Dodoma. Kaimu katibu mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dodoma, Twaha Mwaya amefariki dunia jana Jumapili Januari 19, 2020 katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo alikokuwa akitibiwa baada ya hali yake kudhoofu.
Mwili wa Mwaya utazikwa leo Jumatatu Januari 20, 2020 katika makaburi ya Kwamwatano yaliyoko Maili mbili jijini Dodoma.
Sheikh wa mkoa wa Dodoma, Alhaji Mustafa Rajab Shabani amesema mtendaji huyo ameondoka na kwao wanaona mti mkubwa uliodondoka na kuacha kishindo lakini akabainisha yote ni mapenzi ya Mungu.
“Innaa lillahi wainnaa ilaihi raajiuun. sisi ni wa allah na kwake allah tutarejea. nachukua fursa hii adhwiim kwa moyo ulojaa majonzi na wenye kuamini qadari za allah,” alisema Shekh Rajabu.
Alhaji Rajabu ametaja sababu za kifo cha Mwaya kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu na shinikizo la damu ambalo lilisababisha mauti kumkuta.
Katika uhai wake, Mwaya alikuwa Katibu wa Bakwata wilaya ya Dodoma na alikuwa na ushawishi na muumini wa amani kwani katika vikao alivyohudhuria alizungumzia amani na upendo wakati wote.
Pia Soma
- Kiongozi Kundi la IS mwenye uzito wa kilo 250 akamatwa Iraq
- Serikali ya Tanzania kujenga Hospitali ya Kanda Chato
- Kilimo cha maparachichi chamtajirisha aliyekuwa na ajira ya kufanya usafi
Kiongozi huyo amewataka waumini na wakazi wa Dodoma kutulia katika kipindi hiki wakati wakitafuta kwa sehemu kubwa alifanya kazi kwa kutumikia nafasi mbili kwa wakati mmoja.