Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KKKT ngoma nzito, wazidi kuvurugana

Kkkt Pic Data KKKT ngoma nzito, wazidi kuvurugana

Mon, 13 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Amani Mwenigoha amesema askofu wa dayosisi yoyote akivuliwa uchungaji, anapoteza sifa ya kuwa askofu na kumtaka Askofu Stephen Munga kuheshimu hilo.

Ni kwa msingi huo, Mwenigoha aliyewahi pia kuwa Mkuu wa wilaya ya Bukombe, alisema si sahihi kwa Dk Munga kujishika na Baraza la Maaskofu la KKKT kwa kuwa sio mamlaka yake, bali mamlaka yake yako ndani ya dayosisi.

Kauli ya Mwenigoha inatokana na barua ya Askofu Dk Munga kuwaandikia barua maaskofu wa KKKT ya Novemba 1, 2021 akipinga uamuzi wa halmashauri ya Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kumvua uchungaji Oktoba 30.

Katika barua hiyo aliwaeleza maaskofu juu ya kupokea barua ya askofu wa dayosisi hiyo kuwa yeye (Dk Msafiri Mbilu) na halmashauri yake wamemvua uchungaji ili apoteze sifa ya kuwa askofu mstaafu.

“Yapo mapokeo jinsi uaskofu unavyopatikana, unavyotunzwa na unavyoweza kufika ukomo. Kuna mambo ya msingi ya kibiblia na ya kikatiba yanayoweza kufikisha ukomo wa askofu. Barua ya askofu haijazingatia hilo,” alisema.

Jambo lingine alisema mambo ya maaskofu humalizwa na baraza la maaskofu la kanisa husika. Sijawahi kuarifiwa kwamba jambo linalonihusu mimi limepelekwa kwenye baraza la maaskofu na kujadiliwa na kuwekewa makubaliano,” alieleza.

“Hivi sasa mimi ni askofu mstaafu na ipo misingi ya namna baraza la maaskofu linavyoshughulikia maaskofu wastaafu. Jambo la kumweka au kumuondoa askofu halifanywi kwa utashi wa mtu bali linalindwa na mapokeo ya kanisa.”

“Hoja ya tuhuma alizoweka Askofu Mbilu katika barua yake hazina ukweli. Nipo tayari kutokea kwenye baraza la maaskofu ili kulithibitisha hilo,”alieleza Askofu Munga kwa maaskofu wa KKKT na kusisitiza yeye bado ni askofu.

“Msimamo wangu ni huu; kutii agizo dhalimu linalojengeka juu ya mambo ya uongo, hila na chuki ni dhambi mbele za Mungu. Hivyo nitaendelea kuwa askofu aliyestaafu na nitaendelea kutokea kiaskofu ninapoona haja ya kufanya hivyo”

Hata hivyo, akitoa maoni yake juu ya kauli ya Mwenigoha, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya KKKT, Dk Benson Bagonza alisema tafsiri ya Mwenigoha si sahihi na kwamba, uaskofu unaweza kuondolewa tu kwa kukiuka imani.

“Lakini mimi ningesema ukishaitwa askofu ni universal (ni wa mahali kote) ndio maana dayosisi ikimchagua askofu haimweki wakfu yenyewe na sharti wawepo maaskofu wengine ili uaskofu uwe halali,”alisema na kuongeza:

“Ni lazima wawepo maaskofu wasiopungua watatu na kuendelea huko mbele vinginevyo huo sio uaskofu, na ndio maana ili kuuondoa pia inabidi dayosisi ishauriane na maaskofu wengine.’’

‘‘Lakini pia, jambo jingine ni kwamba, uaskofu tangu kanisa la kwanza baada ya Yesu kuondoka unaweza kuondolewa tu kwa sababu za kimafundisho. Kukiuka imani si masuala haya mengine ya fedha na nini na nini.’’

Hata hivyo, wakati mgogoro ndani ya Dayosisi hiyo uliofika kilele 2020 ukiendelea, Askofu wa dayosisi hiyo, Dk Msafiri Mbilu amegoma kuzungumza lolote akisema masuala hayo ni ya vikao na kwamba asingependa kuyaingiza kwenye magazeti.

Mwenigoha amshukia Askofu Munga

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenigoha alisema askofu akivuliwa uchungaji moja kwa moja anapoteza uaskofu na kutolea mfano wa waziri akiondolewa ubunge moja kwa moja, anapoteza sifa ya kuendelea kuwa waziri.

“Katiba ya KKKT haiiti wala haiajiri wachungaji wala maaskofu. Maaskofu wanaitwa kuajiriwa kwanza kama wachungaji. Kwa hiyo dayosisi yako ikikuondoa kwenye uchungaji automatically (moja kwa moja) umeondolewa na uaskofu,”alisema.

“Maana kwenye kanisa hili hatuna maaskofu ambao ni walei. Ni kama ubunge na uwaziri, mbunge akiondolewa ubunge na uwaziri unaondoka au mbunge akifukuzwa uanachama, automatically ubunge unaondoka.”

“Sasa ndivyo ilivyo kule (kwenye dayosisi), mchungaji wa kanisa la Kilutheri akiondolewa uchungaji na uaskofu unaishia hapo. Sasa hana sababu za kisheria wala za kikatiba za kudai kuwa yeye anaendelea kuwa askofu mstaafu”

“Kwa sababu huwezi kuwa askofu mstaafu bila kuwa mchungaji na ule uchungaji uko kwenye jurisdiction (mamlaka) ya dayosisi. KKKT haihusiki kabisa na ku recruit (kuajiri) wachungaji na kuwasomesha na kuwabariki. Haihusiki,” alisisitiza na kumshauri Dk Munga kutofanya fujo katika dayosisi.

Alitoa wito kwa Serikali kufuatilia mgogoro huo kwa karibu sana na inapobidi kuudhibiti kwani unaweza kusababisha vurugu kubwa ndani ya Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mkoa wa Tanga.

Wachungaji waomba tume huru

Katika hatua nyingine, uchunguzi wa gazeti hili umebaini Novemba 25,2021, wachungaji watatu Dk Eberhardt Ngugi, Dk Anneth Munga na James Mwinuka, walimwandikia barua Askofu Mbilu, kumsihi aunde tume huru ya uchunguzi.

Kwa maelezo yao, baadhi ya wajumbe wa tume hiyo ya kanisa ndio haohao waliokuwa sehemu ya kiini cha mgogoro wa uchaguzi wa askofu uliofanyika mwaka jana na wanaona tayari imewahukumu hata kabla ya kuwasikiliza.

Katika barua yao ya pamoja, wachungaji hao watatu wamemwandikia barua Askofu Mbilu kama mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Dayosisi, wakikiri kupokea barua za kutakiwa kufika mbele ya tume iliyoundwa kwa ajili ya kuwahoji.

“Baba Askofu, kwa njia ya barua hii, tunapenda ifahamike kwamba hatuko kinyume na wito wa kuhojiwa na kamati, lakini hatuna imani na tume maalum ya halmashauri kuu iliyoundwa,”walisema wachungaji hao katika barua.

Wakieleza sababu, walisema “Ni kwa kuwa miongoni mwao (wajumbe) wamo wanaharakati ambao walihusika katika maumivu na mateso yetu. Hivyo tunakosa imani kuwa tume hii itatusikiliza na kutoa maamuzi ya haki dhidi yetu.”

“Tunaomba iundwe tume huru ya kutuhoji ambayo haitaegemea upande wowote kuliko ilivyo kwa sasa kwa tume hii ambayo tunaona tayari imeshatuhukumu hata kabla ya kutusikiliza,” walisisitiza wachungaji hao katika barua yao.

“Ukiangalia haya maswali (wanayotakiwa kujibu) unapata shida kuelewa nia ya Tume maalum. Mchungaji Dk Anneth Munga alikuwa kiongozi wa SEKUCo/SEKOMU tangu mwaka 2007 hadi 2017,”walisema na kuongeza;-

“Ukaguzi wa fedha wa miaka hiyo yote ulishafanyika na kuthibitishwa na Bodi ya Sekuco na Baraza la Sekomu. Ikiwa waliohusika na ukaguzi wa 2019/2020 walikuwa na maswali kwake kwa nini hakuitwa ili kuhojiwa na wakaguzi hao?”

“Ama kutumiwa hoja (queries) za wakaguzi hao kama zilikuwepo? Isitoshe mchungaji Dk A. Munga ameulizwa maswali juu ya msitu wa Chatillon, eneo ambalo halijawahi kuwa chini ya Sekomu,” wameeleza katika barua hiyo.

“Mchungaji Dk Eberhardt Ngugi na mchungaji James Mwinuka wameulizwa maswali wanayotakiwa kujibu kama wanasheria wa dayosisi, lakini hakuna yeyote miongoni mwao aliyewahi kutumika kama mwanasheria wa dayosisi.”

Sekuco na Sekomu ni taasisi zilizo chini ya Kanisa la KKKT.

Wachungaji hao wamedai kuwa kitendo cha tume maalum kuondoa itifaki zao za kiutumishi kwenye barua, kinaendelea kuwapa maswali mengi kwani baadala ya barua kuanza na mchungaji ziliandikwa ndugu au Dk badala ya mchungaji.

“Hiyo ni dalili ya wazi kwamba uamuzi kutuvua uchungaji umeshafanyika na kwa hiyo mchakato unaofanywa kupitia tume maalum ni kuweka ushahidi kwamba tuliwahi kuhojiwa,”wameeleza wachungaji hao na kuongeza:

“Kwa sababu tulizozitaja hapo juu ambazo tunaamini kabisa kwamba ni kwa maslahi mapana ya Kanisa letu, dayosisi yetu na utumishi wetu, hatutakuwa tayari kujibu wala kwenda mbele ya tume maalumu hii.”

Wachungaji hao pia wameeleza namna mchakato wa uchaguzi mkuu wa askofu wa mwaka 2020 ulivyokumbwa na changamoto mbalimbali, kutokana na kuingiliwa na watu waliojiita wanaharakati kutoka ndani na nje ya Dayosisi.

“Kutokana na yote yaliyotokea, tulitarajia kwamba wewe kiongozi mkuu wa kanisa ungetuganga mioyo na kuleta upatanisho katika dayosisi yetu kama ulivyoahidi kwenye hotuba yako ya kwanza baada kuchaguliwa wako.”

“Bahati mbaya, hali tunayoiona sasa ni tofauti kabisa. Baba Askofu, inaonekana dhahiri kwa macho na kusikika kwa masikio kwamba juhudi zako za kuganga mioyo, kuleta upatanisho zimeingiliwa na wanaharakati kwa ajli ya maslahi yao,’’ walisema ndani ya barua yao.

Aidha, wachungaji hao wametahadharisha kuwa huko dayosisi inakoelekea hawaoni nuru ya uponyaji wa mioyo iliyojeruhiwa, upatanisho, wala nguvu ya umoja na badala yake wanaona mateso ya kanisa na migawanyiko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live