Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi watendaji serikalini wanavyoweza kuepuka ‘kibano’ cha wanasiasa

9345 Pic+watendaji TZW

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki hii vumbi la waraka wa Pasaka uliotolewa na maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeendelea kutimka.

Ni miezi mitatu sasa tangu waraka huo utolewe lakini mjadala wake umeendelea kutikisa nchini.

Safari hii Mkurugenzi wa Idara ya sheria na usajili wa vyama vya kidini na vya kijamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ametimua vumbi jipya baada ya kulitaka kanisa hilo kufuta waraka huo.

Waraka wenyewe

Waraka uliopewa jina “Taifa Letu Amani Yetu” uliosainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo, mbali ya kuzungumzia masuala ya kiroho, unataja changamoto mbalimbali.

Changamoto hizo ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Pamoja na mambo mengine, waraka huo umetaka nchi kuwa na siasa safi, uhuru wa mawazo, Taifa liongozwe Katiba si Ilani ya vyama, kukemea utekaji, utesaji, watu kupotea na mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi na kwa upande wa uchumi ukigusia ukusanyaji wa kodi, viwanda kuendana na uwekezaji wa sekta ya kilimo.

Chanzo cha tatizo

Kwa maoni ya msajili hiyo, chombo kilichotoa waraka huo hakitambuliwi kisheria na ulizungumzia masuala yaliyo nje ya malengo ya kanisa hilo.

Huku KKKT ikijibu barua ya msajili huyo na suala hilo likiibua mjadala mzito nchini, Waziri Dk Mwigulu Nchemba anaibuka na kusema barua hiyo ni batili kwa kuwa si maelekezo ya Serikali.

Dk Nchemba hakuishia hapo, pia anatangaza kumsimamisha kazi Msajili huyo, Merlin Komba na akisema iwapo itabainika kuwa ndiye atabainika ndiye aliandika barua hiyo, atachukuliwa hatua za kisheria lakini pia kama kuna mtu aliandika kwa lengo la kuibua taharuki, atatafutwa na kushtakiwa kwa makosa ya mtandao.

Hatua ya Dk Nchemba ambayo ilikusudiwa kufafanua na kumaliza suala hilo imeibua maswali mengine yasiyo na majibu, kubwa likiwa ni nafasi ya watendaji wa serikali katika kuamua “kipi ni uamuzi wa Serikali na kipi siyo, na nani anapaswa kuamua hivyo.”

Pia katika maswali hayo, wachambuzi pamoja na kuhoji, wanaeleza ni hatua gani mtendaji wa serikali anaweza kuchukua iwapo kuna maagizo ya kisiasa anayodhani si sahihi kulingana na maadili na wajibu wake.

Wachambuzi wadadavua

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Ruth Mollel anasema mtendaji wa ngazi yoyote anapopewa maagizo ya kufanya na kiongozi wake akaona kwamba yanaweza kuwa na madhara anapaswa kumjulisha kiongozi aliyeyatoa.

“Lazima mfanyakazi uwe ‘smart’ endapo kiongozi atakulazimisha kufanya jambo hilo, jukumu lako ni kumuomba akuandikie kwa maandishi, kisha na wewe umjibu kwa maandishi na kumweleza kwa nini unaona jambo hilo likitekelezwa linaweza kuleta madhara,” anasisitiza Mollel.

Mollel ambaye amewahi kuwa katibu mkuu wa wizara mbalimbali ikiwamo ya utumishi katika Serikali ya awamu ya nne, anasema endapo kiongozi huyo ataendelea kusisitiza jambo hilo kufanyika, mtumishi ana njia mbili za kufanya.

“Kwanza, ni kutekeleza kile alichoamuliwa kufanya, lakini ahakikishe anatunza kumbukumbu ya mazungumzo baina yake na bosi. Hata kama baadaye zikinyofolewa kwenye mafaili, mtendaji naye awe nazo pindi utakapohitajika ushahidi,” anasisitiza Mollel.

Jambo la pili, ni kuacha kabisa kutekeleza jambo hilo, kisha kuachia ngazi; “hii itasaidia kuonyesha msimamo wako.”

Mollel ambaye kwa sasa ni naibu waziri kivuli wa kambi ya upinzani Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora anasema vyovyote iwavyo mtumishi mwenyewe ndio mwenye wajibu wa kuhakikisha anatunza kumbukumbu zake ili zimsaidie baadaye endapo atafanyiwa unyanyasaji.

Katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza yeye anazungumzia moja kwa moja msajili huyo kuwa alipaswa kutumia busara licha ya kwamba analindwa na sheria, taratibu na kanuni zilizopo chini yake.

“Msajili naye ni binadamu asisahau kama anaishi katika jamii. Swali ni je, alishawahi kuwakumbusha (maaskofu) wajibu wao wa kuitisha mikutano au kujisajili na alifanya hivyo mara ngapi?”

“Sheria inasaidia kuongeza ulaini wa mambo siyo kuongeza migogoro na misuguano katika jamii, alipaswa ajue hilo na kutumia busara badala ya kusimamia sheria au kanuni tu,” anasisitiza Rweikiza ambaye ni mbunge wa Bukoba vijijini (CCM).

Rweikiza ambaye ni mwanasheria, anatoa mfano wa majaji wanapotoa hukumu wakati mwingine wanalazimika kutumia busara zaidi licha ya ukweli kwamba sheria na kanuni zipo.

“Jaji anapotoa hukumu, wakati mwingine pamoja na ushahidi kujidhihirisha wazi, anasema ‘kwa maoni yake’ na bado hukumu hiyo inakuwa halali,” alisema.

Rweikiza anasema sheria haipaswi kuongeza migogoro au misuguano katika jamii badala yake inapaswa kuhakikisha jamii inaishi vyema.

“Haya mambo yana mihemko mingi, huwezi chezea masuala ya kidini kwa kisingizio cha sheria, kama kiongozi lazima ujiongeze na kuhakikisha huwi sehemu ya kuongeza migogoro katika jamii,” anasema.

Wakili wa kujitegemea Peter Mshikilwa anasema kinachoonekana ni kwamba kuna tatizo kubwa ndani ya mifumo ya utendaji.

“Watendaji hawajui wajibu wao; mfano makanisa pia yanasajiliwa ofisi ya Kabidhi Wasii. Taasisi zote hizi ni za Serikali hivi kweli hakuna ‘consultation’ (mashauriano), hapo kuna kasoro kubwa katika utendaji wao.

Mshikilwa anasema kinachopaswa kufanyika sasa ni kwa wahusika kujipanga, waelewe majukumu yao ili kuepuka sintofahamu, hasa inapofika masuala ya kidini.

“Masuala haya yanahitaji uangalifu mkubwa, Uliyafanyia kazi vibaya yanaweza kuleta madhara na kusababisha mpasuko mkubwa kwa jamii,” alisema.

Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano, uenezi na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema anasema tukio hilo ni dalili kwamba serikalini hakuna ‘coordination’ ndiyo maana kila mmoja anafanya yake.

“Hatutaki kuamini jambo kubwa kama hili halijapita na kupewa baraka za Baraza la Mawaziri, lakini baada ya kulileta hadharani likawa na madhara makubwa kwa jamii ndiyo wakaona ni bora kuliruka.”

Kwa mujibu wa Mrema, ndani ya Serikali kuna mahali hapaendi sawa na kwamba mfumo wao wa mawasiliano umekatika.

“Ndiyo maana tunaona mtu kama askofu Kakobe leo anahojiwa kuhusu uraia na Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato (TRA), Nondo naye anaojiwa lakini wapo wengi kama akina Bashe wote hao wamehojiwa kutokana na mihemuko tu,” anasisitiza.

“Unakuta kuna jambo la kisiasa linaendelea na baada ya muda mfupi tu unasikia mtu huyo amehojiwa, kuna kitu hakiendi sawa, hapa lazima wajitathimini.”

Mrema anaongeza kuwa watendaji hao kwa sasa hawaongei lugha moja lakini pia akataadharisha kuwa hakuna mtu au kikundi chochote kilicho salama kwa mwenendo huo, akitahadharisha kuwa hata Waislamu wasifikiri hawataguswa.

“Nyaraka za kitume zipo tangu enzi na enzi, Serikali iwe na msimamo iseme inataka kwenda wapi? Je, bado inasimamia kwamba haina deni au sasa wanataka kusimamia mpaka mahubiri yanayotolewa na madhehebu ya dini?

Mrema anawataka watendaji kujitathimini utendaji wao na wajifunze kutokana na makosa yaliyowahi kufanywa na wenzao.

“Mfano tumeshuhudia Shirika la nyumba (NHC) likibomoa jengo lililokuwa Klabu ya Billcanas lakini sasa kiko wapi, matokeo yake kuna watu waliotolewa kafara.”

Anasema mtendaji anapaswa kuwa makini na utekelezaji wa maigizo ya wakubwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo badala ya kutekeleza ya wanasiasa na jambo linapoharibika huachwa peke yake.

Chanzo: mwananchi.co.tz