Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanisa Katoliki Dar lakusanya Sh2.9 bilioni misa ya mavuno

28701 Pic+katoliki TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, limekusanya zaidi ya Sh2.9 bilioni katika misa ya mavuno iliyofanyika Msimbazi Centre, jijini Dar es Salaam jana.

Fedha hizo zimekusanywa kupitia Dekania ambazo ni muungano wa parokia kadhaa zilizopo eneo moja katika jimbo hilo ikiwa imeongezeka kutoka Sh2.6 bilioni zilizokusnywa mwaka jana.

Katika makusanyo hayo, Dekonia ya Kigamboni ilitoa Sh246.3 milioni, Kilimahewa (Sh36.3 milioni) Mt Joseph (Sh484.5 milioni), Mbezi (Sh257.8 milioni), Mt Gasper (Sh404.7 milioni), Mt Petro (Sh536.6 milioni), Ubungo (Sh378.8 milioni), Ukonga (Sh250.7 milioni), Segerea (Sh107.5 milioni) na Kibaha (Sh145.5 milioni).

Akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Walei Jimbo, Kuu la Dar es Salaam mara baada ya misa ya mavuno, Askofu Msaidizi wa jimbo hilo, Eusebius Nzigilwa alisema matarajio ilikuwa ni kukusanya Sh2.8 bilioni na kwamba anamshukuru Mungu kwa sababu makusanyo yaliyopatikana yamevuka lengo.

Katika ibada hiyo, sadaka ya Sh8.6 milioni ilikusanywa huku malengo yakiwa ni Sh6 milioni.

Akihubiri katika misa hiyo iliyohudhuriwa na waumini zaidi ya 6,000, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kadinali Pengo alisema sadaka hiyo ni desturi ya kanisa hilo lengo likiwa kumwambia Mungu ahsante kwa matendo makuu aliyowatendea.

“Kwa nini tunatoa sadaka hii? Tunataka kukiri kwa Mungu na wanadamu kwamba kila walichonacho kinatoka kwa Mungu na wao wenyewe,” alisema Kadinali Pengo.

Alisema katika historia wanadamu huwa hawatambui ukweli kwamba kila kitu walichonacho ni mali ya Mungu na hivyo kushindwa kurudisha shukrani kwa mambo makuu anayowatendea.

Alisema watu wakipuuzia uwepo wa Mungu na kujitukuza matokeo yake huwa ni maafa.

Pia, aliipongeza Serikali kwa kutokubali masharti ya ndoa ya jinsia moja ili ipatiwe misaada akisema hata kama itatokea njaa, kanisa hilo halipo tayari kukubali jambo hilo.

“Daima naishukuru Serikali katika msimamo huo, tukifa njaa na tufe tu kwani hatulimi mahindi? Hata iwaje atabaki Yesu wetu, wanaotishia hatutaleta fedha za ‘dance’ nani anataka? Tutoke na neno moja tu kama kufa na njaa tufe pamoja na Mungu,” alisema na kuongeza kuwa kumpuuza Mungu ni sawa na kujipuuza mtu binafsi.

Kuhusu sadaka alisema, “Tunaomba Mungu apokee jambo hili akijua linatoka ndani ya mioyo yetu na kwamba tunachotaka kusema ni ahsante.”

Ibada hiyo pia ilitumika kuwaombea viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, watu wanaopitia katika mateso mbalimbali wakiwamo magonjwa, yatima na wajane.

Baadhi ya waumini waliozungumza na mwandishi wetu walisema moja ya mipango ya kanisa lao ni kuwashirikisha kwa “majitoleo ya tegemeza jimbo” kupitia parokia zao.

“Mpango huu tunaupenda na tunaufurahia kwa sababu baraka za maombi haya yote huwa zinarudi kwenye familia zetu,” alisema Eukania Sepali kutoka Segerea.

Alisema wanaamini kuwa maendeleo ya jimbo lao ikiwamo uoaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama afya na elimu yatakuwa kwa kasi kama wataendelea kushiriki katika utoaji huo.



Chanzo: mwananchi.co.tz