Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Je, Maaskofu wa Afrika wana uwezo wakugomea maelekezo ya Papa?

Afya Ya Papa Francis Yaimarika Baada Ya Kulazwa Hospitalini Usiku Je, Maaskofu wa Afrika wana uwezo wakugomea maelekezo ya Papa?

Tue, 26 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hivi karibuni kumeibuka mjadala mkubwa Ulimwenguni ambao kwa namna moja au nyingine unaonekana huenda ukaligawa Kanisa Katoliki Duniani, ingawa kuligawa au kutoligawa Kanisa hilo kunategemea na mapokeo ya mjadala husika na mapokeo ya Waumini kwenye suala hilo. Hivi karibuni Papa Francis alitoa tamko au somo lililohusu 'Baraka' na hasa ikilenga baraka ambayo waumini wanakwenda kuiomba na kuipokea kutoka kwa Viongozi wao wa Kiroho, mapokeo ya somo hilo ndio yaliyoibua mjadala unaendeleaje Ulimwenguni kwa sasa

Kwenye andiko langu hapa sitajikita kuliangalia andiko kama lililenga nini hasa, lakini nitajikita kueleza tafsiri 'tata' iliyoko kwenye suala hili, tafsiri inayoendelea ni kwamba Papa Francis pengine ameruhusu na kutia Baraka kwa Wapenzi/ Wanandoa wa Jinsia moja (Mashoga na Wasagaji) na hapo ndipo suala hili linapoonekana kutaka kuligawa Kanisa, wapo wanaoamini Papa Francis hakuwa sahihi kuzungumza hoja hiyo ambayo inaashiria kuunga mkono watu wa aina hiyo, wapo wale wanaoamini kuwa Papa Francis ametafsiriwa vibaya kwenye tamko lake na kwamba alichokilenga na kinachotafsiriwa ni vitu viwili tofauti, lakini hapa wapo wale walioko katikati ya mjadala na hawajuwi wapokee lipi kati ya hayo mawili, kwa kuwa kwa bahati mbaya au nzuri wanaotolea tafsiri hizo zenye mitazamo tofauti wote ni Viongozi wa Kiroho tunaowaamini, kuwaheshimu na kuwapenda zaidi

Ukifuatilia kwa karibu utagundua kuwa mjadala huu umekuwa gumzo kubwa Afrika na si maeneo mengine ya Ulimwengu, sio kwamba nje ya Afrika haujadiliwi la hasha ila 'moto' unakolea zaidi Afrika, kwa nini?

Mataifa mengi ya Ulaya, Amerika na hata Australia yanaonekana kuunga mkono agenda hiyo inayotajwa kuwa kinyume na maagizo ya 'Mungu', tumeshuhudia hata Viongozi wa Serikali za Mataifa hayo wakiruhusu ndoa za wasagaji na mashoga

Tukirejea kwenye mjadala wa msingi, hapa kwetu Tanzania napenda niwatolee mfano Maaskofu wawili tofauti ambao wanaonekana kutofautiana kwenye tafsiri ya suala hili, wa kwanza ni Askofu Mkuu Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Askofu Jude Thaddaeus Ruwai'chi yeye ameonesha wazi 'kumtetea' Papa Francis licha ya kwamba aliweka wazi kuwa msimamo wake hawezi kubariki Mashoga na Wasagaji kwa sababu hakuna baraka inayopingana na mafundisho ya msingi, lakini anaamini Papa Francis ametafsiriwa vibaya na Jamii hasa ya Watu wa mitandaoni

Askofu Ruwai'chi ameenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa suala hili linakuzwa na wale wasiolitakia mema Kanisa Katoliki, ametumia hoja hizo kuhoji kuwa mtu yeyote anayekuja kuomba baraka ni ngumu kumjuwa kama ni shoga/ msagaji au la,

Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Askofu Flavian Kassala akihutubia katika Misa ya Kitaifa ya Krisimas amesema kwake ni bora abariki jiwe lakini sio Mashoga/ Wasagaji, ingawa hakuna sehemu yoyote ya somo lake alipozungumzia kuwa anajibu tamko la baraka lililotolewa na Papa Francis, lakini kwenye mazingira ya kawaida inadhaniwa kuwa tamko hilo limekuja wakati huu mjadala kuhusiana Mashoga/ Wasagaji kupewa au kutopewa baraka ukiwa umeshika kasi Duniani na hasa ndani ya Kanisa Katoliki, hao ni Maaskofu wawili tofauti walioko kwenye Kanisa Katoliki hapa Nchini, ingawa hadi sasa hakuna tamkoa lolote la pamoja la Baraza la Maaskofu wa Kanisa hilo hapa Nchini lililotolewa kuhusiana na mjadala huo,

Desemba 19 mwaka huu Baraza la Maaskofu Katoliki Nchini Malawi (ECM) lilitoa tamko la pamoja lililoonesha kupinga tamko la Papa Francis, nje ya Malawi Mabaraza kama hayo katika Nchi za Zambia na Kenya nayo yametoa tamko linalopingana na hoja za Papa Francis

Nchini Zambia andiko lao limeenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa kile kilichozungumzwa na Papa Francis hakiko sahihi na hakipaswi kuungwa mkono,

Hiyo ni mifano michache kati ya mingi inayoendelea Barani Afrika kuhusiana na tamko la Papa Francis la kuruhusu Makasisi kuwapa baraka wapenzi walio kwenye mahusiano ya jinsia moja; Swali linalotatiza kwenye vichwa vya watu wengi hadi sasa ni Je, Maaskofu wa Afrika wana nguvu ya kugomea maelekezo ya Papa?

Chanzo: www.tanzaniaweb.live