Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jeneza la Askofu Chengula lasababisha vilio uwanja wa ndege Songwe

28965 Askofu+pic TanzaniaWeb

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Vilio na simanzi vimetawala Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA) jijini Mbeya baada ya waumini wa Kanisa Katoliki na wananchi kulipoliona jeneza lililoubeba mwili wa aliyekuwa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Mhashamu Evarist Chengula liliteremshwa katika ndege.

Mwili wa Askofu Chengula umewasili uwanjani hapo saa 8:20 mchana ukitokea jijini Dar es Salaam na kupokewa na umati wa watu waliojitokeza, ukiongozwa na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila na viongozi mbalimbali wa Serikali na madhehebu ya dini, taasisi na mashirika ya umma.

Baada ya mwili wa Askofu Chengula kuteremshwa na kubebwa na mapadri walioandaliwa, vilio vilitawala huku kwaya mbalimbali zikiimba nyimbo za kuomboleza.

Kabla ya kuondoka uwanjani hapo, yamefanyika maombi maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kuwafikisha salama jijini Mbeya, maombi ambayo yamedumu kwa takribani dakika 20 yakiongozwa na Makamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Francis Magala.

Viongozi wa Serikali waliofika kuupokea mwili wa Askofu Chengula ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, Wakuu wa Wilaya za mkoani hapa, Mbunge wa Mbeya Mjini, (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu 'Sugu’.

Baada ya maombi kumalizika, msafa ulikwenda yalipokuwa yameandaliwa makazi yake ya kudumu baada ya kustaafu rasmi askofu wa eneo la Shewa nje kidogo ya jiji la Mbeya.

Mapema leo asubuhi Jumatatu, Rais John Magufuli ameungana na waombolezaji wengine kutoa heshima za mwisho kwa Askofu Chengula katika misa iliyofanyika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam.

 

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz