofariki dunia aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli.

Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 wakati akipatiwa matibabu ya moyo katika Hospitali ya Emilio Mzena, Dar es Salaam, hali ambayo ilitikisa nchi na kuibua simanzi kwa wananchi.

Hali hiyo ilitokana na ukweli kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwa taifa kushuhudia kifo cha Rais akiwa madarakani tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Ikiwa imetimia miaka miwili tangu kifo cha Dk. Magufuli, jana Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, lilitangaza rasmi kuitambua na kuiadhimisha kila mwaka Machi 17 ikiwa ni kumwombea toba kwa Mwenyezi Mungu na kutambua mchango wake mkubwa kwa kanisa na jamii kwa ujumla.

Askofu wa Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, alisema Kanisa Katoliki jimbo hilo limeipitisha rasmi siku hiyo ambayo itaanza kuadhimishwa kila mwaka na kwamba waumini wa kikatoliki wanapaswa kuitambua kwa kumwombea heri Hayati Magufuli.

Askofu Niwemugizi alikuwa kwenye ibada ya misa takatifu ya kumwombea toba kwa Mungu, iliyofanyika jana kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mlimani Rubambangwe, Chato, takribani mita 100 kutoka nyumbani kwao Hayati Magufuli.

"Siku hii sasa ni rasmi kuiadhimisha kila mwaka. Mimi nitakuja hapa kila Machi 17 hata kama nitakuta waamini wawili. Hata kama nikiwa pekee yangu nitasali maana popote alipo askofu na kanisa liko hapo," alisema.

Askofu Niwemugizi alitumia fursa hiyo kumwombea Hayati Magufuli msamaha kwa yeyote aliyemkwaza enzi za uhai wake na kwamba huenda aliwakosea baadhi ya watu kwa kuwa naye alikuwa binadamu kama wengine.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Inocent Bashungwa, mbali na kushukuru kwa utumishi mwema wa Hayati Magufuli, amesema serikali itaendelea kuenzi mambo yote mazuri aliyotamani watanzania kuyapata.

"Ni miaka miwili imepita tangu tumempoteza aliyekuwa Rais wetu wa awamu ya tano, Hayati Dk. Magufuli. Ni ukweli usiopingika kuwa atakumbukwa sana na serikali na jamii kutokana na maono na alama zake za kimaendeleo alizozifanya kwa Watanzania," alisema Bashungwa.

Mjane wa kiongozi huyo, Mama Janeth Magufuli, aliwashukuru Watanzania kwa kuendelea kumwombea mema Hayati Magufuli sambamba na kulishukuru Kanisa Katoliki kwa kuendelea kumuenzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live