Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Imani zisikwamishe kazi bali zichochee

Kazi Picha Dta Imani zisikwamishe kazi bali zichochee

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Siku nne zilizopita Watanzania walifungua kalenda ya mwaka 2023 kwa salamu za uhusiano wa Mungu na kazi, ikiwa ni miaka 45 imekata tangu Taifa lililoidhinisha kikatiba uhuru wa imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake chini ya ibara ya 1977(19)(1).

Salamu hizo zilitolewa kwa Wakristo wote nchini na Msaidizi wa Askofu Kanisa Kuu la KKKT, Azania Front Jijini Dar es Salaam, Chediel Lwiza katika ibada ya mkesha wa kuaga mwaka 2022 katika kanisa hilo. Hoja hiyo inagusa Wakristo na Waislamu waliokosa maarifa ya kutafsiri ujumbe wa Mungu kuhusu kazi 2023.

Msingi wa hoja hiyo unatokana na wimbi la waumini wengi kuamini mafanikio na miujiza inapatikana kwa kuomba na kufunga misikitini au kanisani, hatua inayozalisha kundi kubwa la Watanzania tegemezi na kuibua migogoro ya uchumi wa ngazi ya kifamilia, kijamii na kitaifa.

Hata hivyo, kwa ushahidi wa kibiblia, Mwenyezi Mungu alifanya kazi ya kuumba dunia na vilivyopo kabla ya kupumzika siku ya saba. Akampatia sharti mwanadamu kufanya kazi siku sita na kumuabudu siku moja ya mapumziko. Pia akaagiza asiyefanya kazi na asile, uvivu ni dhambi na kutobariki wavivu.

“Neno la Mungu linatueleza pia kazi ni amri, sio jambo la hiari yako (Mkristo), Kanisa la Wathesalonike walikuwa na shida ya tafsiri kuhusu Yesu kurudi mara ya pili, hivyo hawafanya kazi wakidhani atarudi wakati wowote, hatua iliyowafanya kushindwa kuwajibika katika familia na Taifa lao,” anasema Lwiza.

Kwa ushahidi wa Quran, Mwenyezi Mungu anampenda mja mwenye kufanya kazi na yeyote mwenye kuhangaikia familia yake anakuwa ni kama anayepigana jihadi katika dini.

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda anasema changamoto iliyopo ni baadhi ya waumini kuamini dini ni kuingia msikitini kuswali na kufunga.

“Dini ni mfumo wa maisha kwa ujumla, Mtume Muhammad alifanya biashara ndani na nje ya nchi. Katika mafundisho yake, kazi imepewa nafasi ya juu, sasa mitazamo kwa wasioelewa wanadhani unapata riziki kwa kushinda msikitini, ni lazima tufanye kazi ili kutoa zaka pia,” anasema Sheikh Ponda.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara, Dk Donath Olomi anasema hakuna Taifa lolote duniani lililoendelea kiuchumi kwa maombi bila kazi, akishauri itolewe elimu ya umuhimu wa kazi kuanzia ngazi ya shule za awali, msingi hadi vyuoni, makanisani, misikitini kila ibada na iwepo kaulimbiu ya kitaifa.

Mfano baada ya uhuru wa Tanganyika kuna kauli mbiu zilitumika ili kuhamasisha wananchi kufanya kazi, mfano uhuru na kazi, kilimo ni uhai pamoja na Hapa Kazi Tu, kila mtu ahamasike kufanya kazi,” anasema Dk Olomi.

Anasema tafsiri isiyo sahihi kuhusu kazi inaendelea kutishia uchumi wa Taifa. Dk Olomi anatumia mfano wa misingi wanayojengewa wanafunzi wa shule za seminary za Kanisa Katoliki kupitia kaulimbiu ya kusoma, kazi na sala, huku Shirika la Kimataifa la Opus Dei likihamasisha kazi na sala.

Msajili wa Jumuiya kutoka wizara hiyo, Emmanuael Kihampa alipotafutwa ili kueleza mipango na tathmini ya athari hizo kwa Taifa hakupokea simu wala kujibu meseji, huku Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini akiomba atafutwe waziri mwenye dhamana ambaye pia hakupatikana kwa simu yake.

Maagizo, athari

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, idadi ya madhehebu na misikiti inazidi kuongezeka kwa kasi, huku wadau wakieleza umuhimu wake katika kupunguza matukio ya uhalifu na baadhi wakitafsiri kama biashara iliyoingia kwa mgongo wa kupotosha na kutapeli wananchi kwa kivuli cha umaskini wao.

Licha ya kutopata takwimu za madhehebu na misikiti nchini, takwimu za wizara hiyo zinaonyesha hadi kufikia Machi 2021 jumla jumuiya za kidini 992 zilikuwa zimesajiliwa nchini, huku Serikali ikisuluhisha migogoro tisa kati ya 11 kutoka jumuiya za kidini kati ya Julai, 2020 hadi Machi, 2021.

Katika sehemu ya mafundisho yake ya kufunga mwaka 2022, Lwiza anasema kazi ni suala la imani linalounganisha mahusiano ya Mungu na mwanadamu.

“Mkristo goigoi, mvivu, mzembe asiyefanya kazi huyo hana imani. Siku hizi katika makanisa yetu, inaonekana tunazalisha Wakristo wavivu. Wakristo wanaaminishwa yale ambayo hata Mungu hakutuaminisha. Makanisa yanajaa maeneo mengi lakini wanaaminishwa kutokufanya kazi,” anasema.

“Sasa Wakristo wenzangu mwaka mzima unakuta wanatembea na chupa za maji, majivu, mafuta, picha za mitume na manabii. Mungu hamsikilizi mtu mvivu, haijawahi kutokea na haitatokea mahali popote. Baraka, miujiza na mafanikio yako yapo katika kazi.”

Mtazamo huo unatolewa siku chache baada ya huduma za kiroho katika Kanisa la huduma ya The Word of Reconciliation Ministries (WRM), jijini Dar es Salaam la waumini zaidi ya 4,000 kufungwa, huku ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi ukiimarishwa kwa madai ya ukiukwaji wa sifa za kisheria.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini idadi kubwa ya waumini wa madhehebu wamekuwa wakitumia muda mwingi katika ibada katika siku za juma, licha ya kutokuwa na ushahidi wa vyanzo vya mapato yao.

Matokeo ya utafiti wa Hali ya Nguvu Kazi nchini mwaka 2021 chini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS), yanayoonyesha uwepo wa asilimia tatu ya kushuka kwa ushiriki wa nguvu kazi katika kipindi cha miaka minane iliyopita(2014-2021) kutokana na sababu mbalimbali.

Pia matokeo hayo yanaonyesha kushuka kwa masaa ya kufanya kazi kwa wafanyakazi wanaolipwa kutoka masaa 58 kwa wiki mwaka 2014 hadi masaa 57 mwaka jana. Je kuna uhusiano wowote na watu kutumia muda mwingi kuabudu makanisani na misikitini?

“Hapana, muislam mwaminifu anajali muda wa ajira yake, ni dhambi kutumia muda wa mwajiri isiyo halali, sasa wanaoshinda misikitini mara nyingi tunaendelea kuwaelimisha, na kuna misikiti mingine huwa inafungwa baada ya ibada ili kuwaondoa wote,”anasema Sheikh.

“Quran inanukuu kwamba “Mkimaliza kuswali Alfajiri msilale mkaacha kwenda kutafuta riziki zenu(kutafuta kazi),”ananukuu.

Chanzo: Mwananchi