Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KKKT wanavyomkumbuka Lowassa

Lowassa Edward Wasifu Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa.

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

“Nitamkumbuka Lowassa kwa mambo mengi, lakini kitendo cha kurejesha wa kwanza kadi ya mchango wa ujenzi wa kanisa Sh1.2 milioni mwaka 1992 ni jambo ambalo siwezi kulisahau.”

Hiyo ni kauli ya mchungaji Mwanga Ole Ndoponoi ambaye licha ya kuwa kiongozi wa kiroho, wamefahamiana na Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa tangu miaka 1960 wakisoma shule moja ya Monduli Middle School.

Alichokieleza Ndoponoi kinaungwa mkono na mchungaji wa Usharika wa Malambo, Ndelilio Ndekirwa aliyesema: “kwa kweli kama alivyokuwa anatoa mawazo serikalini na kuyasimamia na kanisani ilikuwa hivyo hivyo. Pale mnapoona haiwezekani, yeye analisimamia hadi linatekelezeka.”

Viongozi hao wa dini walieleza hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwa Lowassa katika kijiji cha Ngarash, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha ambapo mwili wake ulizikwa Jumamosi iliyopita.

Lowassa (70), alifariki dunia Februari 10, mwaka huu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Ndoponoi alisema mwaka 1992 aliunda kamati ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli na kuandaa kadi zaidi ya 100 ambazo walizigawa kwa wanaushirika.

“Kanisa tunaloabudu sasa hapa Monduli, kadi ya kwanza ya mchango, Lowassa alileta Sh1.2 milioni, miaka hiyo ilikuwa hela nyingi.

“Si kwamba ni tajiri, hapana bali alikuwa na moyo wa kujitolea. Kwa kweli alijitoa kikamilifu kwa Mungu wake na mimi hilo ninalikumbuka,” alisema Ndoponoi ambaye kwa sasa ni Mhubiri wa Injili asiye na mipaka

Alisema fedha hiyo alimpa shemeji yake, mama Alex Lowassa (mke wa mdogo wake) kule Dar es Salaam akamwambia aipeleke kwa mchungaji Ndoponoi Mwanga.

Mchungaji huyo alisema Lowassa akiwa Dar es Salaam alikuwa akisali Usharika wa Azania Front na alipokuwa Monduli alisali katika usharika huo. “Nilikuwa mchungaji wake na akija likizo ama mapumziko anakuja kusali Monduli na tulikuwa tunampa nafasi ya kusalimia,” alisema.

Alisema mara nyingi alipopewa nafasi ya kuzungumza alipenda kuhimiza masuala ya maendeleo, watu kufanya kazi na kuhimiza kupeleka watoto shule. Alisema pia Lowassa alishiriki ujenzi wa hosteli kama kitega uchumi na kueleza kuwa kwa matendo yake hakuna wana Ushirika wa Monduli anayemdai.

Kusimamia wazo Mchungaji wa Usharika wa Malambo, Ndelilio Ndekirwa alisema kiongozi huyo ameshiriki kwa kiwango kikubwa katika ujenzi wa kanisa hilo.

“Lowassa alitoa wazo la kuwa na hosteli na hakuishia kutoa wazo tu, bali akasimamia kuhakikisha wazo hilo linatimia. Katika kutimiza hilo, aliendesha harambee karibu 10. Kwa kweli alikuwa msaada katika kanisa na amefanya mambo makubwa,” alisema.

Pi alisema mwaka mmoja alitoa shukurani kwa kumaliza mwaka salama kwa kujenga peveti na ukuta wa kuzunguka kanisa.

Mchungaji huyo alisema wakati kanisa hilo linajengwa, yeye (Ndekirwa) alikuwa mwinjilisti na pale walipoona haiwezekani, Lowassa alisimamia hadi linatekelezeka.

Katika kuhakikisha kanisa linakuwa na kitega uchumi, Lowassa alihimiza kanisa liwe na mradi wa hosteli na akasimamia zikajengwa.

Alieleza kuwa siku ya maziko, watu walijaa kwenye hoteli hiyo, kwani ni sehemu yenye utulivu. “Mradi umeanza na matunda yanaonekana na kwa kweli ameacha alama inayoishi,” alisema.

Mchungaji Joel Ole Nangole wa Ushirika wa Monduli alisema Lowassa alikuwa mtu wa ibada, hawezi kukosa ibada kama atakuwa hapa Monduli, alisaidia ujenzi wa kanisa wanalolitumia sasa kwa asilimia 73.

Mchungaji Nangole alisema pia Lowassa alimtuma shemeji yake aliyeweka madirisha pamoja na kupeleka piano na vipaza sauti.

“Pia ameshiriki kujenga hosteli yenye vyumba zaidi ya 20 vya kulala,” alisema mchungaji huyo. Hata ushirika ulipozidiwa na madeni ya JKT waliyojenga hiyo hosteli, alisema Lowassa alifanya harambee na madeni yakaisha,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema kiongozi huyo alikuwa mtu wa kusamehe, wale wote waliomdhihaki aliwasamehe, alikuwa mvumilivu na mtu mwenye imani na hakutikisika.

“Ametukanwa, lakini amenyamaza na kama alirudisha, ilikuwa kwa heshima. Yeye alisema wakati wa uchaguzi tutachukua nchi mapema, lakini alitukanwa na hakujibu kwa hasira.

“Lowassa hakiwa na woga, unajua Wamasai si woga, hatujisifii lakini tukisema hapana ni hapana na ndio ni ndio,” alisema.

Michezo, Brass band Mchungaji Ndoponoi alisema walifahamiana na Lowassa katika Shule ya Kati Monduli ambapo kiongozi huyo alikuwa darasa ;a mbele naye la nyuma.

“Kiumri tuko sawa, sema wazazi wangu hawakupenda shule na wazazi wake walipenda asome na ndio sababu akawa mbele yangu,” alisema.

Alisema wakiwa shule, walishirikiana kwenye masuala ya michezo, skauti na brass band.

“Kwenye brass band, yeye alikuwa kiongozi, anashika ile fimbo, alikuwa anajua kuichezesha na mimi nilikuwa napiga filimbi. Kwa kweli alikuwa hodari wenye Brass band.”

Mbali na brass Band, alisema Lowassa alipenda mchezo wa basket ball alioumudu vizuri pamoja na skauti.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live